Connect with us

Kitaifa

Sura mbili uteuzi Makonda CCM

Moshi/Dar. Uteuzi wa Paul Makonda kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM ndiyo habari ya mjini kwa sasa na wadau wa siasa wametaja sura mbili zinazojitokeza huku wakitaja sifa zilizombeba, ikiwemo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

Wadau hao wanaona kwa aina ya siasa za ushindani Tanzania kwa sasa baada ya kifo cha Rais wa awamu tano, John Magufuli, anayeweza kuwa na mikakati ya kukivusha chama hicho, ni mtu wa aina ya Makonda.

Uchaguzi wa mwakani na mwaka 2025 unatabiriwa kuwa na ushindani mkali, endapo utaendeshwa katika mazingira ya haki, huru na demokrasia.

Mbali na sifa hiyo, kuna hisia kuwa uteuzi wa Makonda kama ulivyokuwa uteuzi wa Dk Doto Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu akishikilia wadhifa pia wa Waziri wa Nishati, unalenga kujenga ushawishi na kukubalika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu, Geita, Kigoma na Tabora ndiyo inayotajwa kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ,inayoweza kuamua hatima ya chama gani kishike hatima ya uongozi katika uchaguzi mkuu.

“Kanda ya Ziwa ni muhimu sana kisiasa. Hata Chadema walifanya mikutano mingi kule na wanakubalika. Hii kwangu naona CCM inataka kujiimarisha na watu kama Makonda na Biteko wanatoka huko wanaweza kuisaidia,” alieleza mwana CCM huyo.

Vilevile, mbali na Makonda na Dk Biteko, Rais Samia pia hivi karibuni alimteua Alexander Mnyeti kutoka kanda hiyo kuwa naibu waziri wa Mifungo na Maendeleo ya Uvuvi.

Kada huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alidai kulikuwa na dhana baada ya kifo cha Magufuli, kanda hiyo iliwekwa kando katika nafasi za uamuzi wa kuona kama kulikuwa na kundi la watu wa Kanda ya Ziwa ambalo lilikuwa halionekani.

Dk Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, Mkoa wa Geita, kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Nishati na kuongezewa unaibu waziri mkuu Agosti 30, mwaka huu alikuwa Waziri wa Madini.

Hivi karibuni, Rais Samia alimpongeza Biteko kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya Wizara ya Madini kwa kuongeza mapato na kuwa ndiyo sababu ya kumpa wadhifa huo.

Hoja ya kuimarisha uungwaji mkono Kanda ya Ziwa, inaungwa mkono na mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe aliyesema uteuzi wa Makonda utatibu changamoto ya makundi na kuleta pamoja mtaji wa wapiga kura kutoka kanda hiyo.

“Inaweza kuwa tiba ya kuua makundi ndani ya CCM na kuleta pamoja mtaji wa karibia asilimia 30 ya wapiga kura kutoka Kanda ya Ziwa,” alisema.

Kulingana na mwanazuoni huyo, makundi ndani ya chama hicho yaliripotiwa zaidi hasa baada ya kifo cha Magufuli Machi 17, 2021 hasa lile lililotajwa kuwa linajinasibu kama wafuazi wa falsafa zake.

“Kundi hili lilijiona lina mtaji mkubwa wa wapiga kura kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa. Hata vyama vya upinzani utakumbuka vimewekeza sana kwenye eneo hili kwa kufanya mikutano mingi,” alisema Dk Kabobe.

Hata hivyo, alijenga hoja hiyo akifafanua kuwa, makundi kwenye siasa si jambo ovu, lakini huwa baya pale linapotaka kukigawa chama husika na kuondoa umoja.

Mrithi sahihi wa Nape

Mbali na mtazamo huo wa Dk Kabobe, baadhi ya makada wa CCM, wanaona hakukuwahi kupatikana mtu wa kuziba nafasi ya Nape Nnauye na Humphrey Polepole.

Polepole aliyeshikilia wadhifa huo kati ya Desemba 2016 hadi Aprili 2021 akipokea kijiti kutoka kwa Nape ambaye kwa sasa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

 Hawa wanatajwa kuwa miongoni mwa waliowahi kuutendea vema wadhifa huo na wanamwona Makonda ni mtu sahihi.

Baada ya Polepole, kiti hicho kilikaliwa na Shaka Hamdu Shaka hadi Januari 14, 2023 CCM ilipofanya mabadiliko na kumteua Sophia Mjema, ambaye amehudumu kwa siku 281 hadi Oktoba 22, 2023 alipoteuliwa Makonda.

“Ukweli ni kuwa tangu Polepole aondoke tulikuwa hatujapata mtu wa kuvaa viatu vyake kwa sababu yeye alikuwa na uwezo wa kujibu hoja za wapinzani kwelikweli. Ngoja tuone Makonda naye,” alieleza kada mwingine wa CCM.

Sifa nyingine inayotajwa kumbeba Makonda ni historia yake ya kisiasa kuanzia akiwa Katibu wa hamasa na Chipukizi ndani ya UVCCM, Bunge la Katiba, mkuu wa wilaya ya Kinondoni na baadaye mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, alionyesha uwezo mkubwa wa kutoa maamuzi, ukiacha makandokando anayohusishwa nayo.

