Kitaifa

Ni kidigitali zaidi, simu kutumika kubaini samaki walipo

Dar es Salaam. Sekta ya uvuvi nchini inakwenda kushuhudia ukuaji mkubwa wa uvuvi kwa siku zijazo.

Hii ni baada ya wavuvi kuanza kutumia teknolojia ya kidijitali kufanya kazi zao za uvuvi katika Bahari ya Hindi.

Teknolojia hiyo inayohitaji mvuvi awe na simu janja, itamsaidia kufahamu maeneo walipo samaki kwa muda huo, hivyo kuondokana na uvuvi wa ‘kuwinda’.

Teknolojia hiyo itumiayo setilaiti itazinduliwa kesho na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko katika maadhimisho ya miaka 40 ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri), yaliyoanza jana na kuhitimishwa kesho.

Akizungumza jana jijini hapa katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Tafiri, Ismael Kimirei alisema utafiti wa mfumo huo ulianza kufanyiwa kazi mwaka 2011.

Kimerei alisema itamsaidia pia mvuvi kutumia kiwango kidogo cha mafuta kwenye boti yake ya uvuvi kulingana na eneo analokwenda.

“Mwaka 2011 ndiyo tulifunga setilaiti ya kwanza, lakini wiki mbili zilizopita tumezindua mfumo wa simu, sasa utaona huu ni mwaka takribani wa kumi wenye faida kwetu,” alisema Kimirei.

Alisema kupitia mfumo huo, wametambua maeneo ya uvuvi na sasa wanaweza kumpatia mvuvi taarifa akaenda kuvua samaki bila kubashiri.

“Mvuvi akituma ujumbe wa simu katika mfumo huu, atapata ujumbe ukimuelekeza mahali palipo na samaki wengi na ni umbali gani atakwenda kwa ajili ya kuwavua,” alisema.

Akizungumzia miaka 40, Kimerei alisema wanaifurahia kwa kuwa idadi ya wavuvi imeongeza kutoka 18 wa awali hadi kufikia 145 waliopo sasa.

Akizungumzia mfumo huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema Tafiri wamefanya mambo mazuri katika sekta ya uvuvi.

Alisema kutokana na ubunifu wa kutumia teknolojia, wamevumbua namna bora ya uvuvi kwa kupitia simu za mkononi, jambo litakalowarahisishia wavuvi kuweka mafuta kulingana na umbali wa safari zao za uvuvi ndani ya maji.

“Lakini, Tafiri waboreshe vivutio vya samaki wengi majini ili wazaliane, wavuvi waondokane na umaskini na waongeze vipato vyao kupitia uvuvi,” alisema Ulega.

Hata hivyo, Ulega alisema sekta ya uvuvi ambayo huchangia pato la Taifa kwa asilimia 1.7 kwa mwaka, inahitaji uwekezaji wa kufuga samaki aina ya sangara katika Ziwa Victoria.

Ulega alisema Sangara ana soko kubwa katika viwanda vingi vya samaki.

“Kwa sasa sangara anauzwa hata kwenye vibanda na mamalishe kutokana na uhitaji wake wa protini, zamani watu hawakuwa walaji wa sangara,” alisema waziri huyo.

Alisema ongezeko la watu lisiwe tatizo katika suala zima la upatikanaji wa samaki, bali liwe fursa katika kutengeneza ajira.
“Tufuge sangara ili aingie kiwandani, kiwanda kimoja kitaajiri zaidi ya vijana 100, hili ndilo eneo ambalo Tafiri mnapaswa kuliwekea mkazo,” alisema Ulega.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Zanzibar (Zafiri), Zakaria Ali Hamis alisema licha ya taasisi yao kutimiza miaka minne tofauti na Tafiri yenye miaka 40, wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano.

“Tunafanya kazi pamoja na tunategemeana uwezo, kwa kuwa wenzetu ni wazoefu tunatumia wataalamu wao pia, tulifanya tafiti Zanzibar kuangalia samaki wadogo ambao karibia unatoka,” alisema Hamis.

Akizungumzia mfumo huo wa satelaiti, alisema utawasaidia wavuvi kujua wapi walipo samaki.

Kwa Zanzibar, mfumo huo ulifanyiwa majaribio na tayari umeshaonyesha matokeo mazuri.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi