Connect with us

Kitaifa

Nusu ya mitambo ya umeme Ubungo haifanyi kazi

Dar es Salaam. Baadhi ya maeneo yakiendelea kupata umeme kwa kufuata ratiba, imebainika nusu ya mitambo iliyopo kituo cha kuzalisha nishati hiyo cha Ubungo haifanyi kazi.

Hayo yamebainika jana, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga katika kituo hicho kilichopo jijini hapa.

Kapinga alisema mitambo sita kati ya 12 katika kituo cha Ubungo I imeharibika, huku mmoja kati ya mitatu katika kituo cha Ubungo II nao haufanyi kazi.

“Mitambo iliyoharibika ina uwezo wa kuzalisha megawati 43 kila mmoja, ni umeme mwingi sana. Tunaamini kama matengenezo yakikamilika kwa wakati hali ya upatikanaji wa umeme itaimarika,” alisema Kapinga.

Alitoa maelekezo kwa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kwenye kituo hicho kuhakikisha wanashughulikia tatizo la kukosekana umeme linalotokana na mitambo ya kituo cha Ubungo I kuzimika usiku wa kuamkia jana.

“Natoa maelekezo kwa watendaji kuhakikisha huduma ya umeme inarejea ndani ya saa sita kwenye maeneo ambayo umeme unakosekana kutokana na kuzimika kwa mitambo hii sita ambayo ndiyo inafanya kazi,” alisema Kapinga.

Alisema matengenezo yanahitajika kufanyika ndani ya muda mfupi, wa kati na mrefu, yanapaswa kukamilika kwa wakati ili kusaidia kuimarisha hali ya upatikanaji umeme kwa wananchi.

Pia aliwataka watendaji katika kituo hicho kuhakikisha wanakuwa na mpango madhubuti wa kufanya marekebisho kwa nyakati tofauti.

“Kwa sasa Wizara inaendelea kufanyia kazi maelekezo aliyoyatoa Rais Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kero ya kukatika kwa umeme inakoma ndani ya miezi sita na moja ya hatua ni pamoja na kufanya matengenezo ya mitambo hii ambayo imeharibika,” alisema.

Alisema hata kama wana mikakati mingi, wa kwanza uwe ni upatikanaji wa umeme, ndiyo maana ametoa saa kadhaa kuhakikisha nishati hiyo inapatikana.
Takribani siku nne zimepita tangu Rais Samia alipotoa maagizo kwa Mkurugenzi mpya wa Tanesco, Gissima Nyamo-Hanga kuhakikisha kero ya kukatika umeme inakwisha ndani ya miezi sita.
Maagizo hayo yalitokana na kero ya kukatika kwa nishati hiyo maeneo mbalimbali nchini, moja ya sababu inayotajwa ni kukosekana kwa mvua, hivyo kusababisha kupungua kwa kiwango cha maji katika vyanzo vinavyotumia maji kuzalisha umeme.

Rais Samia alimtaka Nyamo-Hanga kusimamia mchakato wa ukarabati wa mitambo unaoendelea, akisema ndiyo kazi yake ya kwanza ndani ya Tanesco.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano wiki hii, Nyamo- Hanga alisema kuna upungufu wa megawati 400 katika gridi ya Taifa zilizosababishwa na upungufu wa maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme, na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi zinazotumia nishati hiyo.

Alisema pia kuna matengenezo yanayoendelea katika baadhi ya mitambo ya Ubungo I na II na mingine ya gesi ya Kinyerezi.

Alisema kiwango cha upungufu kitaanza kutatuliwa polepole, wiki mbili zijazo tatizo litaanza kupungua.

Mkakati uliopo alisema ni kuongeza megawati 100 kila mwezi, hadi kufikia Machi mwakani changamoto iliyopo sasa itakuwa imekwisha.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi