Connect with us

Kitaifa

Vurugu la ubinafsishaji Bandari Zanzibar bado halijapoa

Unguja. Vuguvugu la mabadiliko ya uendeshaji wa Bandari ya Malindi baada ya kukabidhiwa kwa mwekezaji bado halijapoa, sasa wamiliki wa meli wameibuka wakilalamikia gharama za kulipia meli kutia nanga.

Wamesema hali hiyo huenda ikasababisha kuongezeka kwa gharama za bidhaa.
Tangu Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) lilipokabidhi uendeshaji wa bandari hiyo kwa mwekezaji Kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) ya Ufaransa, Septemba 18, mwaka huu kumeibuka malalamiko ya kuongezeka kwa ushuru na kusababisha baadhi ya shughuli kusimama.

Wadau wa bandari, hususan wa majahazi wanalalamikia kupandishiwa ushuru mara mbili ya bei iliyokuwapo awali.

Wakizungumza na Mwananchi, wamiliki wa meli walisema iwapo yasipofanyika mabadiliko ya haraka, athari zitajitokeza, hususan kwa wananchi wa kawaida kwa sababu bidhaa zitapanda bei.

Mansour Said, mmiliki wa meli alisema mpaka sasa kuna meli tatu zimezuiwa kutia nanga kwa sababu hazijalipiwa. “Huu utaratibu wa kuanza kulipia meli kabla ya kufika bandarini unaibua changamoto mpya, kwa kawaida meli inatia nanga ndipo unalipa, maana kwanza wahusika washushe mzigo.

“Pia gharama za kulipia zipo juu ikilinganishwa na bandari nyingine, tunalipa Dola tatu za Marekani (Sh7,500) kwa tani moja, wakati Bandari za Dar es Salaam na Mombasa tunalipa Dola mbili (Sh5,000)” amesema.

Mmiliki mwingine wa meli, Hamad Khamis, maarufu kama Kisu, alisema hatua hiyo inasababisha hata makasha yasishushwe kwa wakati kutokana na ongezeko la gharama.
Alisema kwa sasa bei ya saruji mfuko mmoja ni Sh17,000, lakini hali hiyo ikiendelea utauzwa hadi Sh20,000 kwa sababu hakuna mfanyabiashara atakubali kuuza bidhaa kwa hasara.

“Serikali inapaswa kuyaangalia mambo haya kwa umakini,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wakala wa Forodha Zanzibar, Omar Mussa alisema pamoja na changamoto hizo, unatakiwa uelewe wa pamoja kutokana na mabadiliko hayo.

Akizungumzia hilo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya alisema baadhi ya wafanyabiashara wameanza kutumia mwanya huo kwa kisingizio cha bandari kupandisha bei za bidhaa, akionya hawatakubali jambo hilo litokee.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohamed, alisema changamoto zinazojitokeza zinatokana na mabadiliko ya kiutendaji na uendeshaji, lakini zinashughulikiwa kwa kadiri inavyowezekana.

Juzi alipotembelea bandari hiyo, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Abdulla alisema Serikali kwa kushirikiana na mwekezaji itaendelea kutafuta njia bora za kuondoa changamoto hizo ndogondogo.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi