Kitaifa
Hivi hapa vigezo watakaonufaika mikopo ya vyuo vya kati
Dar es Salaam. Hatimaye kilio cha kutokuwapo kwa utaratibu wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati kimepatiwa ufumbuzi, baada ya Serikali kutenga Sh48 bilioni kwa ajili ya mikopo hiyo 2023/2024.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda jana Jumatano Oktoba 5, 2023 jijini Dar es Salaam alizindua mwongozo wa utoaji mikopo kwa ngazi ya stashahada, ukizitaja fani sita za kipaumbele.
Mwongozo huu umezinduliwa jana, ikiwa ni takribani miezi saba baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kueleza kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kutoa mikopo kwa ngazi ya stashahada.
Katika mkutano wake wa jana, Waziri Mkenda alisema fedha hizo zitatolewa kwa wanafunzi 8,000 katika maeneo sita ya vipaumbele yenye uhitaji mkubwa wa wataalamu.
Aliyataja maeneo hayo ni afya na sayansi shirikishi, ualimu wa hisabati, fizikia na mafunzo ya amali, uhandisi na nishati, madini na sayansi ya ardhi na kilimo na mifugo.
Waziri Mkenda alisema kuwa maeneo hayo ya vipaumbele yamechaguliwa baada ya Serikali kufanya tathmini ya uhitaji mkubwa wa wataalamu katika ngazi ya kati.
“Serikali imejenga hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini kote ambavyo vinahitaji wataalamu. Serikali pia imejenga na kukarabati shule ambazo zinahitaji walimu wa sayansi pia inatekeleza mageuzi katika sekta za mafuta, gesi, madini na sekta ya kilimo.
“Baada ya kufanya tathmini tumeona tuanze na maeneo haya ili kuwapa fursa vijana wetu kupata ujuzi na kuweza kuajirika baada ya kuhitimu masomo yao,” alisema Profesa Mkenda.
Kutolewa kwa mwongozo huo kunatoa fursa ya kufunguliwa kwa dirisha la kupokea maombi kwa njia ya mtandao kwa siku 15, kuanzia Oktoba 7 hadi 22, mwaka huu.
“Niwasisitize waombaji watumie siku nne kusoma mwongozo na kuangalia vigezo ambavyo vimewekwa, maana usije ukaona afya ukafikiri kila fani ya afya itatolewa mkopo, kuna maeneo tumeyaangalia.
“Tusingependa kuona watu wanaostahili wanakosa mkopo kwa sababu ya kushindwa kuzingatia vigezo. Kitu kingine muhimu kwa waombaji ni kuwa baada ya kumaliza masomo, wanufaika watambue kurejesha mkopo kwa kiwango cha asilimia 15 kutoka kwenye mshahara wake wa mwezi,” alisema Profesa Mkenda.
Kauli za wadau
Akizungumzia hatua hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet), Dk Adolf Rugayugwa alisema inakwenda kuongeza idadi ya wataalamu wa kada za kati.
“Tumesubiri kwa muda mrefu suala hili, wanafunzi wa stashahada wakipata mikopo itaongeza idadi ya wanafunzi kwenye kada hii ambayo ni muhimu katika kutengeneza wafanyakazi.
“Kwa sasa ukiangalia takwimu, wenye shahada ni wengi kuliko wenye stashahada, kitu ambacho si kizuri, utendaji kazi unahitaji mchanganyiko wa kada hizi,” alisema Dk Rutayugwa.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la wanafunzi wa elimu ya juu Tanzania (Tahliso), Maria John amewataka wanafunzi wa stashahada kuchangamkia fursa hiyo, iliyiombwa kwa muda mrefu.
“Kwa muda mrefu tulilihitaji hili, tulimuomba Rais Samia na hatimaye ametusikia, linaenda kutekelezwa, wito wangu kwa wanafunzi tuitumie vyema fursa hii.
“Serikali imetupatia mikopo ili tusome, basi twende tukasome ili lengo la kutupatia mikopo hii litimie, tupate ujuzi na maarifa tulitumikie Taifa na tusisahau tunawajibika kuirejesha mikopo hii na wengine wapate,” alisema Maria.
Akizungumzia bidhaa hiyo mpya ya mikopo, Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB), Profesa Hamis Dihenga alisema ufuatiliaji wa kina utafanyika kuhakikisha mikopo hiyo inatolewa kwa ufanisi na kuwafikia walengwa.