Kitaifa

Samia afagilia kombati za madini

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amefurahia ubunifu wa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wa kuanzisha sare ya makombati kwa wafanyakazi wa wizara hiyo kuwa utasaidia katika kuongeza molari kwa wafanyakazi.

 Rais Samia ayasema hayo leo Oktoba 21 mwaka 2023 alipokuwa akizindua mitambo ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo na mitambo ya Shirika la Madini Taifa (STAMICO).

Katika hafla hiyo pia Stamico walisaini mkataba wa kufanya utafiti wa madini na utengenezaji wa mkaa mbadala.

Akizungumza Rais Samia amesema Mavunde ameingia kwenye wizara hiyo na fikra alizotoka nazo Wizara ya Kilimo ambazo zilikuwa ni mwelekeo (vision) hadi mwaka 2030, sekta ya kilimo iwe imechangia katika pato la Taifa kwa asilimia 10.

Amesema kuwa katika Wizara ya Madini, Mavunde amekuja na mpango wa hadi kufikia mwaka 2030 Tanzania iwe na kanzidata ya madini, jambo ambalo anampa baraka zake zote kuendelea nalo.

Pia Mavunde ameenda katika wizara hiyo na kauli mbiu kuwa madini ni maisha na utajiri jambo ambalo ni kweli.

“Lakini jingine ni uniform (sare). Niliwakuta kilimo (Wizara ya Kilimo) wame-design (wamebuni) kombati za kilimo sasa amekuja huku akasema ili kuwapa molari wafanyakazi lazima tuje na kombati ya aina yake, wakitokea hivi unajua hawa ni staff (wafanyakazi) wa Stamico, hongera sana,” amesema.

Katika Wizara ya Kilimo, magwanda yaliyobuniwa ni ya rangi ya kaki huku kwa upande wa Wizara ya Madini ni ya rangi ya bluu (dark bluu)

Aidha, amesema siku akimuapisha Dk Doto Biteko kuwa Waziri wa Madini alimwambia kuwa walimpatia dhima ya kuhakikisha kuwa sekta hiyo ikifika mwaka 2025 ichangie kwenye pato la Taifa asilimia 10, jambo ambalo alilifikia mwishoni mwa mwaka jana.

“Kwa hiyo ametumia muda mfupi kuliko tulivyomkadiria. Sasa nikaona mbinu ile ile aliyoitumia kule nimpandishe awe Naibu Waziri Mkuu aje atusaidie huku. Lakini nimkabidhi na Nishati pia aende atusaidie huku. Kwa hiyo Dokta hongera na pole,”amesema.

Naye Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko amesema wadau wa sekta ya madini wamezoea kumsikia kwa miaka mingi na kwamba Rais Samia amewapelekea waziri si tu mchapakazi bali mbunifu.

“Mimi mheshimiwa Rais sikuwahi hata kubuni wapendeze namna gani, nilivyoingia humu nikashangaa kweli ubunifu huu wa mheshimiwa waziri (Mavunde) niwakupigiwa mfano nakupongeza sana waziri,”amesema.

Dk Biteko amemweleza Mavunde kuwa salama yake na kazi yake ni kumsikiliza Rais Samia anavyomwelekeza na kuwasaidia wachimbaji wake kama anavyofanya.

Amemuhakikishia kuwa kila ubunifu atakaokuwa nao, Rais Samia atampatia ushirikiano wa kufanya kazi yake kama ilivyokuwa kwake wakati akiwa Waziri wa Madini.

Naye Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema eneo lililofanyiwa utafiti ni asilimia 16 ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ilichangia upatikanaji wa fedha za kigeni kwa zaidi ya asilimia 56.

“Mauzo ya nje kwa sekta ya madini ni Dola za Marekani Bilioni 3.3 sawa na aslimia 56 ya mauzo ya bidhaa nje ya nje…Katika mwaka uliopita kwenye hilo eneo la asilimia 16 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya mapato ya ndani Sh 2 trilioni sawa na asilimia 15 imetoka kwenye sekta ya madini,” amesema.

Amesema kwa kufanya utafiti kutasaidia katika kuongeza pato linalotokana na sekta hiyo nchini.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dk Venance Mwasse aamesema ili kupata taarifa sahihi za kijiolojia na ziwe na maana ni lazima uchoronge kuchukua sampo na kuzipeleka maabaara na kupata majibu.

“Tukaamua kununua mashine 15 kwa ajili ya wachimbaji wadogo tu na hii ni rafiki kwa ajili ya wachimbaji wadogo, zinabebeka kwa urahisi kuitoa sehemu moja kwenda nyingine kwa gharama ndogo, matumizi yake ya mafuta ni rafiki kiasi ambacho kinampunguzia mchimbaji mdogo gharama ambazo sio za lazima,” amesema.

Naye Rais wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina amesema ufanyaji wa tafiti ambao utawezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za madini utakwenda kuondoa migogoro kati wachimbaji wakubwa wa madini na wadogo.

Pia aliomba kuteuliwa kwa mbunge anayewakilisha kundi la wachimbaji wa madini bungeni, ombi ambalo Rais Samia alijibu kuwa analichukua.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi