Connect with us

Kitaifa

Wastaafu Posta, TTCL wamwangukia Rais Samia

Dar es Salaam. Umoja wa Wastaafu wa Chama cha Ushirika (Saccos) Kutoka Shirika la Posta Tanzania na Kampuni ya Mawasiliano ya Tanzania (TTCL) umemwandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan wakimwomba asaidie kupatikana kwa zaidi ya Sh9.2 bilioni wanazodai kwa muda mrefu bila mafanikio.

 Wastaafu hao zaidi ya 1000 na wengine wanaotajwa kufariki wanadai fedha hizo zikiwa ni akiba (Sh1.2 bilioni), hisa (Sh3 bilioni) na hisa za majengo Sh5 bilioni.

Hata hivyo, Meneja wa Chama cha kuweka na Kukopa, (KK) Essau Mwasilembo aliyezungumza na Mwananchi kwa simu leo, amekiri kuwepo kwa madai hayo akieleza sababu kuwa ushirika huo kuwekeza kwenye miradi inayochukua muda mrefu kuzalisha faida.

“Wamenunua majengo na viwanja na kingine kipo Mabibo chenye thamani Sh2 bilioni bado hatujapata wateja na tukiuza tunataka tuwalipe baadhi ya madai yao,” amesema.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Oktoba 7, 2023 Dar es Salaam, Mwenyekiti wa umoja huo, David Hango amesema tatizo hilo lilianza kusumbua tangu mwaka 2017 japo wapo wanaodai tangu 2005 walipostaafu.

“Kwa utaratibu wetu, mfanyakazi ana hiari ya kuingia na kujitoa kwenye chama na anapojitoa kwenye chama chetu cha kuweka na kukopa anatakiwa kuandika barua kwa meneja na baada ya miezi mitatu hutakiwa kulipwa akiba zake zote na hisa zake zote,” amesema

Amesema tangu walipojitoa kwenye ushirika huo, wamekuwa wakipigwa kalenda kwa muda mrefu sasa na meneja wa ushirika huo kiasi kushindwa kupata stahiki zao hadi leo.

“Rais chama chetu kilikuwa na pesa nyingi na kilikuwa kikipigwa mfano kipindi hicho, hatuelewi pesa zetu zimekwenda wapi kutokana na shida hiyo, tunakuomba Rais uunde tume ya ukaguzi wa mahesabu yote ya fedha zilizoingia na kutoka kwenye chama ikiwezekana tangu mwaka 2004 hadi sasa,” amesema Hango

Amesema ndani ya chama hicho kuna ufisadi wa kutisha mathalani kwenye majengo yao na mradi wa viwanja vya Msata Bagamoyo, fedha zimeliwa na baadhi ya viongozi wa ushirika huo huku wadau hawajapata viwanja vyao hadi sasa.

Naye Katibu wa umoja huo, kutoka TTCL, Abdy Mchonga amesema katika kufuatilia madai yao Juni 30 mwaka 2022 walipeleka barua hadi makao makuu ya Tume ya ya ushirika Tanzania bado haijajibiwa hadi sasa.

“Ushirika umeshindwa kutatua kero zetu na kutuacha wastaafu tunazidi kuteseka kufuatilia bila misaada wowote,Wizara ya kilimo hatujali kabisa,” amesema

Mchonga amedai mwanzo Mrajisi wa vyama vya ushirika Makao makuu Dodoma, alionesha ushirikiano lakini baadaye amekuwa hana msaada wowote.

“Tumeendelea kupoteza wastaafu wenzetu waliotangulia mbele ya haki wamefariki bila kulipwa stahiki zao na familia zao hazina pa kuanzia kudai malipo yao,” amesema

Amesema imefikia hatua ya kushindwa kuaminiana kati ya wanachama wa umoja wa wastaafu hao na viongozi wakidhani wanalegalega katika kufuatilia stahiki zao.

Kwa upande wake Ofisa wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Elia Richard amesema wanafuatilia madai hayo kujua mara ya mwisho yalifikia hatua ipi tangu kuwasilishwa kwenye kitengo kinachoshughulikia malalamiko.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi