Connect with us

Kitaifa

Mambo sita kunufaisha Tanzania ziara ya Samia India

Dar es Salaam. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuanza ziara ya siku tatu nchini India, Tanzania itanufaika na mambo sita katika ziara hiyo itakayoanza Oktoba 8 hadi 11, mwaka huu.

Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba alipozungumzia ziara hiyo ambayo Rais Samia amepata mwaliko maalumu na viongozi wa Serikali ya India.

Maeneo ambayo Tanzania itanufaika ni pamoja na sekta za viwanda, afya, kilimo, elimu, maji na usafiri wa majini.

Akizungumzia sekta ya afya, Makamba alisema, “..inatarajiwa baada ya ziara hii, kutaanzishwa taasisi ya upandikizaji figo nchini, pia kutaanzishwa kiwanda cha kutengeneza chanjo ya binadamu na wanyama, ambapo maandalizi yanaendelea.

“Tutaongeza ushirikiano kati ya hospitali za Tanzania na India, ikiwemo kuboresha uwezo na utaalamu na weledi wa matibabu katika taasisi hizi.”

Mmoja wa wataalamu bingwa wa magonjwa ya figo, Dk Shija Kessy katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alisema, “kumekuwa na changamoto ya ugonjwa figo kuongezeka, hasa ile iliyopo hatua ya mwisho, hili tatizo linaongezeka kutokana na magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo kisukari na presha ambayo yana madhara katika figo.”

Alisema kutokana na kasi ya kuongeza magonjwa hayo, Taifa linahitaji mikakati madhubuti ya kukabiliana nayo, ikiwemo kuwepo kwa taasisi maalumu.

“Taasisi itakayoanzishwa haitajikita kutibu ugonjwa, bali itaongeza elimu kwa wananchi ya namna ya kujikinga na magonjwa yanayosababisha figo kushindwa kufanya kazi. Matokea yake kutakuwa na wataalamu wanaojua tatizo la figo kwa ukubwa.

“Pia itasaidia kuvutia wagonjwa kutoka mataifa ya jirani kuja Tanzania kupata matibabu na kuiwezesha nchi kupata fedha za kigeni. Gharama ya kupandikiza figo ni kati ya Sh 32 milioni hadi milioni 40 kwa mtu mmoja, uchunguzi na kulazwa kwa mwezi mzima,” alisema Dk Kessy.

Machi mwaka 2022 aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Alfelo Sichwale alisema Watanzania 5,800 wanahitaji huduma ya kusafisha damu au kupandikizwa figo.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), kila watu 10, mmoja mfumo wa utendaji kazi wa figo zake hauko vizuri. Hii ni sawa na makadirio ya asilimia 10 kwa wananchi wote kusumbuliwa na tatizo hilo, huku asilimia 2.4 wakipoteza maisha na asilimia 2.7 wakigundulika kwenye hatua ya mwisho.

Kuhusu elimu, Waziri Makamba alisema kutokana na uhusiano mzuri wa diplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizo, kumekuwa na mpango wa kubadilishana uzoefu. “Kama mnavyojua, India ni miongoni mwa mataifa yanayoongoza katika mapinduzi ya kidijitali, sasa matokeo ya ziara hii ni viwanda na wawekezaji kuja nchini,” alisema.

Matarajio mengine ya ziara hiyo, Waziri Makamba alisema ni kuvutia wawekezaji katika Teknolojia ya Habari ya Mawasiliano (Tehama).

“Tunatarajia viwanda vya simu janja kuwepo nchini, haya ni moja ya matokeo tunayoyatarajia baada ya ziara,” alisema.

Alisema India ni miongoni mwa mataifa ambayo vyanzo vikuu vya uwekezaji wake na biashara baina yake na Tanzania imekua kwa kasi kwa miaka ya hivi karibuni, kwani wawekezaji kutoka nchi hiyo wamekuwa wakiiona Tanzania kama sehemu sahihi ya biashara.

“Kama mnavyofahamu tunazalisha korosho na mbaazi, moja ya matokeo ya ziara ya Rais Samia ni kuhakikisha soko la bidhaa hizo linakuwa la uhakika na la kudumu, hasa kwa zao la mbaazi ili wakulima wetu wasiwe na mashaka,” alisema.

Kwa nyakati tofauti, wakulima wa mbaazi, hasa kutoka mikoa ya kusini wamekuwa wakihaha kutafuta soko la uhakika la bidhaa hiyo, lakini kwa maelezo ya Waziri Makamba huenda wakaondokana na kadhia hiyo baada ya ziara ya Rais Samia.

“Tunaamini wawekezaji wakubwa watashawishika kuja nchini, ikiwemo kuanzia kongani ya viwanda. Tumejipanga kuanza na ekari 10,000 na kampuni kubwa za India zitaanzisha viwanda nchini,” alisema Makamba.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi