Kitaifa
Ripoti: Moto Kariakoo ni hujuma, siyo ajali
Dar es Salaam. Siku chache baada ya tukio la moto lililotokea Kariakoo na kuteketeza baadhi ya maduka na vibanda vya wafanyabiashara, kamati iliyoundwa na Ofisi Mkuu wa Mkoa imebaini chanzo cha moto huo ni hujuma baina ya wafanyabiashara na sio ajali.
Oktoba Mosi, moto mkubwa uliteketeza maduka na vibanda kadhaa vya wafanyabiashara Kariakoo na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi, huku chanzo cha moto huo kikiwa bado hakijafahamika.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, aliunda kamati ya uchunguzi ikihusisha vyombo vya ulinzi na usalama ambayo ilitwkiwa kufanya uchunguzi wa tukio hilo ndani ya siku Saba.
Akizungumza na wanahabari leo Ijumaa Oktoba 20, 2023 Mkuu wa Mkoa huo amesema kamati hiyo imebaini chanzo cha moto ni hujuma ndani ya wafanyabiashara wa mnadani Kariakoo zilizosabishwa na mgogoro uliopo baina ya wafanyabiashara na uongozi uliopo.
“Maelezo ya waliohojiwa wafanyabiashara na walinzi wa mnadani yalionekana kuwa yamepangwa na hayaakisi uhalisia wa tukio husika pia namna moto ulivyoanza na kukua kwa kasi kwa kuangalia kupitia kamera za CCTV,” amesema Chalamila.
Aidha uchunguzi wa kamati hiyo pia umebaini changamoto zilizojitokeza wakati wa kupambana na moto ikiwemo ukosefu wa msukumo wa maji ya kuzima moto eneo la Kariakoo siku ya tukio.
Amesema kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji, pamoja na uhaba wa maji katika visima vya maji ya kuzima moto na kubaini kuwa visima hivyo ni vichache kwa mkoa kwani havitoshelezi kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Kumekuwepo na ujenzi holela eneo la Kariakoo Mnadani ambao haujahusisha uwekaji wa miundombinu wa njia za dharura pamoja na kuwepo kwa ujenzi uliyotumia mbao ambao imechangia Kwa kiasi kikubwa ukuaji wa moto kwa kasi,” amesema.
“Eneo hilo pia lilihusisha uuzaji wa vifaa asilia ya vimiminika vinavyowaka na kulipuka ambavyo vinamgandamizo wa gesi pamoja na ucheleweshaji wa kutoa taarifa ya wito wa tukio la moto kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,” amesema.
Akizungumzia mapendekezo ya kamati hiyo, Chalamila alisema wafanyabiashara hao wanapaswa kutafutiwa eneo jingine kwa ajili ya kufanyia biashara hiyo kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu.
Pia, Halmashauri inapaswa kuzingatia sharia zinazoelekeza upangaji wa mji na majengo kwa kuacha njia za dharura wazi baina ya jengo na jengo wakati waliokiuka na kuziba njia kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema.
Aidha kamati imependekeza kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kufanya mapitio ya Kampuni ya Kariakoo Auction Mart ili kupata uhalali wa umiliki na namna ya uendeshaji wa kampuni hiyo.
“Inapaswa kuwekwa mipango madhubuti ya uendelezaji wa eneo hilo ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa eneo hilo kwa kuweka miundombinu ya kisasa inayofanana na mazingira ya kibiashara katika mji ili Serikali ipate mapato na kutoa elimu kwa wamiliki wa majengo na wafanyabiashara kukata bima,” amesema.
Aliongeza kuwa uchunguzi huo umehusisha eneo la tukio na kufanya mahojiano ya kina na mashuhuda, wamiliki wa majengo yanayozunguka eneo hilo, wafanyabiashara, walinzi wa zamu pamoja na kupitia picha za kamera zilizorekodiwa kabla na baada ya tukio.