Kitaifa
Kama ndoa yako haijafuata hatua hii basi ni batili
Moshi. Ni kama hukumu ya Mahakama iliyoharamisha ndoa ya mbunge wa zamani wa viti maalumu (CCM), Vicky Kamata na Dk Servacius Likwelile imewaamsha wanandoa wengi kuhusu uhalali wa ndoa walizonazo mbele ya macho ya sheria.
Hukumu hiyo inaelezwa kuibua mambo matatu ili ndoa iwe halali, moja ni lazima kama ni ndoa ya kikristo, anayeoa au kuolewa asiwe na ndoa nyingine hai na pili cheti cha ndoa lazima kisajiliwe Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).
Mbali na masharti hayo, tatu ni lazima anayefungisha awe na leseni ya Rita.
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kanisa Katoliki, Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) na baadhi ya makanisa ya Kilokole, wamefunguka taratibu zinazotumika lakini hofu inayojitokeza ni kwa makanisa yaliyoanzishwa kiholela.
Hii imeibua hofu kwamba huenda baadhi ya ndoa zilizofungwa katika baadhi ya makanisa hayo zikawa hazina uhalali mbele ya sheria kwa kuwa jukumu la kusajili ndoa zao Rita linaachwa kwa wanandoa na hakuna uthibitisho wa kuwa na leseni.
Hukumu hiyo imeibua tatizo la kimfumo, kwamba wanandoa wengi wanapofunga ndoa na kwenda ukumbini kusherehekea na kwenda fungate, mambo yanaishia hapo na hakuna mfumo unaowajulisha ndoa yao tayari imesajiliwa Rita.
Tatizo lingine liko kwa baadhi ya wanandoa waliotengana kienyeji kwa miaka kadhaa bila ndoa hiyo kuhitimishwa na Mahakama kwa kutoa talaka na huamua kufunga ndoa nyingine ama kwa siri au waziwazi.
Tatizo hilo lipo pia kwenye talaka, kwani baada ya Mahakama kuvunja ndoa na kutoa talaka na wanandoa kutakiwa kurejesha vyeti ili vifutwe, badala yake huridhika na nakala ya hukumu na maisha kuendelea kama ilivyo kwenye ndoa.
Mathalan, takwimu za Rita zinaonyesha mwaka 2018, wakala huo ulisajili talaka 3,814 nchi nzima, ikasema idadi ya talaka inaweza kuwa kubwa na mfano ni Kilimanjaro mwaka huo ulisajili talaka tano, wakati Mahakama ina talaka 77.
Akizungumza na gazeti hili jana, Emily John, mkazi wa Kiborlon mjini Moshi, alisema hukumu ya Vicky Kamata imemfungua mambo mengi ambayo alikuwa anayachukulia kimazoea kama suala la kusajili ndoa na talaka mamlaka ya Rita.
“Hii hukumu imenifanya nianze kufuatilia Rita na nimesoma mahali wanasema gharama za kusajili ndoa ambayo haijasajiliwa ni Sh40,000 na vivyo hivyo kupata cheti cha talaka ni Sh40,000. Sijui kama watu wanajua hili.
“Jambo linalonitatiza ni pale tunapokuwa tumefunga ndoa kanisani, ni wajibu wa kanisa au wanandoa kwenda kusajili ndoa au tukishafunga tukapewa vyeti ndio nitolee. Hii hukumu ya Vicky ina mambo mengi,” alisema.
Salome Nestory, alitilia mashaka ndoa zinazofungwa katika makanisa yanayoshamiri hivi karibuni mitaani akisema ana wasiwasi kama wanaozifungisha wanakuwa na leseni za Rita, hivyo kuna haja ya wanaofunga kujiridhisha kwanza.
Mwaka 2019, Meneja Uhusiano wa Rita, Josephat Kimaro alikaririwa na gazeti hili katika mahojiano maalumu akisema baada ya mahakama kutoa talaka, aliyepewa tuzo hiyo anawajibika kuisajili talaka hiyo Rita.
“Unajua utaratibu ni kwamba wakishamalizana huko mahakamani na talaka ikatolewa, sheria inataka huo uamuzi uletwe Rita ili usajiliwe na hapo ndio inahesabika ni talaka,” alisema Kimaro katika mahojiano hayo.
Pia Kimaro alinukuliwa akisema wakati huo kulikuwa na mazungumzo yanaendelea na Muhimili wa Mahakama kupitia mpango wa e-system, ili kuunganisha mahakama na Rita ili hukumu ya talaka inapotoka, Rita waione.
Kilichobainika ndoa ya Vicky Kamata
Vicky Kamata aliyepata umaarufu katika medani za siasa na muziki, alifunga ndoa na Dk Likwelile Januari 30, 2016 katika Kanisa la Deliverance and Restoration jijini Arusha na kupewa cheti cha ndoa namba 0580353 na kuishi naye kwa miaka saba.
Hata hivyo, baada ya Dk Likwelile kufariki Februari 19, 2021 na mtoto wake wa kiume, Raymond Likwelile kuomba kuteuliwa msimamizi wa mirathi na Vicky Kamata kupinga, Mahakama iliamua kuwa yeye hakuwa mke halali bali kimada.
Familia ya Dk Likwelile ambayo ilitoa ushahidi Mahakamani, ilisema ndoa ya wawili hao haikuwa halali kwa kuwa baba yao alikuwa na ndoa ya Kikristo na mama yao aitwaye Mary Ibrahim, iliyofungwa 1986 na talaka haijawahi kutolewa.
Licha ya Vicky kuwasilisha cheti cha ndoa, ofisa aliyetoa ushahidi kwa niaba ya Rita alikana kukitambua cheti hicho na kwamba hakipo kwenye kumbukumbu za Rita.
Viongozi wa dini wafunguka
Katibu Mkuu wa Baraza la Maasofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima alisema kabla kanisa halijafungisha ndoa, ni lazima kujiridhisha hakuna ndoa nyingine kati ya wawili hao na anayefungisha lazima awe na leseni.
Padri Kitima alisema kwa Kanisa Katoliki, ndoa huweza kufungishwa na askofu, padri au shemasi lakini ni lazima awe na leseni inayotolewa na Rita na baada ya ndoa kufungwa, kanisa hutoa taarifa kwa Rita ya taarifa za ndoa hiyo.
Mchungaji kiongozi wa Usharika wa Kiborlon wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fred Njama alisema baada ya kufungisha ndoa, kanisa huwajibika kurudisha Rita nakala ya cheti kimoja cha ndoa.
“Sisi tunanunua vitabu Rita tunafungisha ndoa na kunakuwa na vyeti vinne, mke anapewa nakala halisi na mume anapewa nakala. Kwenye kitabu kunabaki nakala kwa hiyo moja inarudi Rita na nyingine inabaki usharikani kanisani,” alisema.
Mchungaji Njama naye alisisitiza anayefungisha lazima awe na leseni kutoka Rita.
Kwa upande wake, Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Born Again Christian Gathering lililopo Sanawari Jijini Arusha, Shalom Muzo alisema baada ya ndoa, kila mwanandoa anakaa na cha kwake na ni lazima ndoa itangazwe kanisani kwa wiki nne kabla ya kufungwa.
Mchungaji Muzo alisema wanandoa wakishaoana huwa hakuna kuachana na suala la kwenda kusajili vyeti vyao Rita ni wajibu wa wanandoa.
Katibu wa Bakwata Mkoa Kilimanjaro, Awadhi Lema alisema kwa waislamu si kila sheikh anaruhusiwa kufungisha ndoa japo kila sheikh anaweza kufungisha ndoa.
“Kila sheikh anaweza kufungisha ndoa kulingana na kila mwanazuoni ana elimu ya kufungisha ndoa, lakini kuhusu vitabu vya vyeti kwa upande wa Bakwata wanapewa masheikh maalumu wenye leseni za kufungisha ndoa.
“Kwa hiyo tukishafungisha hivi vitini tunarudisha Rita wana ofisi zao pale kwa DC (mkuu wa wilaya),” alisema na kuongeza; “Sasa kujua kama vyeti vyao vimesajiliwa Rita ama la hilo sasa linawahusu wanandoa wenyewe kufuatilia.”
Askofu mstaafu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) ambaye sasa ni mchungaji kiongozi wa Kilimanjaro International Christian Centre (KICC), Dk Glorious Shoo alisema si kila mchungaji anafungisha ndoa, bali aliyesimikwa pekee.
“Chini ya kila cheti panakuwepo na nakala ambayo nakala moja inabaki kanisani na nakala ya pili inatumwa Rita. Kwa hiyo inafungashwa inatumwa Rita kwa ajili ya kusajiliwa kwa ndoa ile au kuingizwa kwenye kumbukumbu,”alieleza.