Hata hivyo, wapo wanaoona kuwa kukaa kwake nje kwa karibu miaka mitatu, amepata fura ya kujitafakari.

Hili lilielezwa na mtangulizi wake kwenye uenezi, Nape, juzi muda mfupi baada ya taarifa ya uteuzi huo.

Kupitia mtandao wake wa X, Nape aliandika, “mdogo wangu Paul, karibu sana kwenye uongozi wa juu kabisa wa chama chetu. Nina hakika umetumia vizuri muda wa likizo and now you are ready for the job…

Lakini kutokana na kilichochapishwa na Nape, aliyewahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Fatma Karume alihoji, “Nape mdogo wangu, ina maana CCM haina mtu yeyote wa kuweza kusambaza itikadi zenu isipokuwa Makonda?

“Au hulka ya ubabe za Paulo inaendana na itikadi za CCM? Mnaona Paulo katulia? Si mmempa power (mamlaka) sasa subirini,” alihoji Fatuma ambaye pia ni mtoto wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume

Hoja hiyo ya Fatma ilijibiwa na Nape ambaye ni mbunge wa Mtama, akisema, “nakuelewa shangazi na najua concern (dukuduku) yako but (lakini) mie ni katika wanaoamini kuwa likizo ina mengi ya kujifunza.

“Wengi wetu hupitia likizo kama hizi kwa sababu mbalimbali zikiwemo za udhaifu wa kibadamu. Tusihukumu mapema. Mwenyezi Mungu anatufundisha busara ya second chance in life (nafasi ya pili)!”

Halikadhalika baadhi ya wachambuzi, wanachama wa CCM na wananchi wanamuona Makonda kama mmoja wa viongozi vijana na wenye ubunifu na mikakati na sifa hiyo inaweza kuisaidia CCM katika mipango yake kuelekea 2025.

Ingawa, hawakutaja mikakati hiyo, Makonda aliwahi kuyavuta makundi muhimu yenye ushawishi katika huongozi wake, mfano wamachinga, wanawake waliotelekezwa, wenye migogoro ya ardhi na kutoa vitambulisho kwa walimu ili wasilipe nauli.

Kujibu mapigo

Kujibu mapigo katika hoja zinazoibuliwa na wapinzani hasa kipindi hiki ambacho mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa imeruhusiwa, ni jambo lingine lililompa turufu Makonda katika uteuzi huo kwa mujibu wa Dk Kabobe.

“Namuona Makonda kama kijana na mwanasiasa anayeweza kumudu mikikimiki ya siasa za upinzani hasa kwa nafasi yake ya itikadi na uenezi,” alisema.

Hata hivyo, gazeti hili limedokezwa CCM imeamua Makonda (41), kushika nafasi hiyo kama mtu anayeweza kujibizana majukwaani kwa hoja na makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu anayeonekana kuisumbua CCM.

Mjumbe mmoja wa NEC ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema Lissu amekuwa akimwaga sumu katika mikutano ya hadhara nchini na makatibu uenezi waliomtangulia Makonda, walikuwa ‘wamepoa’ katika kujibizana na Lissu.

Makonda anayo historia ya kukabiliana vilivyo na Edward Lowassa mwaka 2010, mwanasiasa aliyekuwa tishia ndani ya CCM, mashambulizi yaliyompa jina katika medani za siasa.

Hulka ya Makonda kama kiongozi, ni jambo linalotajwa na Dk Kabobe kama sababu ya kuteuliwa kwa mwanasiasa huyo, akifafanua ni kiongozi mwenye uthubutu na asiye na woga.

“Ukichilia mbali tuhuma mbalimbali dhidi yake ambazo hazijawahi kuthibitishwa rasmi, Makonda ni kiongozi mwenye kuthubutu na hana woga hasa pale anapojua mamlaka iko upande wake, ana msimamo kwa anachokiamini hata kama si sahihi kwa watu wengine,” alisema.

Dk Kabobe anasema Makonda ni kiongozi mwenye kutaka kuona matokeo sasa badala ya kesho, hata kama taratibu zilizopo haziruhusu atajitahidi kutumia mbinu mbadala ili aone matokeo.

“Kwa hulka hii, CCM imepata mtu sahihi wa kukabiliana na changamoto za usimamizi wa miradi ya maendeleo iliyoko kwenye ilani ya 2020/25,” alisema.

Lingine lililombeba, kwa mujibu wa Dk Kabobe ni aina yake ya uongozi wa kupenda kazi yake ionekane kwa watu hasa kwa kutumia vyombo vya habari.

“Utakumbuka alipokuwa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitumia sana vyombo vya habari kutatua changamoto za watu hadi wakati mwingine alionekana akipigiwa simu na mamlaka “live” kuonyesha kuwa anachofanya mamlaka inakiunga mkono,” alisema.

Alieleza kazi inayofanywa na CCM inahitaji kutangazwa kwa umma na kama Makonda akiendeleza tabia yake ya kutaka mambo yaonekane, basi uteuzi wake unaweza kuwa sahihi.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi