Connect with us

Kitaifa

Saa 48 za moto kwa watendaji halmashauri

Dar es Salaam. Kama kuna watu walio kwenye wakati mgumu kwa sasa serikalini, ni pamoja na watendaji wa halmashauri na wilaya mkoani Kigoma.

Ndani ya saa 48, vigogo wamekiona cha mtema kuni, baada ya baadhi yao kusimamishwa kazi kwa tuhuma mbalimbali, zikiwamo ubadhirifu na kushindwa kusimamia miradi.

Juzi akiwa wilayani Uvinza, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliagiza kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Zainab Mbunda na Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, Majid Mabanga.

Ukiondoa hao, mkoani Simiyu nako hakujapoa, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busega, Veronica Sayore.

Uchunguzi Kigoma

Jana, Waziri Mkuu, alisema atapeleka timu maalumu ya uchunguzi wilayani Kigoma, kuchunguza fedha zinazopotea kinyemela kupitia mtandao wa watumishi wasio waaminifu.
Alisema hayo jana, alipozungumza na viongozi wa dini, Serikali, Chama cha Mapinduzi (CCM) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF, uliopo Kigoma mjini.

Alisema fedha zinazotoka Serikali Kuu huwa zinatumwa na maelekezo mahsusi kwamba zinakwenda kufanya shughuli gani; na za makusanyo ya ndani maamuzi ya matumizi yake ni lazima yafanywe na baraza lote la madiwani.

“Hapa Manispaa mnapokea fedha, zinakaa kwenye akaunti kwa muda halafu zinapotea. Hazijulikani zimefanya nini. Nitaleta timu, waje wafuatilie hapa Kigoma, waende hadi Tamisemi ili tuone huo mnyororo unaenda wapi,”

Katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake, Waziri Mkuu alitoa mfano kuwa Manispaa ya Kigoma ilipokea Sh500 milioni kutoka Ofisi ya Rais-Tamisemi zikakaa kwenye akaunti kwa muda mrefu, lakini baadaye zikatoweka na hazijulikani zilitumika kufanya nini.

“Kuna kiasi kingine cha Sh447 milioni kilitumwa Kigoma, wakati zinaandaliwa kutoka, mkurugenzi akazuia. Hongera mkurugenzi na uendelee kuzizuia. Sisi tunamfuatilia mkurugenzi aliyekuwapo kwa sababu anajua zile Sh500 milioni zilitokaje,” alisema.

Wilaya ya Kigoma

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, alisema wanakabiliwa na matatizo mengi, yakiwamo matumizi mabaya ya fedha, makusanyo kidogo kwa sababu ya malumbano, mawakala kukaa na fedha mikononi badala ya kuzipeleka benki, baraza la madiwani kukosa taarifa za fedha na kutumia fedha za miradi kulipana posho.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi