Connect with us

Makala

Prime Mambo 10 ya kiafya kwa wanawake wenye miaka 40

Mwanamke mwenye umri wa miaka 40 na kuendelea yupo katika hatari ya kupata matatizo mbalimbali ya kiafya.

Matatizo hayo ni pamoja na saratani kama vile ya shingo ya uzazi na matiti na magonjwa yasiyoambukiza kama magonjwa ya moyo, kisukari, kiharusi, magonjwa sugu ya figo, unene uliokithiri na magonjwa ya akili.

Pia magonjwa ya kuambukiza, ikiwamo maambuzi ya virusi vya Ukimwi (VVU), TB, malaria na magonjwa yanayoshambulia viungo vya uzazi, ikiwamo yanayoenea kwa njia ya kujamiiana.

Kuna mambo 10 ambayo wanawake wazee wanapaswa kushikamana nayo ili kujikinga na magonjwa na hatimaye kuwa timamu kiafya na kuishi maisha marefu.

Moja, inahitajika kuepuka ulaji holela wa vyakula, ikiwamo chumvi na sukari nyingi, wanga na mafuta mengi na badala yake wale zaidi mbogamboga na matunda.

Umri unaposonga na kinga nayo hushuka, hivyo ni rahisi kupata magonjwa yanayoshambulia mfumo wa chakula, ikiwamo usugu wa vimelea katika vyakula. Kunywa maji ya kutosha angalau glasi 10 kwa siku.

Pili, fanya mazoezi mepesi na kazi zinazoushughulisha mwili. Kwa siku angalau fanya mazoezi ya kutembea dakika 30 hadi 60 au tembea kilomita mbili katika siku tano za wiki. Fanya shughuli za nyumbani kama za bustani na usafi wa mazingira ya ndani.

Tatu, fanya uchunguzi wa kiafya, muhimu kujitokeza wakati wa uchunguzi wa matatizo ya kiafya yanayomgusa mwanamke moja kwa moja, ikiwamo saratani ya mlango wa uzazi na matiti. Pia fanya uchunguzi wa jumla angalau mara moja kwa miezi sita.

Nne, zingatia elimu ya afya, hasa zile za kampeni za kitaifa, ikiwamo namna ya kujichunguza matiti na maeneo ya uzazi. Lengo ni kuweza kubaini ishara za awali za saratani, ikiwamo ya matiti na shingo ya uzazi.

Tano, shikamana na matibabu yako, endapo unaugua magonjwa ya muda mrefu, ikiwamo VVU, shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya akili hakikisha unashikamana na matibabu na ushauri.

Sita, epuka matibabu yasiyo rasmi. Ni kawaida baadhi ya wanawake huvutika katika matibabu yanayosambaa mitandaoni au mtaani ambayo mengine hutolewa na watu wasio na ujuzi wa mambo ya tiba. Mfano, dawa za kupunguza unene, vipodozi na virutubisho ambavyo havijathibitishwa na mamlaka ya dawa na vifaa tiba.

Saba, hakikisha una uhusiano mzuri na jamii na kifamilia, kwani matatizo yoyote ya kimahusiano yanaweza kukuweka katika hatari ya kupata matatizo ya kiakili.

Nane, kulala na kupumzika. Ni muhimu kupata mapumziko na kulala maeneo rafiki yasiyo na usumbufu. Kiafya inashauriwa kulala saa 6 hadi 8 kwa siku. Ikumbukwe umri ukisonga hatari ya kupata matatizo ya usingizi huongezeka.

Tisa, hakikisha unajiongezea ufahamu kuhusu matatizo mbalimbali ya kiafya yanayowakabili wanawake wazee. Hii inasaidia kuchukua hatua za kujikinga mapema.

Kumi, umri wa uzee ni kihatarishi cha kupata magonjwa, hivyo ni muhimu kuwa na bima ya afya kabla ya kuumwa.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi