Kitaifa
Hatua kwa hatua upasuaji kuongeza matiti, makalio
Dar es Salaam. Siku chache baada ya kutangazwa upasuaji wa kurekebisha maumbile utakaofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, madaktari wameeleza hatua za kufuatwa kabla ya huduma kutolewa.
Oktoba 10, mwaka huu katika mkutano na waandishi wa habari hospitali hiyo ilitangaza kuhusu huduma hiyo itakayotolewa na wataalamu wa Mloganzila kwa kushirikiana na daktari bingwa wa upasuaji wa kupunguza uzito na upasuaji rekebishi kutoka India, Dk Mohit Bhandari na taasisi ya afya ya MedINCREDI ya Tanzania.
Upasuaji huo utakaohusisha kupunguza mafuta mwilini na kurekebisha maungo, ikiwamo kupunguza au kuongeza ukubwa wa matiti na makalio, kupunguza tumbo au nyama kwenye mikono na sehemu nyingine za mwili, unatarajiwa kufanyika Oktoba 27, mwaka huu.
Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa hospitali hiyo, Dk Eric Muhumba katika mahojiano jana kupitia kipindi cha Power Breakfast kinachoendeshwa na Clouds FM, alisema upasuaji huo rekebishi unawahusu waliochora tattoo, waliopata ajali ya kuumia hivyo kuwa na kidonda kikubwa kinacholazimu kuchukua nyama au ngozi sehemu nyingine ya mwili na kuungua moto.
“Mwingine hana kovu, hana tatizo lolote lakini anataka kurekebisha maumbile iwe matiti, hipsi kuongeza au kupunguza nyama za tumbo, hawa lazima tuwashirikishe wataalamu wa saikolojia kabla ya kumfanyia upasuaji,” alisema.
Alisema huduma hiyo inatolewa baada ya ile ya awali ya watu kuwekewa puto ili kupunguza uzito. “Hawa wameshapungua na wengine nyama zimetepeta, wanahitaji marekebisho. Pia tulipokea maombi kutoka kwa Watanzania wanataka huduma za aina hii,” alisema.
Daktari bingwa wa upasuaji Mloganzila, Edwin Muhondezi alisema baada ya kukutana na mtaalamu wa saikolojia, anayehitaji atafanyiwa vipimo na kupewa mwongozo kulingana na mahitaji ya huduma anayotaka.
Alisema ili kuongeza makalio, huchukua mafuta kutoka tumboni na kuyahamishia kwenye makalio.
“Hii ni aina mojawapo ya kuweza kuongeza makalio, mafuta lazima yawe yako. Yalikotolewa hayataweza kurudi tena na kama yalipelekwa makalioni ukila ukaanza kunenepa, unanenepa makalio sababu zile chembechembe zinaongeza mafuta ndani ya seli,” alisema Dk Muhondezi.
Kuhusu matiti, alisema hutumia tishu ambazo hazihusiani na uzalishaji wa maziwa.
Hata hivyo, alisema kwa wanaoongeza ukubwa wa matiti, iwapo watazaa watalazimika kufanya upasuaji mwingine, kwa kuwa husinyaa baada ya kumaliza kunyonyesha.
Mpaka juzi, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi alisema watu watano wamejitokeza kujisajili kupata huduma ya kurekebisha maumbile, akisisitiza kinachofanyika kinalenga matibabu.
Alisema hadi sasa ni mgonjwa mmoja pekee aliyeomba kupatiwa huduma hiyo kwa ajili ya urembo. Kwa awamu hii alisema watatoa huduma kwa watu kati ya sita hadi 10.
“Tunategemea wahitaji zaidi. Kwa mara ya kwanza hatuwezi kufanya wengi, muda ni mdogo, tutaona kwa sababu tutafanya nyingine na wenzetu wa Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka,” alisema Profesa Janabi alipozungumza na waandishi wa habari.
Mtaalamu wa saikolojia na mkurugenzi wa taasisi ya The Better You, Jiwa Hassan alisema wanaohitaji huduma ya kurekebisha maumbile wapo wanaokwenda kwa ajili ya tiba na wengine ili aonekane wa thamani kama mtu fulani. “Huyu hajajikubali, anajikosoa, hajiamini, anaweza kujikuta kila siku thamani yake ni ndogo. Watu wa aina hii kuna haja ya semina ya afya ya akili.
Kuna namna ukimwangalia mtu unabaini ana changamoto ya afya ya akili, lakini pia wanaume ni sababu kwa kuwa wao wanatamani kwanza ndipo wanapenda,” alisema Jiwa.