Kitaifa
Uozo watisha ofisi za umma
Mwanza. Saa 144 za ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika mikoa ya Kigoma na Kagera zimeibua mambo mazito, hali inayotafsiri kuwa upo uozo wa kutisha katika ofisi za umma.
Ndani ya saa hizo, takriban viongozi, watendaji na watumishi 12 wa halmashauri na taasisi za Serikali katika mikoa hiyo wameonja joto ya jiwe, ama kwa kusimamishwa kazi, kuhamishwa vituo na wengine wakichunguzwa kwa madai ya ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka au upotevu wa fedha na rasilimali za umma.
Haya yanayotokea katika ziara ya Waziri Mkuu ni mwendelezo wa mengi yanayoshuhudiwa katika ziara nyingine za viongozi wa kitaifa akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wake, Dk Phillip Mpango katika maeneo tofauti nchini.
Usimamizi duni, kutowajibika na ubadhirifu wa fedha na rasilimali za umma ni baadhi tu ya yanayoibuliwa wakati wa ziara za viongozi hao, hadi unaweza kujiuliza ikiwa ziara zitafanyika nchi nzima hali itakuwaje.
Akizungumzia mapungufu ya kiutendaji, ukiwemo uwajibikaji duni na ubadhirifu wa fedha na mali za umma, mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na maendeleo ya jamii, Shilinde Ngalula alisema kiuhalisia, mambo si shwari katika halmashauri na ofisi nyingi za umma nchini.
“Uwajibikaji katika ofisi za umma umeshuka kwa kasi, wananchi kila kona wanalalamikia utendaji duni wa baadhi ya viongozi na watendaji.
“Ziara za Rais, Makamu wake Dk Mpango na Waziri Mkuu Majaliwa ni uthibitisho kuwa mambo si shwari huko chini. Muda umefika wahusika wawajibishwe,’’ alisema Ngalula.
Alishauri kuwepo mfumo wa kupima utendaji na uwajibikaji wa viongozi, watendaji na watumishi katika ofisi za umma huku udhibiti wa fedha na rasilimali ukiwa moja ya vipengele muhimu.
“Viongozi karibia wote kuanzia Rais Samia, Makamu wake na Waziri Mkuu walikuwa katika Serikali iliyopita, walichapa kazi na waliwajibisha viongozi na watendaji walioshindwa kuwajibika, sijui kimetokea nini. Nashauri sasa waanze kuchukua hatua kuwawajibisha watendaji bila kuwaonea muhali,’’ alisema Ngalula.
Alitaja kutofanya kazi kwa mfumo wa malipo ya kodi, ushuru na mapato ya Serikali na kukatika kwa umeme nchini, kuwa miongoni mwa kero katika siku za hivi karibuni zinazopaswa kufuatiliwa na kushughulikiwa kwa karibu na Rais Samia, Dk Mpango na Majaliwa.
“Viongozi na watendaji katika ofisi za umma hivi sasa wanafanya watakavyo bila hofu…mtu anaweza kuhangaika na mfumo wa kulipia kodi, ushuru na mapato ya Serikali kwa siku nzima bila mafanikio. Rais na wasaidizi wake lazima wachukue hatua,’’ alisema Shilinde
Shilinde anaungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk George Kahangwa aliyesema hali iliyopo inachangiwa na suala la maadili kwa wafanyakazi kushuka.
“Watu wanakuwa hawana uaminifu, hivyo wanapokabidhiwa dhamana za kusimamia wanajijenga wao wenyewe. Kwa watu wa aina hiyo lazima hatua za kisheria ziendelee kuchukuliwa,” alisema.
Alisema kuna baadhi ya maeneo wanafanya kwa kushirikiana, hivyo mtandao unaotengenezwa unapaswa kufuatiliwa na ukibainika uchukuliwe hatua.
“Tena (Serikali) iwawajibishe kwelikweli na wawajibishwe hadharani kila mmoja aone,” alisisitiza. Dk Kahangwa alisema baadhi “wanakuwa na presha za maisha zinawafanya wanatumia mbinu zisizostahiki kupata fedha. Fikiria kama unaishi Dar es Salaam ukiangalia kama bei za viwanja, nyumba unaona haziendani na mishahara ya Watanzania wengi, hapo ndipo watu wanalazimika kutumia njia nyingine.”
Mhadhiri huyo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa UDSM (Udasa) alishauri Serikali kuangalia mifumo ya fedha ili kuzuia mianya ya ubadhirifu inayotokea.
Wanachokisema wataalamu hao, kinafanana na alichoeleza Edina Maro, mjasiriamali mkazi wa Jiji la Mwanza, aliyepongeza hatua zinazochukuliwa dhidi ya viongozi, watendaji na watumishi wasiowajibika, huku akionyesha kuwa hatua hizo zisiwe za zimamoto kwa sababu ya uchaguzi unaokaribia.
Upimaji kuanza Oktoba 16
Jana, gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa kujua mikakati ya kumaliza tatizo hilo ambapo alisema, “kwa muda mrefu tumekuwa na watumishi wengi hawapati mafunzo ya kukumbushwa jinsi ya kuondoa ajali kazini na hali hii imesababisha kuwa na watendaji wasiokuwa na uwezo wa kutosha na wengine wanaingia kwenye mkumbo wa kimaadili.
Mchengerwa alisema “kumekuwa na utendaji wa kimazoea unaohitaji ufuatiliaji na uwajibikaji na tumekuja na mpango wa kupima na kufuatilia kuanzia Oktoba 16, mwaka huu. Kila mtendaji au mtumishi wa chini atawajibika kujaza fomu hii.
“Kupitia mfumo huu, tutafahamu rekodi za watumishi wote na utaratibu huu utatusaidia sana. Utakuwa ni kipimo kwa mfano kwa mkoa, mtendaji wa Dar es Salaam, wilaya ya Temeke akikosea au kushindwa kuwajibika vyema basi mkoa mzima unakuwa na upungufu na kutakuwa na alama zinatolewa kila mwezi.
“Kila mwezi tutakuwa tunajua alama za mtu mmoja, kimkoa. Kwa hiyo mkuu wa mkoa, wilaya atapaswa kusimamia hili na hii itawafanya watoke ofisini na kwenda kwa wananchi kwani mfumo huu ni mnyororo, wilaya ikiharibu ni mkoa mzima,” alisema Mchengerwa.
Waziri huyo alisema mfumo huo utasaidia kubaini watumishi wasio na uwezo ili wajengewe uwezo.
“Yaani ni mfumo utakaomfanya kila mmoja atekeleze wajibu wake ipasavyo na unaweza kupunguza haya matatizo tunayoyaona sasa,” alisema.
Saa 144 za Majaliwa
Wakati wadau hao wakitoa kauli hizo, ziara ya Majaliwa katika mikoa ya Kigoma na Kagera imedhihirisha ulegevu katika usimamizi, uwajibikaji na udhibiti wa fedha na rasilimali za umma miongoni mwa baadhi ya watendaji.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Zainab Mbunda na Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, Majid Mabanga ni miongoni mwa waliojikuta wakiingia kikaangoni baada ya Majaliwa kuagiza mamlaka zinazohusika ziwasimamishe kazi.
Pamoja na kuwasimamisha kazi watendaji hao, waziri mkuu aliahidi kutuma timu maalumu ya uchunguzi wilayani Kigoma kufuatilia upotevu wa fedha za umma unaodaiwa kuhusisha mtandao wa watumishi wasio waaminifu.
Alitolea wa Sh500 milioni kutoka Ofisi ya Rais, (Tamisemi) zilizotumwa Manispaa ya Kigoma na kukaa kwenye akaunti kwa muda lakini baadaye zikatoweka na hazijulikani zilitumika kufanya nini.
Kiongozi huyo alibaini pia uwepo wa matumizi mabaya ya fedha, makusanyo kidogo na mawakala kukaa na fedha mikononi badala ya kuzipeleka benki.
“Kuna watu wamejilipa posho ya Sh11 milioni kwa safari ya Dodoma. Pia wametumia Sh6 milioni kufanya matengenezo ya gari. Hili ni gari la aina gani? Wengine wametumia Sh9 milioni kwenye sherehe za Siku ya Mtoto wa Afrika na wengine wamejilipa Sh14 milioni kwenda kwenye sherehe za Nanenane Tabora, hivi mlikaa siku ngapi huko?” alihoji Waziri Mkuu.
Aliagiza timu hiyo ya uchunguzi kukamilisha kazi hiyo mapema na kuwasilisha taarifa kwa Waziri wa Nchi, Ofis ya Rais (Tamisemi), Mohamed Nchengerwa ambaye pia ametakiwa kwenda Kigoma mara moja kuchukua hatua.
Kishindo cha Majaliwa hakijawaacha salama wataalamu na watumishi 10 katika Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi ambao baadhi wamehamishwa, wengine wanachunguzwa huku wakiwa wameagizwa kurejesha mamilioni ya fedha za umma zinazotokana na makusanyo ya halmashauri.
Akiwa mpakani Mutukula, Majaliwa aliagiza kurejeshwa makao makuu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Ofisa Mfawidhi wa Kituo cha TRA cha Mutukula, Feisal Nassoro na maofisa watatu wa mapato, Gerald Mabula, George Mwakitalu na Emmanuel Malima kwa tuhuma za kudharau mamlaka na kuikosesha Serikali mapato.
Kuhusu mapato ya Serikali, Majaliwa aliagiza kufuatiliwa kwa watumishi sita wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi wanaodaiwa kutowasilisha fedha za makusanyo za Julai na Agosti, mwaka huu.
Aliwataja watumishi hao ni Chrispin Mbuga, Andrephnus Kalisa, Nashrath Buyungilo, Lusiana Irunde, Issack Sadick na Willington Mutabilwa ambao ni watoza ushuru wa halmashauri wanaodaiwa kutowasilisha zaidi ya Sh37 milioni.