Makala

Kwa nini wenza wanaibiana fedha?

Telegram

Hivi unajua sheria ipo wazi kwa anayeiba kitu cha mtu? Adhabu yake endapo atapatikana na hatia ni kifungo kisichopungua au kisichozidi miaka mitano hadi saba jela.

Lakini hilo linaonekani halitiliwi maanani katika jamii, wakiwamo wanandoa kutokana na kuibiana fedha zinazokuwa zimehifadhiwa na mmoja kati yao.

“Nililazimika kuficha hela zangu juu ya bati, kutokana na mke wangu kuwa na tabia ya kuziiba, ikizingatiwa sina kipato cha hivyo cha kusema nikazihifadhi benki au kwenye mitandao.”

Hiyo ni kauli ya Rashid Abdulkarimu, mkazi wa Tanga aliyoitoa wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu madai ya wenza kuibiana fedha.

“Ukweli ukizihifadhi benki au kwenye simu wakati unapozihitaji lazima kuna makato, jambo ambalo siliwezi, ndiyo maana nazihifadhi nyumbani ili napozihitaji iwe rahisi kuzipata, lakini ndio hivyo, napata changamoto ya kuibiwa na mke wangu,” anasema Abdulkarimu.

Mkazi mwingine wa Dar es Salaam, Abiudi Jonathan anasema alihifadhi fedha zake chini ya godoro Sh150,000 kwa ajili ya kutoa kwenye mchezo wao wa kila mwisho wa mwezi.

Hata hivyo, anasema siku ilipofika na kwenda kuzichukua, hakuziona na ndani wanaishi yeye na mkewe, kwa hiyo alijua ni yeye alizichukua, japo alipomuuliza alikataa.

Mwajabu Semvua, mkazi wa Arusha anasema alijichangisha hela kwa ajili ya kununua kiwanja kutokana na kuchoka kuishi katika nyumba za kupanga.

Anasema ilipofika Sh2 milioni, mume wake aliyeishi naye kwa zaidi ya miaka 12, alimwibia na hapo ndio ikawa mwisho wa uhusiano wao.

Mwajabu anasema awali ilikuwa kila anapomwambia mumewe suala la kununua kiwanja hachangii chochote, hivyo akaona ajichange mwenyewe kupitia kazi yake ya mama lishe anayoifanya, lakini kitendo cha kumwibia akaona kama hana nia njema naye ya kuleta maendeleo katika familia.

Ziada Abdulkarim anasema kutokana na kumuamini mume wake, alimpa hadi nywila ya kadi ya benki, kumbe alikuwa akienda kuchukua fedha bila kumtaarifu na siku alipokwenda kutoa akakuta akaunti inasoma sifuri na hakuna cha maana alichoona amefanya katika fedha hizo zilizokaribia Sh5 milioni.

Mkazi mwingine ambaye hakutaka kuandikwa jina lake, anasema: “Mimi kiukweli nilikuwa namchomolea mume wangu hela, kwa kuwa hakuwa akitaka kufanya maendeleo yoyote, fedha hiyo ilinifanya nijenge bila ya yeye kujua.”

Hizi ni baadhi ya simulizi zilizotolewa na wenza, namna wanavyoibiana fedha ndani ya nyumba.

Hata hivyo, mwandishi wa Jarida la Familia amefanya mahojiano na baadhi ya wachumi, wanasaikolojia na wanasheria waliozungumzia suala hilo na kuelezea kinachosababisha na namna ya kutibu tatizo.


Kiuchumi imekaaje?

Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kiyondo anasema mantiki ya mwenza kumwibia mwenzie haikai vizuri, isipokuwa anachokiona ni kuchukua kitu bila kutoa taarifa.

Profesa Kiyondo anasema mnapoamua kuwa wenza ni wazi kila mnachokitafuta ni kwa ajili yenu wote, hivyo ndiyo maana inamuwia vigumu kusema wenza wameibiana. “Mwenza wako akichukua Sh1,000 au Sh2,000 akaitumia sio mbaya, hawa watu ni mwili mmoja, hivyo wakitumia hela yao pamoja ni kitu kizuri,” anasema Profesa Kiyondo.

“Isitoshe, mwanamume anayejielewa hela yake ikitumiwa na mwenza ni fahari na mwanamke kwa dunia iliyopo leo, akimtoa mwanamume wake out kidogo ni fahari pia,” anasema mtaalamu huyo.

Nini kifanyike?

Hata hivyo, anatoa angalizo kwa wenza wanapochukuliana hela kinachofanyika kionekane kwa macho.

Anasema hiyo itaweka uwanja mpana wa kujadiliana na kuonyana pale hela ilipotumika ndivyo sivyo na wakati mwingine asirudie kufanya hivyo, kwa kuwa uliitenga fedha kwa ajili ya kufanyia jambo fulani.

Akielezea namna uchumi wa ndani ulivyo, Profesa Kiyondo anasema wenza wanaweza wakawa na akaunti tofauti za kuhifadhi fedha, wanafanya kazi tofauti na vipato vikawa vinatofautiana.

“Lakini mnapoingia ndani ya nyumba utofauti wa kazi zenu mnapaswa kuuweka pembeni, mnashirikiana katika vipato vyenu, bila kujali wewe ni profesa na mwenza wako ni mfanyabiashara ndogondogo,” anasema mtaalamu huyo wa uchumi.

Akielezea kuhusu mwenza kuficha fedha maeneo mbalimbali ya nyumbani ilimradi zisionwe na mwenzake, Profesa Kiyondo anasema hayo ni makosa makubwa kwa kuwa kufanya hivyo sio tu unamkomoa mwenzako, bali unajikomoa na wewe.
Anasema kuna wakati unaweza ukasahau hata ulipoziweka fedha zako au zikachukuliwa na mtu mwingine ambaye wala hahusiki na familia yenu.

“Yaani haitakiwi kuwa shida hela yako kutumiwa na mwenza wako, isipokuwa ni kuambiana tu unapohitaji hela au unapochukua uniambie,” anasema Profesa Kiyondo.

“Mnapaswa kuitumia hela mnayoitafuta kwa maendeleo ya familia yenu, hata kama mke kanunua kiatu kizuri kwa hela uliyoitafuta ni sawa, maana hata watakayemuona kapendeza wataulizana huyu ndiye mke wa fulani.

“Vivyo hivyo na kwa mwanamume, anaweza kununua suruali au shati likampendeza na akasifiwa, hivyo itakuwa sifa kwa mwanamume anapoulizwa huyu ndio mume wa fulani.

“Lakini ni mbaya pale mwenza hasa mwanamume anapochukua hela na kwenda kula raha na kimada, jambo ambalo baadaye linasababisha kuleta mfarakano ndani ya nyumba,” anasema Profesa Kiyondo. “Wakati mwingine unakuta mwanamke kaingia vikoba na mikopo mbalimbali ya kausha damu kupitia hela aliyoichukua kwa mumewe pasipokujua hadi kuja kuuziwa nyumba au kuchukuliwa samani za ndani.”

Profesa Kiyondo anasema zipo sababu za wenza kuibiana, ikiwamo baadhi huchomoa fedha zao kama wanazichungulia wakati wanapoombwa.

“Hauwi muwazi nazo kwa mwenza na mbaya zaidi ni kuishi mke na mume kama unaishi na jirani yako au mpangaji mwenzako, hivyo kunakuwa hakuna yale mapenzi ya kweli na uwazi,” anasema Profesa Kiyondo.

“Kama angekuwa anaziona zote kila wakati ingesaidia, kwa kuwa hata zinapopungua angejua zimepungua na kuogopa wakati mwingine kuzichukua.”
Hata hivyo, Profesa Kiyondo anasema wenza wanaoamua kuhifadhi fedha nyumbani, inachangiwa na mambo mbalimbali, ikiwamo elimu ndogo au elimu kubwa na wengine wana sababu za msingi kabisa.

“Mfano kwa mtu mwenye sababu za msingi utakuta fedha zake ni za mzunguko kama wale wanaouza bidhaa fulani zinazohitajika kununuliwa kila wakati.
Lakini kuna wale hela yao kuipata sio ya muda maalumu, anaweza kuipata leo ikapita hata miezi mitatu minne bila kupata nyingine,” anasema Profesa Kiyondo.
Pia, anasema watu wa aina hiyo wanapaswa kuwa na vifaa maalumu vya kuhifadhia fedha, ikiwamo ‘safe’ ambayo huwa ina nywila za kufungulia na haifungukia hata ikiibwa au kuungua moto.

Je, ni tatizo la saikolojia?

Mwanasaikolojia maarufu, Aunt Sadaka anasema tabia ya kuibiana hela sio kwa wenza waliooana tu, bali hata wachumba au wapenzi.
Sadaka anasema kwenye saikolojia tabia hiyo inapoteza uaminifu na kuweza kuvunja uhusiano hata kwa Sh10,000, jambo ambalo halipendezi kama kweli mnapendana.

“Kuna wakati kweli unaweza ukawa umechukua hiyo hela, lakini nikikuuliza umeifanyia nini ukashindwa kunipa majibu, nitabaki najiuliza umeenda kuhonga, umeenda kujenga kwenu au nini,” anasema Sadaka.

“Kwa tabia za namna hii ni wazi kuwa anayepewa hela na anayetoa hela kila mmoja atamuogopa mwenzake na mwisho wa siku kuvunja uaminifu na kukaribisha umaskini katika familia.”

Alipoulizwa nini kifanyike kwa wenza waliofikia hatua hiyo, Sadaka anasema ni muhimu wenza kuwa na muda wa kuongea kuhusu tabia zao katika masuala ya fedha.

“Kuna matatizo ya kisaikolojia, hasa watu waliopitia wimbi la umasikini na anapozipata hutumia kwa fujo kama njia ya kuponyesha vidonda kwa yale aliyopitia katika maisha yake,” anasema Sadaka.

Pia, anasema wapo wanaoiba fedha kwa wenza wao kutokana na ubahili, hivyo wanapoziona wanaona njia sahihi ni kuzichukua tu.

“Hilo nalo ni tatizo, anachokiona kwa wakati huo ni kuwa hathaminiwi, hivyo anaona ajithaminishe na vitu vya watu. Hii tabia ya wenza kuibiana sio kitu cha kawaida na ni ya kukemewa kwa nguvu zote, haiwezekani mpenzi wako, mke au mume wako unamwibia au unamtapeli kuwa akupe hela ili ukanunue kitu fulani cha thamani halafu hufanyi hivyo, sio jambo zuri,” anasema Sadaka.

Hata hivyo, anasema kwa walio katika uhusiano, unapozungumzia uchumi wako unazungumzia hela yako mwenyewe, lakini linapokuja suala la uchumi wa familia unazungumzia hela yako na ya mwenzako, “hivyo ni muhimu kuwa nazo makini katika matumizi yako kwa faida ya pande zote mbili.”

Hatua gani za kuchukuliwa kisheria?

Mwanasheria Abdulghafar Marijani anasema kuchukua kitu cha mtu bila kumwambia inatafsiriwa ni wizi kama wizi mwingine kisheria, isipokuwa hilo linapokuja katika familia ya mke na mume au watu walio katika uhusiano inachukuliwa kivingine.

“Kama sio kuogopa maneno ya wake na ndugu wa mwenza wako, nahisi wengi wangepelekana mahakamani kutokana na tabia hizi za wenza kuibiana,” anasema Mwanasheria Marijani.

“Sema ndio hivyo, ukiwaza ndugu watakavyokuchukulia na wakati mwingine tayari mna watoto unaona madhara yatakuwa mabaya zaidi kuliko faida, hivyo huoni haja ya kulifikisha hili kwenye vyombo vya sheria.

“Japokuwa sheria ipo wazi kwa anayeiba kitu cha mtu, adhabu yake endapo atapatikana na hatia ni kifungo kisichopungua au kisichozidi miaka mitano hadi saba jela na faini au vyote kwa pamoja kutegemeana na uamuzi wa hakimu,” anasema Marijani.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi