Kitaifa
Samia kuzindua ripoti utafiti wa afya leo
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 28, 2023 anatarajiwa kuzindua Ripoti Kuu ya Utafiti ya Afya ya Uzazi na Mtoto na viashiria vya malaria ya mwaka 2022.
Ripoti hiyo itakuwa dira ya nchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ikitumika katika sekta ya afya kupanga mahitaji na mipango mipya katika kushughulikia masuala ya afya nchini hususan mama na mtoto.
Tafiti hii huongoza kwenye tathmini ya uwajibikaji katika kutatua changamoto za utoaji wa huduma za afya uzazi kwa kupima viashiria vilivyopo na jinsi tulivyofikia malengo ya utoaji wa huduma bora za afya ya uzazi pamoja na kupunguza au kuondokana na athari zitokanazo na changamoto za afya ya uzazi.
Tafiti hii hufanyika nchini kila baada ya miaka mitano kupitia Ofisi za Mtakwimu Mkuu wa Tanzania Bara na Zanzibari kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pande zote mbili na Ofisi ya Rais Tamisemi pamona na wadau ambapo Ripoti hutoa dira juu ya hali halisi ya utolewaji wa huduma za afya ya uzazi na mtoto.
Sambamba na uzinduzi wa Ripoti hii Rais Samia anatarajiwa pia kuzindua magari ya kubebea wagonjwa, magari ya usimamizi pamoja na kugawa vifaatiba nchi nzima.