Kitaifa

Wasomi wataja kasoro panga pangua ya Samia

Dar es Salaam. Mabadiliko ya ghafla na ya mara kwa mara katika uteuzi wa viongozi unaofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan yanaashiria kwamba kuna jambo haliko sawa ndani ya Serikali na hali hiyo inawajaza hofu watendaji, wachambuzi wa masuala ya utumishi na utawala wamesema.

Wachambuzi hao, wakiwemo wanazuoni, wamesema hali hiyo inachangiwa na kasoro katika vyombo na mfumo wa mamlaka za uteuzi.

Hoja hiyo inatokana na kujirudia kwa matukio ya Rais Samia kuteua na kutengua viongozi ghafla au kuwahamisha wengine hata kabla hawajajipanga kutekeleza majukumu yao mapya.

Jana Rais Samia alibainisha baadhi ya sababu za hali hiyo, akitaja kukosa taarifa za watendaji kuwa kunafanya awaondoe mapema baadhi yao.

Akihutubia baada ya hafla ya kuwaapisha wateule wapya jana, Rais Samia alisema, “tunaomba mtuletee taarifa za mnayoyafanya huko ndani, saa nyingine unaweza ukaamua lakini hujui unayemwondoa amefanya kazi gani.

“Lakini tukiwa na taarifa zenu hapa, unapopanga na kupangua unaweza kusema hapana huyu asitoke anaendelea kufanya kazi vizuri. Kwa hiyo kijana niliyemwondoa TTCL (Shirika la Mawasiliano Tanzania)kumbe alishafanya kazi nzuri sana, baadaye sasa ndiyo mwenyekiti wake wa bodi ananiletea taarifa,” alisema.

Kauli ya Rais Samia inalenga kilichofanyika Septemba 23, alipomteua Maharage Chande kuwa Mkurugenzi wa (TTCL) akitoka kuwa mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na siku moja baadaye akamteua kuwa Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania.

Papo hapo, aliyekuwa Mtendaji mkuu wa TTCL, Peter Ulanga alimwondoa akiahidi kumpangia kazi nyingine, siku mbili baadaye akamrejesha kwenye nafasi hiyo akisema hakuwa na taarifa za kutosha.

Hii si mara ya kwanza Rais Samia kufanya mabadiliko hayo ya ghafla, alifanya hivyo Agosti 30, mwaka huu, alipomteua Profesa Kennedy Gaston kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na siku iliyofuata Septemba 1 akamwapisha.

Lakini siku tatu baadaye, Septemba 3, mwaka huu alimtea katika wadhifa mpya wa naibu mwanasheria mkuu wa Serikali.

Jambo kama hilo, lilitokea pia kwa Alexander Mnyeti, mbunge wa Misungwi aliyeteuliwa Septemba 30, mwaka huu kuwa naibu waziri wa Kilimo, kabla ya kuapishwa alihamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Hata Thobias Mwesiga alikumbana na hali hiyo Aprili 4, 2021 alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), lakini kabla ya kuapishwa siku iliyofuata alitenguliwa na James Mataragio aliyekuwepo kabla ya uteuzi, aliteuliwa kuendelea na nafasi hiyo.

Dk Raphael Chegeni naye, aliuonja wadhifa wa Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa siku tatu kuanzia Julai 28, mwaka jana hadi Julai 31, mwaka huo, alipotenguliwa na nafasi yake kujazwa na Meja Jenerali Suleiman Mzee.

Kama hiyo haitoshi, katikati ya uapisho, David Kafulila alihamishwa na kutoka mkuu wa Mkoa wa Arusha aliokuwa amepewa kwenda Simiyu na John Mongella aliyekuwa Mwanza akahamishiwa Arusha.

Ukiacha mifano hiyo, wapo mawaziri lukuki waliohamishwa kutoka wizara moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi, akiwemo Mohammed Mchengerwa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenda Maliasili na Utalii kisha Ofisi ya Rais, Tawala za Rais na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Uhamisho kama huo pia, ulimkumba Dk Damas Ndumbaro, aliyetoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda Katiba na Sheria na sasa ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Dosari kwa mamlaka ya uteuzi

Akizungumza na Mwananchi kuhusu hali hiyo, aliyewahi kuwa katibu mkuu Utumishi, Ruth Mollel alisema inaonyesha uwepo wa dosari kwa mamlaka ya uteuzi.

Dosari hiyo, alisema unakosekana uchunguzi wa kutosha kwa anayetarajiwa kuteuliwa, hivyo mamlaka ya uteuzi inajikuta imeamua ikiwa na taarifa chache.

Hilo linathibitishwa na Rais Samia aliposema, “Maharage Chande niliona TTCL panakufaa zaidi, sasa baadaye nikagundua una biashara ndani ya TTCL, nikaona sasa nikupe Postamasta Mkuu.”

Kwa upande mwingine, Mama Mollel alisema kiongozi mtendaji inamchukua mwaka mmoja au mmoja na miezi mitano kuielewa vema taasisi na kutengeneza njia ya utendaji, hivyo akiondolewa mapema ni vigumu kuona matokeo ya kazi yake.

Mabadiliko hayo ya mara kwa mara, alisema yanaathiri utumishi wa umma na kwamba angalau kwa mawaziri si tatizo, kwa kuwa sehemu kubwa ya kazi zinaendeshwa na watendaji (wanaozielewa vema).

Kulingana na Mollel, mabadiliko hayo ni kikwazo cha kujiamini kwa watendaji hao, muda mwingi wana hofu ya iwapo wataendelea kutumikia nafasi walizonazo.

“Hii inafanya watu wasitulie, unatakiwa mtu ukae kwenye nafasi ukiwa vizuri, lakini unakaa kama umekaa upande, hujui utaondolewa saa ngapi, hii si sawa,” alisema Mollel, aliyewahi kuwa waziri kivuli wa utumishi.

Suluhu ya yote hayo, alisema ni kuzingatia nafasi za utendaji wasipewe watu kwa kigezo cha itikadi za kisiasa, wapewe wenye uwezo na eneo husika.

Pia, alishauri viongozi wanaotarajiwa kuteuliwa waandaliwe mapema kupitia mafunzo maalumu, kisha wakati wa uteuzi mamlaka zizingatie kanzidata ya waliofunzwa.

“Rais apelekewe majina matatu afanye uchaguzi wa nani anaona anafaa kuwa kwenye nafasi husika, hiyo itakomesha leo umempeleka huyu kesho yule,” alisema.

Wakati Mama Mollel akisema hayo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari, alisema kuna changamoto ya kukosekana umakini kwa mamlaka ya uteuzi.

Alisema uchunguzi wa anayeteuliwa unapaswa kufanyika kwa kina kujua taarifa zake kulingana na eneo analotarajia kwenda kusimamia na asipewe nafasi kwa taarifa nusunusu.

“Unapoteuliwa kuna ufuatiliaji mkubwa unaotakiwa kufanywa ili kuhakikisha unateua watu wanaoendana na kazi unayoitarajia,” alisema.

Usiri tatizo

Kasoro nyingine iliyotajwa na Profesa Bakari ni pale inapoamua kumteua mtu kwa siri, bila kumdokeza, ndiyo sababu wanatokea wanaogomea teuzi baada ya kuteuliwa.

“Utaratibu wa kawaida mtu anayeteuliwa anakuwa na taarifa za kitakachoendelea, lakini kukiwa na usiri kunakuwa na changamoto na wakati mwingine hata mtu anaweza kukataa,” alisema.

Kuhusu mabadiliko ya mara kwa mara, Profesa huyo alisema yanawavunja moyo watendaji, kwani pamoja na mipango mizuri wanayopanga huwa wanakosa imani iwapo watafanikiwa kuitekeleza wakiwa katika ofisi husika.

“Kidogo inaweza kuleta hali ya kupoteza kujiamini, hata taasisi au wizara husika inakwama kwa sababu akija huyu kabla hajatekeleza lengo anaondoka anakuja mwingine, wakati anajipanga anaondolewa,” alisema.

Hata hivyo, licha ya hayo yote, alisema mamlaka ya uteuzi haipaswi kulaumiwa, kwa kuwa mara nyingi wanaotenguliwa huonekana hawajafanya vizuri au zimepatikana taarifa mbaya kuwahusu.

“Inawezekana taarifa mbaya kumhusu mtu husika zimepatikana baada ya kuteuliwa, hiyo inaishawishi mamlaka ya uteuzi kufanya mabadiliko,” alisema.

Bandika bandua

Hoja hiyo imemwibua Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema kinachoendelea kinathibitisha kuwa CCM na Serikali yake hawajui wanapoipeleka nchi.

“Tunaona ni bandika bandua na suluhisho la hili ni kuwa na Katiba mpya ili kuwa na mifumo madhubuti ya uteuzi,” alisema.

Mbowe alisema kwa hali ya sasa ya uhaba wa dola, mgawo wa umeme na gharama za maisha, alitarajia Serikali ijielekeze kwenye kutatua hayo, lakini imejikita kwenye kuteua na kutengua akisema, “ni mvurugano tu.”

“Tunasisitiza tubadili Katiba ili kubadili mifumo ya nchi, tunaona CCM imepoteza uelekeo, wanachukuliwa makada wa CCM wanapelekwa katika utumishi wa umma.

“Kuna utaratibu wa kuwaingiza watu katika utumishi wa umma na kuwapandisha madaraja, sasa wanapelekwa kuwa wakurugenzi wa halmashauri, katika mambo kama hayo fedha zikiibwa na kuvurugwa utamlaumu nani,” alisema Mbowe.

Alisisitiza hoja ya Ruth kuwa, uteuzi unafanyika kisiasa akisema, “uteuzi wa nafasi za watumishi wa umma umekuwa wa kisiasa, haueleweki. Kila siku mtu anateuliwa, tunahamisha watu kwa kuwateua mabalozi, sasa tutateua mabalozi wangapi.”

Alisema katika kipindi cha takribani miaka miwili ya Rais Samia, “ameunda wizara mpya, unaongeza gharama za uendeshaji, sasa unajiuliza tatizo lipo kwa washauri wake au kina nani? Kwa kifupi Serikali imevurugwa, CCM imevurugwa na msaada unaoweza kuwasaidia ni kupata Katiba mpya.”

Kwa kinachoendelea sasa, alisema watumishi hawajiamini kwa kuwa hawajui watafukuzwa, kuhamishwa, kusimamishwa au kuteuliwa lini.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi