Connect with us

Kitaifa

Mitazamo tofauti mkataba uwekezaji bandari

Dar/Dodoma. Jana Jumapili Oktoba 22, 2023 mikataba mitatu mahususi ya uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam, miongoni mwa waalikwa katika hafla hiyo alikuwepo Katibu Mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima na Rais wa TEC, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga ambao walishuhudia utiaji saini huo na kisha kutoa maoni yao.

Akizungumza na Mwananchi Digital baada ya tukio hilo, Padri Kitima alisema kwa vitu ambavyo wamevieleza katika mikataba hiyo, maaskofu wanaanza kuridhia na kwamba awali walivyokuwa wakiangalia mikataba mama ilionyesha kuna hali ngumu kidogo.

Alisema kwa sasa kuna maeneo waliyorekebisha na wakayataja, hasa ukomo wa muda wa mkataba, unatathminiwa kila baada ya miaka mitano, kwa hiyo wameona kidogo kuna kitu kimefanyika na DP World hatapewa bandari yote, bali ni sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam aendeshe na afanye kazi kwa ubia wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Alisema maaskofu wameona mkataba huo umefanyiwa kazi baadhi ya vipengele ambavyo vilikuwa na utata mkubwa lakini bado wanasubiri maandishi.

“Maaskofu wanahitaji kuusoma, kusikia tu wameona na walikuwepo watatu kushuhudia tukio na walipoitwa hawakuambiwa kuna nini, lakini walichosikia wameona angalau kuna kusikilizwa kwa maoni ya wananchi na maaskofu walikuwa wanawasemea kwa sababu zile rasilimali za wananchi zilikuwa hatarini,” alisema Padri Kitima.

Alichokisema Padri Kitima kinaungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Bob Wangwe aliyesema ili kujiridhisha na kauli ya Rais Samia kwamba mikataba hiyo imezingatia maoni ya wananchi, ni vema mikataba hiyo ikawekwa wazi.

“Kutokana na aina ya makubaliano au mkataba uliopitishwa bungeni jinsi ulivyokuwa na ulivyotia mashaka na kutengeneza mazingira ya kutowaamini walioupitisha, itakuwa vizuri kama Rais ataiweka wazi mikataba hii ili kutengeneza imani kwa wananchi,” alisema Wangwe.

Alisema kama haitawekwa hadharani, ataamini kile kilichokuwa kimedhamiriwa katika makubaliano ya awali, kimeendelea kwenye mikataba hiyo mitatu.

Hoja hizo zinafanana na za ACT Wazalendo walioongeza sauti wakiitaka kuweka wazi mikataba hiyo mitatu iliyosainiwa jana kwa lengo la kuendesha Serikali kwa uwazi na kuongeza uwajibikaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Janeth Rithe, baadhi ya mapendekezo waliyoyatoa yamefanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kutumika kwa sheria za Tanzania, ukomo na fursa ya kuvunja mkataba.

“ACT Wazalendo tulipendekeza iundwe Kampuni maalumu ya umma itakayoingia ubia na DPW kuendesha shughuli zote bandari, Serikali imiliki asilimia 50 ya hisa zote za ubia. Pendekezo hili pia limechukuliwa,” inaeleza taarifa hiyo.

Akizungumzia kusainiwa kwa mikataba hiyo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) anayemaliza muda wake, Askofu Fredrick Shoo alimpongeza Rais Samia na Serikali kuwa usikivu iliyouonyesha kwa kuzingatia maoni ya Watanzania.

“Kwa kweli kwanza kipekee kabisa nimpongeze Rais na Serikali. Imetufurahisha sana kuona Serikali ni sikivu. Ilipokea maoni mbalimbali na imeyafanyia kazi. Kuanzia ukomo wa mkataba na sasa ni miaka 30 na nini nchi itapata,” alisema.

“Nimepata nafasi ya kusikiliza na yeye mwenyewe amesema Serikali imesikiliza maoni mbalimbali yakiwemo kutoka kwa sisi viongozi wa dini. Mkataba si wa gati zote wala hauhusishi bandari zote. Kwa kweli Rais ameonyesha usikivu.”

Agosti 2023 akiwa katika maadhimisho ya miaka 60 ya KKKT, Askofu Shoo alimweleza Rais kuwa kanisa lina imani naye, kuwa atafanyia kazi maoni ya Watanzania, na kuliendea suala la DP World kwa hekima kubwa ili lisigawe Watanzania.

Mwenyekiti wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed alisema utiaji saini umefanyika baada ya Serikali kusikiliza na kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali.

Mohamed alisema kamati ya majadiliano iliyokuwa ikiongozwa na Dk Hamza Johari imewezesha kuleta majibu ya ukomo wa mkataba kwamba ni miaka 30 badala ya miaka 100, Serikali inaweza kuvunja mkataba na kwamba hakuna ajira itakayopotea.

“Uwekezaji huu utasaidia pia kuwa somo kwa bandari zingine nchini kama Tanga au Kigoma kujifunza namna kuendesha kwa ufanisi,” alisema.

Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo alisema mikataba iliyotiwa saini ni ishara ya kuwajaza mapesa wananchi.

“Mwaka 1995 wakati nagombea urais nilisema sera yangu ni kuwajaza ‘mapesa’ wananchi na huu mkataba umekuja kuwajaza mapesa wananchi,” alisema.

Cheyo aliwataka watendaji kuhakikisha yale yaliyotiwa saini yanafanyika kwa ufanisi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa NCCR Mageuzi (Bara), Joseph Selasini alisema aliitwa kwenye hafla hiyo bila kuambiwa kuna jambo gani.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi