Connect with us

Kitaifa

Hii ndiyo Boeing 737-9 Max, tofauti yake na zilizopo

Dar es Salaam. Ndege mpya iliyonunuliwa na Serikali aina ya Boeing 737-9 Max inatarajiwa kuwasili nchini kesho kuungana na nyingine ambazo zinapeperusha twiga na bendera ya Tanzania.

Boeing 737 Max 9 ya Tanzania ipo angani kutokea Mji wa Seattle, inatarajiwa kuwasili nchini kesho Oktoba 3, 2023 katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Terminal I.  Mapokezi ya Ndege hiyo yataongozwa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango.

Pengine unaweza kujiuliza ndege hiyo ina uwezo gani na sifa zake nyingine ni zipi ikilinganishwa na ndege ambazo tayari zipo katika shirika la ndege la Tanzania (ATCL).

Uwezo wake wa kupakia abiria ni wastani wa abiria 220 kulingana na mpangilio wa ndani huku ikisafiri hadi umbali wa kilometa 6,110 bila kulazimika kutua.

Ndege hiyo ambayo toleo lake la kwanza lilitoka mwaka 2017 inatumia injini ya LEAP-1B ambayo inatengenezwa na CFM International ya Marekani. Gharama yake inatajwa kuwa Dola za Marekani milioni 128.9 hadi 135 (Sh323.79 bilioni hadi Sh339.12 bilioni).

Urefu wake ni mita 42.16 na upana wa mabawa yake ni mita 35.9 inaendeshwa na marubani wawili na wahudumu wa ndani ya ndege wanne. Tanzania ambayo imenunua jumla ya ndege mbili inakuwa nchi ya nne bara ni Afrika kumiliki ndege hiyo baada ya Nigeria (18), Ethiopia (17) na Afrika Kusini (5).

Jumla ya oda za Max 9 tangu mwaka 2017 ni 5651 hadi Agosti 31, 2023 hata hivyo zilizokwisha kufikishwa kwa wanunuzi ni 1298. kwa mwaka huu tayari wamewafikishia wateja wao ndege 344 nyingi zikiwa ni Max 9.

Ukiachana na ndege za ATR-72 na Bombardier Q400 zitumiaza injini za mapanga katika anga la Tanzania ndege za ndani za abiria zitumiazo injini ya ‘Jet’ ni Airbus A220-300 na Boeing 787-9 (Dreamliner) zote zinazoendeshwa na ATCL.

Tofauti kubwa ya Max 9 na A220 ni uwezo wa abiria kwani A220 uwezo wake wa juu ni kupakia abiria 160 wakati Max 9 uwezo wake wa juu ukiwa ni abiria 220.

Umbali wa kuruka bila kusimama Max ni Kilometa 6570 huku A220 ikiwa ni 6112 huku uwezo wa kupaa ukiwa na mzigo ni tani 67.5 kwa A220 na tani 88.3 kwa Max 9.

Spidi ni kilometa 840 kwa saa A220 huku ya Max 9 ikiwa pungu kwa Kilometa moja kwa saa (839). Bei ya A220-300 inatajwa kuwa Dola milioni 91.5 (Sh229.84 bilioni).

Ukizilinganisha ndege hizo mbili na Dreamliner imeziacha mbali, kwanza uwezo wake wa kupakia abiria ni 242 na ina uwezo wa kuruka ikiwa na uzani wa tani 227.9 huku uwezo wake wa juu ukiwa ni spidi ya kilometa 954 kwa saa.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi