Kitaifa
Mashirika ya umma 19 kufumuliwa
Dar es Salaam. Mchakato wa kuyafumua mashirika 19 ya umma umeiva na ndani ya muda mfupi ujao yatawekwa wazi, imefahamika.
Uamuzi huo wa Serikali ambao bila shaka unawaweka mabosi wa mashirika hayo matumbo joto, umelenga kuunganisha baadhi ya majukumu ya taasisi hizo hadi kubaki na saba.
Uamuzi huo unafanyika ikiwa ni miezi miwili tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoagiza yafanyike mageuzi katika mashirika na taasisi hizo ili kuongeza ufanisi na kuchangia kukuza uchumi wa nchi.
Mkuu huyo wa nchi alitoa maelekezo hayo Agosti 19, mwaka huu jijini Arusha katika kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma.
Hata hivyo, alielekeza kabla ya kufikiwa uamuzi wa kufuta au kuyaunganisha mashirika na taasisi hizo, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji zinapaswa kukutana nayo.
“Nendeni mkawasikilize kabla ya kutoa maamuzi, kama wakiwashawishi kuwa wanaweza kuboresha utendaji kazi wao basi watazamwe,” alisema Rais Samia siku hiyo.
Katika utekelezaji wa maelekezo hayo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu aliliambiwa Mwananchi jana, kuwa ofisi yake imeshakutana na mashirika mengi kati ya yale iliyopaswa kukutana nayo kwa ajili ya mazungumzo na tathmini.
Kutokana na hilo na kwa tathmini iliyofanyika, Mchechu alisema uamuzi umeshafanyika wa kuyaunganisha mashirika 19 na katika hayo yatabaki saba.
“Kuna ambayo tayari tumeshaamua kuyaunganisha, ni mashirika 19 yataunganishwa na kubaki saba,” alisema Mchechu bila kuyataja mashirika hayo kwa sababu alizosema ni za kiutendaji.
Uamuzi huo, alisema umetokana na sehemu kubwa mashirika hayo ama yalikuwa na shughuli zinazofanana na mengine au kushabihiana.
Kwa mujibu wa Mchechu, kwa sasa hatua za ndani ya Serikali zinaendelea kukamilisha hilo na kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha mashirika hayo yatatangazwa.
Hata hivyo, alisema mikutano ya mashirika mbalimbali ya umma na wahariri wa habari inaendelea, ikiwa ni sehemu ya mashirika hayo kueleza kazi yalizozifanya.
Hatima ya wafanyakazi
Ingawa Mchechu hakutaka kuingia kwa undani, katika hotuba yake ya Agosti 19, Rais Samia alisema kuunganishwa kwa mashirika na taasisi hizo, hakutaathiri ajira za watumishi, akifafanua kuwa asilimia 17 ya ajira ndani ya nchi zinatoka katika taasisi na mashirika ya umma, hivyo hakuna atakayepoteza kibarua chake.
“Wote waliopo kwenye mashirika hayo, ama watapelekwa kwingine au yatakuja mashirika mengine ambayo yana maana zaidi sasa hivi, kuliko wakati yalipoanzishwa na hakuna ajira itakayopotea,” aliwahakikishia.
Itapunguza urasimu
Akizungumzia hatua hiyo, Mhadhiri wa Rasilimali watu na Utawala wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Dk Lazaro Swai alisema uamuzi huo utapunguza msururu wa urasimu na kuongeza tija.
“Kama yalikuwa yanafanya kazi zinazolingana, kuyaunganisha itasaidia kupunguza urasimu na tija itaongeza, kwa sababu kazi fulani itajulikana inafanywa na shirika fulani, hivyo mtu hatalazimika kwenda hapa kisha pale,” alisema.
Lakini, uamuzi huo pia alisema utaipunguzia mzigo Serikali wa kusimamia na kulea mashirika ambayo wakati mwingine hayatakuwa na tija.
“Kuwa na mashirika machache ambayo utakuwa na uwezo wa kuyasimamia na yenye nguvu ni vema zaidi kuliko kuwa na mengi ukashindwa hata kuyafuatilia, watu wanajiamulia nini cha kufanya,” alisema Dk Swai.
Katika utekelezaji wa hilo, mhadhiri huyo aliitahadharisha Serikali isiogope kuwatema watendaji waliokuwa chanzo cha hali duni ya baadhi ya mashirika na taasisi hizo.
“Ukisema unawaunganisha na wengine maana yake unapeleka ugonjwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hawa ambao hawakuwa wasimamizi wazuri, wasipewe nafasi hiyo katika hili lililounganishwa ili ufanisi unaotarajiwa ukapatikane,” alishauri.
Mchawi ripoti
Mzizi wa hoja ya kufutwa au kuunganishwa kwa mashirika ni kauli ya Rais Samia ya Machi mwaka huu, alipopokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ile ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Baada ya kupokea ripoti hiyo, mkuu huyo wa nchi alisema mashirika 14 yanaendeshwa kwa hasara, akiyataja Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Ndege (ATCL) na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC).
Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia alisema kwa muda baadhi ya mashirika yamekuwa yakiendeshwa kwa hasara kwani hayaingizii Serikali chochote. “Kuna haja ya kufanya tathimini kama baadhi ya mashirika ya umma yanafaa kuendelea kuwa nayo, yale yanayofaa yaendelee na yasiyo na tija yafutwe,” alisema.