Connect with us

Kitaifa

Serikali yakiri kumlipa mwekezaji Sh75 bilioni

Dar es Salaam. Serikali imethibitisha kuilipa kampuni ya Winshear Gold Sh75 bilioni, ikiwa ni stahiki yake baada ya kukamilika kwa mazungumzo nje ya mahakama.

Taarifa za malipo hayo yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania kwa Winshear zilitolewa juzi na kampuni hiyo, ikifafanua ni sehemu ya fidia baada ya kumaliza migogoro kati yao na Serikali.

Mzizi wa mgogoro huo ni Serikali kuifutia kampuni hiyo leseni ya uendeshaji wa mradi wa dhahabu wa SMP ambapo kampuni hiyo haikukubaliana na uamuzi huo na mwaka 2020 ilifungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) nchini Uingereza ikiwakilishwa na kampuni ya uwakili ya Lalive.

Kufutwa kwa leseni ya kampuni hiyo kulitokana na mabadiliko ya sheria ya madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2017 pamoja na kanuni zake zilizofuta leseni hizo.

Katika taarifa yake kwa umma juzi, Winshear iliweka wazi kuwa mgogoro huo umemalizika baada ya Serikali kuilipa kiasi hicho cha fedha walichokubaliana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Winshear, Richard Williams alisema hatua hiyo ni nzuri kwa pande zote.

“Ni wakati mzuri wa pande zote kuendelea na mambo yake na tunaitakia Tanzania mafanikio katika kuvutia uwekezaji mpya,” alisema.

Katika taarifa hiyo, Williams alipongeza mawakili waliosimamia kesi hiyo.

Alipotafutwa juzi kuzungumzia hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi alikiri malipo hayo kufanyika, ingawa hakufafanua kwa kina majadiliano yalivyokuwa mpaka wakakubaliana jambo hilo.

Majibu ya Dk Felesh yalitokana na kuulizwa kuhusu taarifa ya Winshear kupokea malipo kutoka Serikali ya Tanzania iliyokuwa ikisambaa mtandaoni ambapo alijibu kwa ufupi “ndiyo ni kweli.”

Hata hivyo, gazeti hili lilizungumza na Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniface Luhende kutaka kujua undani wa kesi hiyo ambaye hakuwa tayari kuizungumzia kwa madai kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiye mtu sahihi.

Alipotafutwa tena kufafanua hilo, Dk Feleshi simu yake iliita bila majibu.

Hii si kesi ya kwanza kwa Tanzania kushindwa na kujikuta ikitakiwa kulipa mabilioni ya fidia.

Julai mwaka huu, Serikali ilitakiwa kulipa fidia ya Sh260 bilioni kwa kampuni ya Indiana Resources, iliyoshinda kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID), baada ya kujiridhisha ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika mradi wa Nikel wa Ntaka Hill mwaka 2018.

Uamuzi kama huo pia ulitolewa na ICSID mwaka 2019 ukiiamuru Serikali kuilipa kampuni ya IPTL fidia ya Sh426 bilioni kwa ukiukwaji wa masharti ya mkataba.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi