Kitaifa
Nitaifumua Wizara ya Mambo ya Nje – Samia
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameweka wazi kuwa ataifumua na kuisuka upya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ili kuirudishia hadhi baada ya kuwa na utendaji usioridhisha kwa muda mrefu.
Hatua hiyo imekuja kutokana na wizara hiyo kupoteza ushawishi kwenye medani za kidemokrasia, huku mashirika ya kimataifa yakilalamika kutoridhishwa na utendaji wa wizara hiyo nyeti.
Rais Samia amesema hayo jana, wakati akipokea ripoti ya kamati ya kutathmini ufanisi na utendaji wa wizara hiyo, kazi iliyofanyika kwa miezi sita chini ya uenyekiti wa Balozi Hassan Simba Yahaya.
Amesema muundo wa wizara hiyo unaenda kuangaliwa upya, ikiwemo namna ya kuwapata watumishi wenye sifa stahiki, kwa kuwa wengi waliopo hawana uwezo.
Amesema kwa muda mrefu wizara imekuwa ikitawaliwa na urasimu katika kuajiri, hali iliyosababisha watu wasio na sifa kuajiriwa kwa maelekezo ya vigogo ndani ya wizara.
“Ripoti imeeleza hapo katikati ajira hazikuwa katika mpangilio mzuri, zilikuwa chache na zilitolewa kwa kujuana. Sasa mengine nayafahamu mie hata kwenye ripoti hayajawekwa, pia kuna makundi, hamisha hamisha na panga pangua ya maofisa waandamizi haya yote yalichangia utendaji wa wizara kupwaya.
“Hili ni moja ya masuala yanayonisukuma kutaka kamati hii uindwe na kuifanyia tathmini wizara, ubobezi ule wa miaka ya 90 na 2000 sasa wizarani hakuna, unguli, umahiri na ushawishi wetu kwenye medani za kidemokrasia umekuwa wa kujikongoja.
Kumekuwa na malalamiko kutoka taasisi za kimataifa zilizopo nchini kuhusu utendaji usioridhisha wa wizara hii,” amesema Rais Samia.
Pia aligusia uwakilishi wa nchi kupitia balozi zake katika mataifa mbalimbali akitaka mpangilio huo kuangaliwa upya kulingana na hali ya sasa.
“Tunapaswa kuangalia upya suala la uwakilishi wetu kupitia balozi tulizonazo nje ya nchi na hadhi zake kutokana na mabadiliko yaliyopo duniani. Wakati ule tulikuwa tunaanzisha balozi kwa kuangalia wanaotusaidia pesa nyingi, lakini mambo yamebadilika, lazima tuangalie wapi tuwe na balozi za kupewa nguvu,” amesema.
Sambamba na uwakilishi wa nchi, alizungumzia pia namna teuzi za mabalozi zinavyofanyika, huku akitaka jukumu hilo sasa wapewe watu wanaostahili na sio kwa kuoneana haya.
“Tunavyofanya sasa wizara inaleta mapendekezo, yanavyoletwa na mie nina yangu mkononi naletewa nani kaharibu wapi anaweza kupelekwa. Sasa hujui mapendekezo yapi ya kisiasa, yapi ya kitaaluma.
“Sasa hivi tufumbe macho anayevurunda kazini akae pembeni, hakuna haja ya kumpoza kumpeleka kwenye ubalozi, lakini pia nafasi za kisiasa hatusemi zisiwepo, lakini tuangalie kwa asilimia gani. Ila changamoto wakati mwingine hao wenye taaluma hawapo pale wizarani kwa sababu ya undugu uliojaa,” amesema.
Kufuatia hilo, kiongozi huyo mkuu wa nchi alielekeza kuwepo vigezo vya kuajiri watumishi katika wizara hiyo na kuondokana na mfumo uliopo sasa ambao unaruhusu watu wasio na sifa kubebwa.
“Hapa mkono wa Rais unakwenda kuingia kwenye hii wizara, tutaanzisha mfumo maalumu wa ufadhili wa kutengeneza vijana ambao watakwenda kufanya kazi pale.
“Haitakuwa rahisi, ni lazima wawe vijana wenye sifa, watafanya mitihani, wakifaulu ndiyo watawekwa kwenye fellowship hii kwa miaka miwili wakipikwa kisha tuwapeleke wakafanye kazi,” amesema Rais Samia.
Awali, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Balozi Yahaya alipendekeza kubadilishwa kwa jina la wizara, akieleza jina la mambo ya nje haliakisi vizuri majukumu ya wizara husika.
“Pia tunashauri kuwa na umadhubuti wa uongozi wa mambo ya nje ili viongozi waweze kutumikia kwa muda wa kutosha kwa lengo la kutunza kumbukumbu na misimamo ya nchi na kushughulikia masuala ya kimataifa yanayohitaji ufuatiliaji,” amesema balozi Yahaya.
Pia, kamati ilipendekeza kuundwa kwa idara ya uchambuzi wa kimataifa na kupendekeza jukumu la uchambuzi wa taarifa hizo, habari na matukio mbalimbali liondolewe kutoka idara ya Sera na mipango na iundwe idara mpya.