Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umeomba Sh8 bilioni kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umeme ili biashara katika eneo la Kariakoo ifanyike kwa saa 24.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila katika mkutano mkuu wa mwaka wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC).
Fedha zinazoombwa alisema ni pamoja na za kubadilisha nyaya, kwa kuwa zilizopo ni za zamani, kufunga swichi za kielektroniki ili umeme utakapokatika eneo hilo uendelee kuwaka.
Mbali ya hilo, alisema wiki ijayo watakutana na wadau mbalimbali kuangalia namna watakavyoweza kufanya biashara hiyo.
Wakati huohuo, Makamu Mwenyekiti wa Machinga Tanzania, Steven Lusinde amesema licha ya viongozi wa Serikali kutoa ahadi za kuwaboreshea mazingira na miundombinu ya kufanya shughuli, suala hilo limeendelea kuwa shubiri kwao.
Alisema kundi hilo lenye watu wengi limekuwa likitumiwa zaidi na wanasiasa kwa masilahi yao binafsi, huku wakiachwa wakipata shida.
Alisema hayo jana, kwenye kongamano la wamachinga Wilaya ya Kinondoni, lililoandaliwa na taasisi za Vijana Imara Organization na Hatua kwa Hatua.
Hata hivyo, madai hayo yalijibiwa na Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dk Nandela Mhando aliyesema kundi hilo lipo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, ambayo inaendelea kushirikiana na sekta nyingine kuona mahitaji yao yanapatiwa ufumbuzi.
“Mmeeleza changamoto nyingi tutazishughulikia, ikiwemo mazingira ya kufanya shughuli zenu. Nitoe maagizo kwa wakurugenzi kuendelea kuwahusisha kwenye shughuli za upangaji miji na maeneo yanayoanzishwa masoko ili yajengwe maeneo yaliyo rafiki kwenu,” alisema.
Dk Nandela alimwakilisha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima katika kongamano hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule alisema Serikali inaendelea kuboresha masoko na katika wilaya hiyo imejenga manne, yakiwamo ya Tandale lenye thamani ya Sh12 bilioni na Mwenge (thamani ya Sh9 bilioni).
Akizungumzia DCPC, Chalamila alisema mkoa unawategemea katika kufanya maendeleo, ikiwamo kumpa ushauri wa nini wangependa kuona kinafanyika ili mkoa uwe wa kuvutia.
Katika hatua nyingine, Chalamila alipokea tuzo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, iliyotolewa na DCPC ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuboresha tasnia ya habari.
Akieleza sababu ya kumpa Rais Samia tuzo hiyo, Katibu wa DCPC, Fatma Jalala alisema chini ya utawala wake, amefanya maboresho mbalimbali, ikiwemo kuiunganisha Wizara ya Habari na Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kuleta tija na ufanisi.
“Ametimiza ahadi ya kurekebisha sheria ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 2016 na tunaamini ataendelea kuiboresha ili kukidhi mahitaji ya wadau na kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji,” alisema Fatma.
Akimkaribisha Chalamila, Makamu Mwenyekiti wa DCPC, Salome Gregory aliahidi klabu hiyo kuendelea kumpa ushirikiano pamoja na ofisi yake ili kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa na mkoa na Taifa kwa ujumla.
Kuhusu DCPC
Akizungumzia DCPC, Chalamila alisema mkoa unawategemea katika kufanya maendeleo ikiwamo kumpa ushauri wa nini wangependa kuona kinafanyika ili mkoa uwe wa kuvutia machoni mwa watu na kuutofautisha na mingine.
Chalamila alikubali kuwa mlezi wa klabu hiyo baada ya kuombwa na DCPC.
Apewa tuzo ya Rais Samia
Katika hatua nyingine, Chalamila alipokea tuzo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, iliyotolewa na DCPC ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuboresha tasnia ya habari.
Akieleza sababu ya kumpa Rais Samia tuzo hiyo, Katibu wa DCPC, Fatma Jalala alisema chini ya utawala wake amefanya maboresho mbalimbali ikiwemo kuiunganisha Wizara ya Habari na Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kuleta tija na ufanisi.
“Ametimiza ahadi ya kurekebisha sheria ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 2016 na tunaamini utaendelea kuiboresha ili kukidhi mahitaji ya wadau na kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji,” alisema Fatma.
Akimkaribisha Chalamila, Makamu Mwenyekiti wa DCPC, Salome Gregory, aliahidi klabu hiyo kuendelea kumpa ushirikiano pamoja na ofisi yake ili kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa na mkoa na Taifa kwa ujumla