Makala
Sababu wanawake kuongeza matiti, makalio Alhamisi, Oktoba 12, 2023
Dar es Salaam. Kutangazwa kwa huduma mpya ya upasuaji wa kuongeza makalio na matiti ambayo inaanza kutolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kumezidi kuibua kilicho nyuma ya pazia kuhusu wanawake wanaosaka huduma hiyo.
Mahitaji na kiwango cha gharama vinathibitisha kuwa huduma hiyo inawavutia wanawake wengi, huku wataalamu wakionya kuwa inatokana na kutojikubali, kutojiamini na wakati mwingine ikichangiwa na wanaume.
Hali hiyo pia imetajwa kuchangia baadhi ya wahitaji wasio na kiwango cha fedha kinachotakiwa kujikuta wakivaa mavazi ya kuongeza maumbile yao maarufu vigodoro au sidiria zilizoongezwa sponji ili tu waonekane wana makalio na matiti makubwa.
Ushuhuda huo umetolewa kipindi ambacho wanafunzi wawili pacha wamefariki dunia mkoani Simiyu, ikidaiwa ni baada ya kupakwa dawa na mganga wa jadi kwa lengo la kuongeza ukubwa wa matiti.
Ushuhuda wa wahusika
Miongoni mwa wahusika hao ni pamoja na wale waliozungumza na gazeti la The Citizen hivi karibuni kuhusu sababu za kuhitaji huduma hiyo, mawakala na madaktari wanaofanya upasuaji huo, ambao wanafafanua kitaalamu na kueleza athari zilizopo.
Irene John (38), mkazi wa Mwanza anasema alifanyiwa upasuaji wa kunyanyua na kukuza matiti yake mwaka mmoja uliopita akiamini yatakuwa makubwa.
Alisema matiti yake yalikuwa madogo sana ukilinganisha umri wake sambamba na ukubwa wa mwili.
“Nilichokitaka ilikuwa kupata dawa yoyote itakayonipa matokeo ya kuyakuza. Rafiki yangu wa kike alinishauri twende India kwa ajili ya upasuaji. Lakini akanishauri ili niwe na umbo zuri zaidi, nikuze pia na makalio na gharama yake ilikuwa Sh48 milioni,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa anamiliki biashara zake kubwa jijini Mwanza, Mombasa na Nairobi haikuwa shida kupata fedha hizo.
Hivyo alizungumza na mtaalamu akaratibu safari na wakaenda India kwa upasuaji.
Tofauti na Irene, Marry Steven (29), mkazi wa Arusha yeye alisema alifanya upasuaji wa kurekebisha midomo yake na kuongeza matiti kwa msukumo wa mchumba wake.
Alisema miaka sita iliyopita alipata mchumba raia wa Cyprus, aliyefika Arusha kutalii na ambaye walianza uhusiano na wakakubaliana kusafiri pamoja kwenda kwao.
“Siku chache nikiwa huko, akanishawishi kufanya upasuaji wa kurekebisha makalio, matiti na midomo, sikuwa na jinsi zaidi ya kukubali, akanichukua mpaka hospitalini na nikafanyiwa upasuaji,” alisimulia Marry.
Simulizi nyingine ilitolewa pia na mkazi wa Zanzibar, Aisha Salum (34) aliyesema aliamua kuongeza makalio yake kwa sababu tu alikuwa akitamani yawe makubwa tangu alipokuwa na umri wa balehe.
“Nilihitaji kuishi ndoto zangu ndiyo maana nilienda kufanya huu upasuaji,” alisema Aisha.
Mbali na hao, wapo mawakala wa shughuli, akiwemo mkazi wa Dar es Salaam, Samson Peter (38) ambaye husafiri na wateja mbalimbali kwenda Uturuki na India kubadilisha maumbile, anayesema wengi humtafuta wenyewe.
Ni sababu za kisaikolojia
Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, Aidan Njau amesema wengi huamua kurekebisha maungo yao kwa sababu za kisaikolojia.
Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu hali hiyo, alisema kutokana na hali hiyo, wameendelea kupokea wanawake wanaohitaji kuongezwa maumbile kulingana na kiungo anachohitaji.
“Anaona hawezi kuvaa nguo ikamkaa vizuri akapendeza, sababu za kijamii wanamcheka, labda na maisha ya kawaida na wengine maungo yao yanawaletea tatizo kwenye ndoa na mahusiano.”
Akizungumzia ongezeko la wahitaji, Dk Njau anasema tangu mwaka huu uanze, wameshawafanyia upasuaji wa kuongeza au kupunguza matiti, wanawake 10.
“Hii ni tofauti na miaka ya nyuma, tulikuwa tukipokea idadi ndogo, lakini mwaka huu imeongezeka, tulikuwa tukipokea zaidi waliokuwa wanataka kuondoa vitambi na nyama uzembe,” anasema Dk Njau.
Anasema uhitaji unazidi kwa sababu hivi sasa huduma hii inapatikana kirahisi hapa nchini na wengi wanapata elimu. Lakini pia tunahisi wengi sasa hawaendi nje ya nchi kama Uturuki, Afrika Kusini, India na kwingineko,” alisema.
Dk Njau anasema gharama za upasuaji huo nje ya nchi ni kubwa kwa sababu inaingiza pia gharama za nauli ya ndege ambayo inakuwa na ya msindikizaji, malazi, chakula na mizunguko ya hapa na pale.
“Lakini pia baadhi yao wakirejea nchini wanapata athari, wanakuja hapa Aga Khan wana vidonda vilivyoharibika, inabidi turudie upya,” anasema.
Na anasema changamoto nyingine waliyokuwa wanakumbana nayo ni jinsi ya kumpata daktari husika aliyemfanyia upasuaji.
“Wengi wakiwapigia madaktari hao, hawapati mawasiliano na wakati mwingine anamkimbia, kwa hiyo kurudi kule hawezi, anapata wapi tena Sh20 milioni za kurudi.”
Muhimbili yajitosa
Akizungumzia huduma hiyo ambayo sasa inaanza kutolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Mkuu wa Idara hiyo ya Upasuaji, Dk Eric Muhumba alisema tangu wametangaza kuanza kwa huduma hiyo Oktoba 27, wameanza kupokea maombi kutoka kwa wateja mbalimbali.
Anasema wengi wanaamini kwa hapa nchini watafanikiwa kwa sababu wameshashuhudia huduma ya kupunguza unene kwa puto ilivyofanikiwa.
“Na wengi wanaohitaji huduma hii ya kurekebisha maumbo ni wale tuliowawekea puto wakapungua, sasa kuna maeneo kama matiti na makalio na wengine nyama zimetepeta, hivyo wanahitaji mtaalamu awarekebishe maungo yao,” anasema Dk Muhumba.
Dk Muhumba alisema wamesogeza huduma hizo nchini na bei yake sasa itaanzia Sh15 milioni mpaka Sh22.5 milioni.
“Gharama itakuwa rahisi tofauti na mtu akienda nje ya nchi, lakini pia hatujaweka gharama halisi, maana mteja akifika kila mmoja ana namna yake ya kupatiwa huduma, hivyo itategemea huduma gani anapewa, ndiyo maana tukasema itaanzia Dola 6,000 za Marekani mpaka Dola 9,000,” alisema.
Hata hivyo, Daktari bingwa wa kurekebisha maumbile Hospitali ya Muhimbili-Upanga, Dk Lauren Rwanyuma alisema mwitikio si mkubwa sana, huenda kwa sababu ya gharama au kutojitangaza.
Alisema kwa kuwa Mloganzila wanaanza, wataangalia mwitikio wa kule, ndipo watajua wafanye nini ili wapate wahitaji zaidi wa huduma hiyo.
Ni kutojiamini
Mtaalamu wa saikolojia, Saldin Kimangale alisema wanawake wanaofanya upasuaji wa kurekebisha maumbile wanasukumwa na hali ya mtu kutokujiamini na kutojikubali. “Yaani hali ya mtu kujihisi watu wanamuona mbaya au si mrembo kutokana na vigezo vilivyozoeleka kwenye jamii, ikiwemo muonekano wa kimaumbile. Hali hiyo ikichukua muda mrefu husababisha kufanya maamuzi hayo,” alisema.
Kimsingi, alisema mtu mwenye matatizo hayo mara nyingi huwaza tofauti na watu wanavyomtazama na kumchukulia.