Kitaifa
Ndani ya Boksi: Kilele cha ‘Jiniasi’ Nyerere Julius
Akili kubwa imelala kijijini Butiama pale. Ni Baba wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mwaka wa 24 huu ‘kiranja’ wetu huyu hatupo naye. Wacha tule ‘wikiendi’ tukifurahia maisha yake.
Alituachia kila kitu. Muungano, amani, mshikamano, upendo, ujamaa, viongozi, michezo, viwanda, ndege, mashirika, taasisi. Na heshima kubwa kwa mataifa yote duniani. Wacha tufurahie maisha yake
MICHEZO
Mwalimu alikuwa siyo mpenzi wala shabiki sana wa soka. Ingawa alikuwa na urafiki wa karibu sana na viongozi wa Yanga. Enzi hizo wakati wa uongozi wa Mzee Tabu Mangala.
Mara chache alikubali kuwa mgeni rasmi wa mchezo wa soka. Lakini alikerwa na kuacha kabisa kuhudhuria uwanjani baada ya kukasirishwa na timu ya Bongo iliyocheza na timu ya Sudan.
Kilichomkera ni wachezaji wa Bongo kuingia uwanjani wakiwa matumbo wazi. Kwa madai kwamba hawana jezi za kuvaa. Hiki kitu kilimfedhehesha na kususa kabisa kwenda uwanjani.
NI MWANANCHI
Kwa mujibu wa kada maarufu na mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mzee Steven Wassira, ni kwamba Mwalimu alikuwa mwananchi, yaani mnazi na shabiki wa Yanga.
Mzee Wassira alinukuliwa akidai kuwa, hata habari za soka Nyerere alienda kupata kwa rafiki yake kipenzi Mzee Tabu Mangara, aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga kwa wakati ule.
KIPIGO CHA KIHISTORIA
Ni awamu ya tano ya Magufuli ambayo hatukushuhudia kipigo kikali kutoka kwa Mnyama kwenda kwa Wananchi. Wakati wa Jakaya, Wananchi walilambwa goli tano na Mnyama 2012.
Wakati huo Mnyama wa moto na kina Okwi, Mafisango na Kaseja. Wakati wa Ben Mkapa, pia Mnyama aliwafurusha Wananchi kwa goli 4 katika uwanja wa Uhuru, ilikuwa mwaka 2001.
1994 wakati huo Ikulu ya Mgogoni ikiwa chini ya Mzee Ruksa Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Mnyama aliipelekea moto Yanga na kuifumua goli 4. Goli la Constantine Kimanda, likafuta chozo la Wananchi.
Funga kazi ni wakati wa Mwalimu Nyerere. Baada ya Simba kutandikwa goli 5. Wakaja kulipa kisasi nao, kwa kuwazibua Wananchi goli 6. Goli hizi zote hazijawahi kulipwa.
TIMU ZA MASHIRIKA YA UMMA
Wakati wa Mwalimu, timu za masharika ya umma zilikuwa na nguvu sana kuliko za wananchi wa kawaida. Ni Simba na Yanga tu zilizotamba kwa wingi wa wafuasi.
Ni kwa sababu mchezaji alikuwa ni mwajiriwa wa shirika husika. Hawakuwa na njaa njaa. Soka ilikuwa ni ridhaa na starehe. Lakini ajira ikawa kipaumbele cha kwanza, na wachezaji hawakuwa na njaa.
Mashirika yaliyotamba na timu kali ni pamoja na Pamba ya Mwanza. RTC Kagera, RTC Kigoma, Reli ya Morogoro, Ushirika Moshi, Sigara ya Dar es Salaam, CDA Dodoma, Ndovu Arusha, Mecco Mbeya nk.
NYERERE NA BOB MARLEY
Mwaka 1980 wakati Zimbabwe ikipata uhuru wake kutoka kwa Mwingereza, kwenye sherehe za Uhuru walialikwa viongozi wengi, akiwemo Baba wa Taifa, Julius Nyerere.
Kwenye sherehe hiyo, Nyerere alikuwa kama taa ya viongozi wote. Kwa sababu jasho, mali na muda mwingi aliutumia katika ukombozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika, likiwemo taifa la Zimbabwe.
Katika sherehe hizo alialikwa nyota wa muziki kutoka Jamaica, hayati Robert Nesta Marley (Bob Marley), akiwa wa moto sana na dunia nzima ikiimba ngoma zake.
Nyerere hakumjua vyema Bob Marley. Mwamba kutoka Kingstone alishika maiki, gitaa na kusimama jukwaani rasta zake zikitawanyika kama ndege walifurushwa kwenye shamba la mpunga.
Akapiga pini nyingi ikiwemo Zimbabwe, iliyopagawisha watu. Lakini hakuweza kuteka hisia za Julius. Baada ya drums kuashiria ujio wa ngoma ya Africa Unite. Kila kitu kilibadilika.
Mistari michache ya mwanzo iliuvuruga ubongo wa Mwalimu. Akashuka kwenye viti vya waheshimiwa jukwaa kuu, kisha akaelekea lilipo jukwaa la ‘muhuni’ wa Kijamaica na kumpa mkono. Saluti!
Julius Kambarage Nyerere kasimama, nani wa kuendelea kukaa kwenye vitu? Big Man akiyanyuka wote nyanyuka.
Ndo kilichotokea, wote wakaunga tela la kumpongeza Robert Nesta Marley.
Mwalimu alipata kunong’onezana na Bob. Za ndani ni kwamba alimtaka atie timu kwenye ardhi yake hapa Bongo.
Lakini mwaka uliofuata mwamba aliaga dunia kwa kansa.
Africa Unite ni wimbo ambao maudhui yake, ndiyo lilikuwa tamanio kubwa la Julius. Alitaka Waafrika tuungane tuwe kitu kimoja. Nyerere amekufa na ndoto ya kuiunganisha Afrika iwe moja.
NYERERE NA MUZIKI
Enzi za Mwinyi vikundi vingi vya muziki wa kizazi kipya viliibuka kwa wingi. Lakini wakati wa Mkapa ndipo milango ya Bongo Fleva ilipofunguka rasmi. Wakaibuka kina Sugu, Prof. Jay na wengineo.
Hata Nyerere, vijana wa wakati ule ni wanamuziki wa dansi. Kama ambavyo Bongo Fleva ilichipukia kwa kasi wakati wa Mkapa, pia dansi ilikamata wakati wa Nyerere.
Mzee Zahir Zorro, wakati wa Nyerere alikuwa mdogo kuliko Mbosso. Bichuka, Hamza Kalala, Nguza Vicking, King Kiki, Chidumule, Dk Remmy, Marijani Rajabu nao walikuwa wadogo sana.
Kama Marijani alifariki 1994 akiwa na miaka 44, piga hesabu enzi za Nyerere miaka ya 70 alikuwa na umri gani? Kama Mbaraka Mwishehe alikufa akiwa na miaka 35 mwaka 1979.
Walikuwa vijana wenye mafanikio. Miaka ya 70 tayari Dr Remmy alirekodia muziki Uingereza. Ndio maana hata sasa ngoma zake ukisikiliza zina utofauti mkubwa na wenzake kwa sababu ya sound tamu.
Manaake nini? Nyerere pia aliwafungulia njia vijana wa wakati ule pengine zaidi ya waliomfuatia. Wafanyakazi wa umma waliburudishwa na muziki wa bendi zilizomilkiwa na taasisi zao.
Ilikuwa ni lazima kila shirika la umma kumiliki bendi. Uhamiaji Band, Polisi Jazz, JKT Jazz, Vijana Jazz, OTTU Jazz, DDC Mlimani Park, Tancat Almas Iringa na nyingine kibao.
Kama vile timu za soka za mashirika, kote walijaa vijana tupu. Kifupi Mwalimu alikuwa ni mchanganyiko wa kila kitu. Hakuna aliloacha lijiendee kibwegebwege tu.
Lala Mwalimu…
Imeandikwa na By Dk Levy