Connect with us

Kitaifa

Tiba ya Methadone inavyogharimu Serikali mabilioni

Tanga. Kuna simulizi nyingi kwenye baadhi ya familia kutokana na vijana wao kujikuta wametumbukia katika wimbo la matumizi ya dawa za kulevya.

Licha ya jambo hilo kugharimu uchumi wa familia, pia Serikali nayo haipo kando kutokana na kugharamia matibabu ya watu hao kila siku kupitia matumizi ya dawa za methadone.

Vijana wengi wameathirika kiafya kwa kupata maambukizi ya magonjwa sugu yakiwamo ya virusi vya Ukimwi, kifua kikuu na homa ya ini huku wengine wakijikuta wakijiingiza katika uhalifu wa uporaji na utapeli.

Serikali kupitia mpango wake wa utoaji huduma ya dawa ya methadone ya kuwatibu waraibu wa dawa za kulevya aina ya heroine ujulikanao MAT imejenga vituo katika baadhi ya mikoa.

Mbali ya Jiji la Dar es salaam, Serikali imejenga jengo la kituo methadone katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tanga ya Bombo kilichoanza kutoa huduma Juni, 2020 na mpaka Septemba mwaka huu imeshahuduma waraibu 951.

Kwa mujibu wa takwimu za Mkoa wa Tanga kwa kipindi cha miaka mitatu hadi Desemba mwaka jana, Serikali imetumia wastani wa zaidi ya Sh 2.5 bilioni kuwatibu waathirika 951 wa kituo cha Bombo pekee kwa kuwapa dawa za methadone ili kuwaokoa wasiingie kwenye majanga mengine ikiwamo kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kifua kikuu, homa ya ini na wengine kufungwa au kufa.

Akizungumza na Mwananchi, mkuu wa kituo hicho, Dk Wales Karata anasema mtu akianza kutumia dawa za kulevya humuingia haraka kwenye ubongo na kuelegeza mwili na ili ajisikia vizuri humlazimu kupata angalu kete 10 za heroine kila siku.

Anasema heroine hutumika kwa kuvuta puani, kujidunga kwa sindano kupitia mishipa ya mikononi, miguuni, shingoni na wengine ambao ni wabobezi hujidunga kwa kupitishia sindano kwenye mishipa ya sehemu zao za siri kwa upand wa wanaume.

Dk Karata anasema matumizi ya dawa za kulevya yanaathiri uchumi kwa ngazi ya familia kwa sababu ili mtumiaji ajisikie vizuri lazima atumie kete 10 za heroine ambayo kila moja huuzwa Sh3,000 na wengi wao kwa sababu hawawezi tena kufanya kazi za uzalishaji mali, hulazimika ama kuiba chochote nyumbani au mtaani, kupora au kufanya utapeli ili atibu arosto unapofikia muda wa kumsumbua.

“Matokeo yake, mraibu wa dawa za kulevya hujikuta akijitenga baada ya kubaini hatakiwi na familia yake na jamii kwa ujumla hivyo anakimbilia kwenye magenge yasiyo mazuri na huko mambo yanayoendelea ni ya kubakana, kulawitiana na wengine kujeruhiana. Inapofikia hatua hiyo mraibu anapoteza matumaini ya maisha,” anasema Dk Karata.

Mtaalamu huyo anasema mbali ya kuwapa dawa waraibu hao, kituo hicho hutoa huduma ya kuwajenga kimaadili na kiakili ili warejee katika hali ya kawaida na wasirejee kwenye matumizi ya dawa hizo za kulevya.

Anasema kituo hicho kimekuwa kikishirikiana na asasi za kiraia zilizopo jijini Tanga za Gift Of Hope Foundation, Tanga Drug Free na Oyabi ambazo ndizo huwafuata waathirika wa dawa za kulevya vijiweni na kuwapeleka kupata ya dawa za methadone.

“Asasi hizo zina wataalamu wanaojua namna ya kujichanganya na waathirika wa dawa za kulevya na wanaweza kuzungumza lugha inayowafanya kukubalika na wasionekane kama ni maadui zao ambao wanataka kuwakamata…baadaye huwashawishi na kuwaleta hapa kituoni na hapa tunawaandaa kwa wiki mbili kabla ya kuanza kuwapa methadone,” anasema Dk Karata.

Mtaalamu huyo ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya na Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na dawa za kulevya (DCEA) chini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu ambayo imefanikisha huduma ya methadone inayowasaidia vijana wengi.

Anasema hadi sasa vijana 20 waliokuwa wameathirika na heroine wameshapona na wamerejea katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa.

Waraibu wanasemaje?

Charles Michael, mkazi wa Ngamiani Jijini Tanga anaiomba jamii kushirikiana na vyombo vya dola kuwafichua wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa sababu wananufaika na kujitajirisha huku wakiwatesa vijana na kuwapotezea ndoto zao za maisha.

Selemani Haji, mkazi wa Wilaya ya Pangani anasema madhara ya matumizi ya dawa za kulevya ni makubwa kuliko inayodhaniwa kwa sababu imefikia hatua ya watu wa makundi na kada tofauti wamejiingiza.

Ali Musa ambaye kwa sasa amekuwa akizunguka kwenye maskani za wanaotumia dawa za kulevya kwa ajili ya kuwapa nasaha na kuwashawishi kwenda kupata methadone anasema mbali ya mraibu kutengwa na familia pamoja na jamii na kuona kilimbilio ni kwenye mageto ya kutumia dawa hizo, anapokuwa ameathirika kwa kiasi kikubwa hata wenzake getoni humtenga na kumnyanyapaa anapoanza kukohoa kwa hofu ya kuambukizwa kifua kikuu au maambukizi mengine.

Huduma yaonyesha mafankio

Katibu Mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali Gift of Hope Foundation lenye makao yake Jijini Tanga, Said Bandawe anasema limekuwa na jukumu la kuibua waraibu, kuwaelimisha na kufuatilia watumiaji wa methadone.

“Naipongeza Serikali kwa kuamua kugharamia kuwatibu waraibu wa dawa za kulevya kama isingeratibu na kugharamia tiba hii hali ingekuwa mbaya, vijana wengi wangekufa kutokana na vifo vitokanavyo na matumizi ya dawa za kulevya,” anasema Bandawe.

“Tumefanya tathimini na kubaini ukweli kuwa huduma ya methadone imeanza kuleta mabadiliko kwa waathirika kwa zaidi ya asilimia 65 kwa sababu wengi wamerejea na kuonekana kama binadamu wengine, wamerejea kwenye familia zao na kutekeleza majukumu yao baada ya kupona,” anasema Bandawe.

Waomba tiba kwa njia ya kazi

Baada ya kufanikisha kuratibu matibabu ya dawa za methadone,wengi wa waraibu wamepona na kuwa na ari ya kufanya kazi lakini wanakabiliwa na changamoto za kukosa nini cha kufanya ili waendeleze maisha yao.

“Ili kuwarejesha katika hali ya uzalishaji mali,tungetamani uratibu ufanyike kwa waraibu waliopona kufunguliwa fursa za kuwaendeleza kulingana na ujuzi wao.

“Waraibu waliopona wapo wenye fani, ujuzi na uhodari na wengine ni wasomi walio na shahada ya pili (masters) lakini bado jamii inawatenga kwa sababu ya kutowaamini tena…kama ilivyowawezesha kuwatibu na kuwaponya kwa kutumia methadone, tungetamani ufanyike uratibu wa kubaini ujuzi wa kila mmoja na wafanyiwe tiba kwa njia ya kazi,”anasema Bandawe.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi