Kitaifa
Bei mpya ya mafuta yazidi kung’ata

Dar es Salaam. Wakati ukitamani ya leo kuwa mazuri kuwa mazuri kuliko ya jana hali imekuwa tofauti kwa waendesha vyombo vya moto na wamiliki wa mitambo inayotumia mafuta baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kutangaza bei mpya za mafuta zitakazoanza mwezi Oktoba zikizidi kupanda.
Bei ya dizeli imezidi kupaa ikilinganishwa na mwezi Septemba huku moja ya sababu ikitajwa kuwa ni kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia.
Kwa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, James Mwainyekule jana Oktoba 3, 2023 imeonyesha jijini Dar es Salaam bei ya dizeli kwa lita ni Sh3,281, dizeli Sh3,448 na mafuta ya taa yakiuzwa Sh2,943.
Mkoa wa Dar es Salaam kwa mwezi Septemba bei za mafuta ilikuwa ikiuzwa petroli Sh3,213 na dizeli Sh3,259.
Hata hivyo kwa upande wa mikoa mingine yenye bandari zinazoshusha mafuta bei nayo imepanda; Mtwara dizeli ikiuzwa kwa lita Sh3,520, petroli Sh3,353 na mafuta ya taa Sh3,016.
Hali kadhalikwa bei ya mafuta pia imepaa kwa Mkoa wa Tanga ambapo kwa sasa lita moja ya petrol ni Sh3,327, dizeli Sh3,494 na mafuta ya taa ikifika Sh2,989.
Aidha, ukiachana na mikoa hiyo mitatu yenye bandari nako Arusha bei imezidi kung’ata bei zikiwa kama ifuatavyo, petrol ikiuzwa Sh3,365, dizeli Sh3,532 na mafuta ya taa Sh3,027.
Ewura imetaja sababu ya mabadiliko ya bei hizo za mafuta kwa mwezi Oktoba 2023 ikiwa ni kupanda kwa gharama za bidhaa hiyo katika soko la dunia hadi kufikia asilimia 4.21, gharama za uagizaji kufikia asilimia 17 kwa petroli, asilimia 62 kwa dizeli na asilimia 4 kwa mafuta ya taa.
Pia, uamuzi wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani (OPEC+) kupunguza uzalishaji na vikwazo vya kiuchumi ambavyo nchi ya Urusi imewekewa na mataifa ya magharibi.
