Kitaifa
Siku 729 za Chande, Issa Tanesco
Dar es Salaam. Kukosekana kwa umeme katika maeneo mbalimbali nchini kunatajwa kuwa kunaweza kuchangia kuondolewa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Maharage Chande na Mwenyekiti wa Bodi, Omari Issa.
Chande alikuwa amebakisha siku mbili pekee kufikisha miaka miwili ya utumishi ndani ya Tanesco tangu alipoteuliwa Septemba 25, 2021 akichukua nafasi ya Dk Tito Mwinuka.
Miongoni mwa alama aliyoiacha Chande katika kuliongoza shirika hilo kubwa kwa mali kuliko yote nchini ni ufanisi wa mawasiliano kwa umma na uanzishaji wa matumizi ya teknolojia katika kuunganisha wateja wapya kupitia programu ya Ni-conekt ambayo inatajwa kupunguza msongamano na gharama wakati wa kuomba kuunganishiwa nishati hiyo.
Rais Samia Suluhu Hassan, jana alimteua Gissima Nyamo-Hanga kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco akichukua nafasi ya Chande, aliyehamishiwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Nyamo-Hanga aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).
Rais Samia pia amemteua Meja Jenerali Paul Simuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, huku taarifa ya Ikulu ikieleza Issa ataendelea na majukumu mengine aliyopangiwa katika Ofisi ya Rais – Tume ya Mipango.
Mabadiliko hayo ya Rais yanafanyika kipindi ambacho tatizo la kukosekana umeme wa uhakika linatikisa sehemu tofauti za nchi, huku vilio vya watu wa kawaida, wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo vikisika kila upande.
Katika siku za hivi karibuni wananchi wamekuwa wakilalamika shughuli zao za uzalishaji kukwama kutokana na kukosekana kwa umeme.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Uwekezaji wa Tanesco, Declan Mhaiki, alinukuliwa akisema kupungua kwa maji na kuongezeka kwa mahitaji ya nishati hiyo ndiyo sababu ya tatizo lililopo.
Maoni ya wadau
Akizungumzia mabadiliko hayo, Dk Donalth Olomi, ambaye ni mtaalamu wa uchumi na biashara, alisema Tanesco linahitaji viongozi watakaokaa kwa muda mrefu walisome, wajue tatizo na namna ya kukabiliana nalo na si kuhamishwa kwa kuwa haiwezi kuwa suluhisho.
Mtaalamu na mchambuzi wa siasa, Dk Paul Luisulie alisema kibarua kikubwa watakachokutana nacho viongozi hao ni kuhakikisha watu wanapata umeme wa uhakika na kuondoa ule wa ratiba.
Alisema hilo litawezekana ikiwa watatafuta kiini cha tatizo na kukitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Alisema kufanya mabadiliko ya uongozi huwakumbusha uwajibikaji viongozi wanaoteuliwa kuwa kama hawatakidhi mahitaji yaliyokusudiwa basi wataondolewa katika nafasi zao.
Kwa upande wao, wananchi wengine wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu mabadiliko hayo, hisia za baadhi yao ni kwamba hatua iliyochukuliwa na Rais Samia italeta nafuu kwa changamoto wanazopitia sasa.
“Kuondolewa mkurugenzi wa Tanesco ni hatua nzuri, naamini mpya atakuwa na mipango mipya ya kushughulikia tatizo lililopo, muhimu ni watumishi waliobaki kujua wanachohitaji wananchi,” alisema Said Salumu.
Uteuzi wa Chande, Bodi
Aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba aliwahi kueleza kuwa uteuzi wa Chande na Bodi ya wakurugenzi wa Tanesco haikuwa rahisi, lakini alijenga hoja kwa Rais Samia na akaeleweka.
Alisema kabla ya uteuzi wa Chande alikuwa na mahojiano naye, alimuuliza akipewa Tanesco ataifanyia nini na majibu yalikuwa ni kuanza na watu (wafanyakazi wa Tanesco) kisha wateja.
Makamba alisema, “Baada ya hapo nilienda kumuona Rais (Samia Suluhu Hassan) nikamuambia nadhani tumepata mtu sahihi ambaye atatusaidia,” alisema.
Alisema uteuzi wa Chande uliibua hoja kuwa mteule si fundi umeme na hilo shirika ni la umeme, lakini alijibu kuwa shirika lina mafundi wa kutosha linachohitaji ni kiongozi.
“Nikawaambia kuna mafundi na kuna uongozi, nyuma yake kutakuwa na mafundi wengi wa kumsaidia na kwa sababu tunaomfahamu ataweza kuwashawishi waweze kuungana naye katika dira atakayoiweka,” alisema Makamba.
Alisema maneno hayohayo pia yaliibuka wakati alipofanya uteuzi wa bodi, kwa kuwa watu walisema anataka kulipeleka wapi shirika hilo kwa kile alichokieleza kuwa watu wamezoea wastaafu tu.
Makamba alisema aliamua kuchagua bodi iliyokuwapo kwa sababu aliamini Tanesco ni shirika la umma na kihandisi, lakini pia ni shirika la kibiashara na huduma, misingi ya uendeshaji biashara na misingi ya uendeshaji wa taasisi zinazotoa huduma na biashara hazibadiliki hata zikiwa za umma na binafsi.
“Sisi tulikuwa tunadhani kuwa mashirika ya binafsi yana wanahisa ambao wanachukua mikopo ambayo lazima warudishe na umakini wa bodi na menejimenti, hivyo tukaweka watu wanaotoka huko ili waje watusaidie,” alisema Makamba.
Kumbukumbu
Kwa upande wake, Dk Tobias Swai, mhadhiri mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) alisema Maharage amefanikisha mageuzi katika uendeshaji Tanesco na kuifanya kuwa ya kidijitali.
“Tukumbuke kuwa umeme ni hitaji la muhimu ambalo likikosekana watu watapiga kelele, alikuja akakuta shirika liko kwenye hali fulani, amefanya anachoweza, amefanya mabadiliko ya vitu kama miundombinu lakini mahitaji ya umeme yanakua, viwanda vinaongezeka na watumiaji wa kawaida wanaongezeka,” alisema Dk Swai.
Alisema mabadiliko hayo ni ya kawaida na yanalenga kupata anayeendana vizuri na eneo husika, lakini akitoa angalizo kuwa kubadili viongozi kisiasa katika mashirika ya aina hiyo ni ngumu kupata matokeo chanya.
“Sehemu kama hii watu waombe kazi, wapewe vitu wanavyopaswa kufanya wakiwa humo, wajipime na wapimwe kwa kazi waliyofanya,” alisema Dk Swai.
Miongoni mwa mambo atakayokumbukwa nayo kwa mujibu wa Greyson Mgonja, mchambuzi wa masuala ya maendeleo ya jamii ni namna alivyobadili kitengo cha mawasiliano Tanesco.