Connect with us

Kitaifa

Kizungumkuti cha Toto Afya Kadi pasua kichwa

Dar es Salaam. Licha ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kusisitiza maboresho ya mfumo wa utoaji bima ya afya kwa watoto shuleni, wadau wamezidi kuukosoa wakisema una kasoro na utawakosesha haki mamilioni, hasa wale walio nje ya mfumo wa elimu.

NHIF ilifuta mfumo wa awali wa utoaji bima kwa watoto ambapo mtoto mmoja alikuwa analipiwa Sh50,400 na kuanzisha utaratibu mpya wa kusajili watoto kupitia shule zao, ambapo wadau wanasema haujawafikia wengi na upo uwezekano wa idadi kubwa ya wanafunzi kuikosa haki hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu, watoto walio nje ya mfumo wa elimu, wale wenye umri chini ya hadi minne wako milioni 9.21 na wengine milioni 5.65 wenye umri kati ya miaka mitano hadi 17 hawapo kwenye vigezo na masharti ya bima hiyo maarufu kama Toto Afya Kadi.

Baadhi ya wananchi wamekosoa mfumo huo wakisema unawatenga watoto, hasa wanaotoka shule zenye idadi ndogo ya wanafunzi, familia duni zisizotumia bima na wasio na wazazi.

Maoni hayo yametolewa kupitia mjadala wa X-Space ulioandaliwa na Mwananchi Communications Ltd, ukiwa chini ya mada isemayo Mabadiliko ya huduma Toto Afya Kadi nini sababu, matokeo na suluhisho lake?’

Ugumu wa sharti

Mbali na mjadala huo, uchambuzi uliofanywa na Mwananchi umebaini, sharti la kuandikisha watoto kuanzia 100 katika shule ili wapatiwe bima ya afya, nalo linaelezwa kuwa kikwazo kwa kuwa linafanya zaidi ya wanafunzi 80,000 kukosa kigezo hicho kwa kuwa shule wanazosoma hazijafikisha idadi hiyo ya wanafunzi.

Takwimu za Elimu Msingi zilizotolewa na Ofisi ya Rais – Tamisemi 2023 zinaonyesha jumla ya shule za msingi 842 na sekondari 481 zina wanafunzi chini ya 100.

Kwa mujibu wa NHIF, hadi sasa shule 240 zimekwishasajiliwa na wanafunzi wake watapata kadi hizo, ingawa haijaeleza kama wamesajiliwa watoto wote wa shule hizo au la.

Katika ufafanuzi wake, mfuko huo umesema utaratibu mpya wa Toto Afya Kadi unalenga kuongeza wigo wa wanachama katika mfumo kuelekea bima ya afya kwa wote na kuhakikisha wanachama wanajiunga kama familia, kaya au makundi ya wanafunzi kupitia shule wanazosoma.

Hata hivyo, jambo linalozua maswali ni sharti la kuitaka shule husika kusajili watoto hadi wafike 100 ili wapewe huduma hiyo.

Akichangia mada katika majadala huo, mhariri msaidizi wa habari wa Mwananchi, Ibrahim Yamola alihoji sababu ya kuweka sharti la kuandikisha watoto 100 ndipo wapate huduma.

“Kama kulikuwa na lengo zuri kulikuwa na sharti gani kwa shule kuwa na watoto 100? Kuna watoto wanakosa fursa kwa kuwa hawajafika idadi hiyo.

“Hata kama shule ina watoto 98 hawapati bima, NHIF watueleza nini wanafanya kuondoa hili sharti linawakosesha watoto hawa kupata bima ya afya?”

Maoni hayo yameungwa mkono pia na wachangiaji kwenye taarifa zilizotokana na mjadala huo kwenye mtandao wa Instagram, akiwamo Hamisi Nyirenda Mohamedi aliyehoji:

“Kwa nini iwe lazima kupitia shuleni? Toto Afya Kadi ilikuwa ni kwa ajili ya watoto ambao hawajatimiza miaka 18, kuna watoto hawapo shuleni ama hawajatimiza umri wa kwenda shule au hata wale wa mtaani ambao wakati mwingne tunawasaidia kuwalipia ili wapate matibabu.

“Sasa inapoonekana mtoto lazima apitie shule maana yake ni kwamba tunamnyima fursa mtoto wa mtaani kupata bima ya afya, mimi maoni yangu ni kwamba Toto Afya Kadi irudi kama ilivyokuwa mwanzo.”

Naye Heriel Mark alisema, “shule fulani ilifikisha watoto 68 ikashindwa kujiunga, kisa hawajafika watoto 100, mwisho tukarudisha hela kwa wazazi, kama taasisi tuliumia sana lakini hatukuwa na namna.”

Kwa upande wake, Roland Malaba maarufu Madenge, alisema suala kwamba watoto chini ya miaka mitano wanaoshindwa kuandikishwa kupitia bima ya wazazi au vifurushi vingine watumie fursa ya matibabu bila malipo, ni kuwatenga na mfumo wa bima.

“Tunahitaji watu wengi wenye afya njema ili kusaidia watu wachache wanaougua, lakini ukiondoa umri kuanzia 0 hadi 5 na kuwaunganisha na wazazi kwenye bima si sahihi, alafu ukachukua kuanzia miaka mitano na kuendelea kuwapata shuleni huo ni uongo,” alisema.

Hata hivyo, akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema huduma hiyo haijabadilika, bali imefanyiwa maboresho katika namna ya kusajili watoto.

“Mwaka 2016 hadi 2018 tuliendelea kusajili watoto kwenye afya kadi lakini mwelekezo wake haukuwa mzuri. Tuliona michango ya kundi hili pamoja na matumizi yake si mazuri na kundi kubwa la watoto wanajiunga wakiwa tayari wagonjwa. “Sasa tuliamua kuja na njia ya kuongeza watoto kwa njia mbili, moja, kupitia shule na pili kupitia familia zao.

“Kupitia shule njia tunayotumia ni ushawishi na hatujachukua fomu kwenda kulazimisha watoto kujiunga, bali kupitia vikao halali vya shule, baba au mama akilipia atawasaidia watoto, kwa hiyo suala hili bado ni hiari si lazima,” alisema Konga.

“Hatujasitisha huduma kwa wananchi ila tunahitaji huduma hii iwe endelevu. Lakini pia watoto ambao walikuwa wanatibiwa na Toto Afya Kadi wanaendelea na matibabu kama kawaida mpaka pale watakapofikia ukomo wa muda wa matumizi ya kadi zao,” alisema.

Laibua bima kwa wote

Akichangia mjadala huo kwenye X-Space, Mtaalamu wa afya, Dk Elisha Osati alisema suluhisho la suala Toto Afya Kadi ni kupitisha Bima ya Afya kwa Wote.

“Suala la bima ya afya kwa wote lilienda bungeni likatolewa na hatujaambiwa sababu, bajeti ya Wizara ya Afya ilipita haikulizungumzia chochote, nafikiri NHIF inajua sababu za ndani kwa kuwa Serikali ilitakiwa kuweka hela ili huduma iweze kuanza,” alisema.

Kuhusu Toto Afya Kadi, Dk Osati alisema watoto wametolewa kwenye matibabu na hakuna mkakati wa kuwaingiza ili wapate huduma hiyo haraka.

“Hatujaona hizo juhudi za mfuko na wizara wakihamasisha, hatujaona NHIF ikizungumza na Tamisemi (Ofisi ya Rais) na idara nyingine kuhamasisha wazazi watoto wajiunge na mfuko,” alisema.

Alisema bado Serikali haijatoa majibu sahihi kuhusu upatikanaji wa bima kwa watoto.

“Mimi ni mwenyekiti wa moja ya bodi za shule, sijawahi kuwaona NHIF wakija kusisitiza watu kujiunga na bima na gharama zinazotakiwa,” alisema.
Akijibu hoja, Konga alisema huo ni mchakato unaoendelea.

“Hatujakwamia njiani na tupo makini kama nchi, tunataka tukianza tumeanza ili tuwe mfano kwa mataifa mengine,” alisema.

Kwa upande wake mtaalamu wa famasia, Tumaini Makole alizungumzia umuhimu wa utoaji elimu kuhusu suala hilo ili uelewa uongezeke.

“NHIF watoke ofisini na kuwafuata wananchi kuwahamasisha kujiunga na bima, kwa hiyo tunataka wafuatwe mitaani.
“Pia kuwe na usimamizi mzuri wa mfuko uimarishwe, kile kilichopo kwenye mfuko kitumike vizuri, magonjwa yanayowasumbua watoto yanazuilika na huduma zisitolewe kwa vifurushi,” alisema.

Akifafanua suala la elimu, Konga alisema hawatoi elimu kwa watoto bali kwa wazazi na elimu hiyo haitolewi hospitalini, bali kwenye nyumba za ibada na maeneo mengineyo.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Taasisi za Afya Binafsi Tanzania (APHFTA), Dk Egina Makwabe aliwataka Watanzania kubadilisha mitazamo kuhusu kugharimia huduma za elimu, afya na maji.

“Zamani ilikuwa bure, kwa sasa maisha yamebadilika. Hivi vitu kwa sasa lazima vichangiwe, lazima tuwe tayari kuchangia. Mfumo wa kwenda shuleni nadhani ndiyo njia sahihi ya kupata wachangiaji wengi,” alisema.

Alipendekeza pia NHIF kupeleka maombi serikalini ili kwa umri chini ya miaka 15 iweke kiasi cha fedha angalau Sh200 bilioni mpaka 300 bilioni ili kusaidia watoto hao.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi