Connect with us

Kitaifa

Naibu Waziri abaini ucheleweshaji miradi ya TPA

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameitaka Mamlaka ya Bandari (TPA) kuhakikisha inaongeza usimamizi katika utekelezaji wa miradi ili iweze kukamilika kwa wakati.

Hiyo ni kutokana na kile alichokieleza kuwa, kumekuwa na tabia ya miradi kutekelezwa nje ya muda huku akitolea mfano wa baadhi ya maeneo ambayo amewahi kutembea kukuta mkataba unaonyesha utekelezaji ni miezi 24 lakini hadi mwezi wa 26 haujatekelezwa.

Pia kauli hiyo imekuja ikiwa ni muda mchache tangu kutembelea eneo ambalo utafanyika uunganishaji wa bandari na reli ya kisasa (SGR).

Kihenzile amesema usimamizi mzuri ndiyo utakaofanya miradi kukamilika kwa wakati na kuleta faida hivyo itasaidia viongozi katika utendaji.

“Miradi hii inasubiriwa, thamani ya miradi kama ilivyokusudiwa, haya mambo mawili yakifanyika vizuri tunaweza kuwa tumeitendea haki Taifa letu,” amesema Kihenzile.

Aliyazungumza hayo leo Jumanne Septemba 26, 2023 wakati akifanya majumuisho baada ya kufanya ziara katika maeneo mbalimbali ndani ya Bandari ya Dar es Salaam ikiwemo eneo la kushushia mafuta,  magari, kontena, makasha na gati inayohudumia majahazi.

Kihenzile alitumia nafasi hiyo kuwataka watumishi wa bandari kuziba masikio juu ya yale yanayoendelea mitaani kwa kile alichokieleza kuwa dhamira ya serikali wanaifahamu na manufaa yake.

Ameitaka TPA kuangalia bandari zinazofanya kazi kwa ufanisi kati ya 86 zilizopo nchini ili kujua namna ya kuziwezesha zaidi.

“Tuangalie tumetumia ngapi, inawezekanaje Kenya anayetegemea Bandari ya Mombasa akahudumia mizigo tani milioni 30 kuliko Tanzania, hatuna haja ya kulegalega ndiyo maana jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kuhakikisha kuwa mipango mingi inafanikiwa,” amesema Kihenzile.

Awali, alipokuwa akizungumzia uunganishaji wa reli ya kisasa kwenda bandarini, Mrisho Suleiman Mrisho ambaye ni Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam amesema utekelezaji wa reli hiyo unaendelea na unatarajiwa kutumia miaka miwili kukamilika kwake.

Amesema katika utekelezaji wa mradi huo kuna baadhi ya majengo yatabomolewa ndani ya bandari kwa sababu inatakiwa kuwapo kwa eneo maalumu la kuhudumia kontena za kwenye behewa.

“Sasa hapo ndiyo mifumo yote itawekewa mashine kubwa za kubeba kontena kutoka kwenye meli kwenda kwenye behewa,” amesema Mrisho.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi