Kitaifa
Maumivu mgawo wa umeme yazidi kutikisa
Dar/mikoani. Ni maumivu. Hivi ndivyo unavyoweza kutafsiri vilio cha wafanyabiashara na wananchi baada kukwama kufanya shughuli mbalimbali, huku wengine wakilia na hasara baada ya kuanza kwa mgawo wa umeme unaotokana na uhaba wa nishati hiyo.
Miongoni mwa walioguswa na mgawo huo ni watengenezaji wa keki, wasindikaji wadogo wa nafaka za lishe, wafanyabishara wa samaki wabichi, mafundi vyuma na wauzaji wa vinywaji baridi, ambao wameeleza shughuli zao kukwama na hivyo kupata hasara.
“Mimi ni mtengenezaji wa keki za sherehe, niliona ratiba ya mgawo wa umeme, niliandaa keki zangu usiku zenye thamani ya Sh130,000, niliamka mapema na kuanza kuzipika, wakati zinakaribia kuiva umeme ukakatika, zote zimeharibika, sina la kufanya,” alisema Chamika Hezron, mkazi wa Chanika, Dar es Salaam, miongoni mwa wengi walioathiriwa na mgawo huo.
Wakati maumivu hayo yakiendelea, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Uwekezaji Tanesco, Declan Mhaiki, ameeleza sababu ya kukatika kwa umeme kwa baadhi ya maeneo nchini kuwa ni upungufu wa maji na kuongezeka kwa mahitaji ya nishati hiyo.
“Sasa ni kiangazi, mtiririko wa maji umepungua, kwa hiyo uwezo wa uzalishaji kwa njia ya maji umepungua, wakati huohuo mahitaji yameongezeka kwa miaka mitatu ya hivi karibuni kutokana na ukuaji wa uchumi,” alisema.
Hata hivyo, Mhaiki alisema kwa sasa gesi asilia inachangia asilimia 65 ya umeme unaozalishwa na Tanesco, huku maji yakichangia asilimia 35 pekee.
Jana, gazeti hili lilifanya mahojiano na wananchi na wafanyabiashara kwenye baadhi ya mikoa yenye mgawo wa umeme na kueleza makali wanayopitia kufuatia kukosekana kwa nishati hiyo.
Daudi Salehe, mfanyabiashara wa samaki wabichi mkoani Tanga alisema tayari amepata hasara ya Sh700,000 baada ya samaki aliowahifadhi kwenye jokofu kuoza kwa kukosa umeme.
“Sijui nitafanyaje, maana mtaji wa samaki hawa ambao huwa nawauza kwa oda kwa makandarasi wa barabara raia wa China umeharibika,” alisema.
Naye, Jacob Semindu, mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro alisema changamoto ya kukatika umeme imewaathiri yeye na wenzake ambao wamejiajiri kupitia uchuuzi wa samaki.
Si hao tu, Jane Haule, msindikaji wa unga lishe wa nafaka za mazao mchanganyiko mkoani Mbeya alilalamika kupoteza wateja wake kutokana na mgawo, huku mahitaji ya bidhaa hiyo yakiwa makubwa.
“Huu mgawo unatuathiri, ni vyema sasa ukawekwa utaratibu wa kutoa taarifa za mgawo wa umeme siku moja kabla ili kuwezesha kufanya maandalizi mapema ambayo yatasaidia kuepuka hasara zinazoweza kuepukika,” alisema.
Kwa upande wake, Emmanuel Asseno, fundi uchomeleaji vyuma wilayani Moshi mkoani Kilimajaro alisema kwa sasa shughuli zake zimesimama.
Kilio chake ni kukatika kwa umeme siku nzima, akidai hana taarifa juu ya mgawo unaoendelea, akisema kipato chake kimekwenda mrama.
Kwa wafanyabiashara wa vinywaji baridi, nako si shwari. Rashid Hashim wa soko la Chuno mkoani Mtwara, alisema kukatika kwa umeme mara kwa mara kumesababisha wateja kupata vinywaji wasivyohitaji na wengine kuachana navyo.
Kilio hicho si tofauti na cha Ibrahim Mbolembole, mkazi wa Somanga mkoani Lindi aliyesema, “kwa wiki mbili ndiyo imekuwa shida zaidi, unakatika saa 4 (asubuhi) unarudi saa 10 jioni, napo haukai sana unakata tena.”
Naye Hassan Mohamed, anayepaka rangi za kucha alisema kipato chake kimeshuka kutokana na kukosa wateja, ingawa hakuwa tayari kusema mapato yake yameshuka kwa kiasi gani.
“Mfano jana nimeshindwa kuwahudumia wateja watatu, kila mmoja alikuwa anahitaji huduma ya Sh30,000 kwa sababu hapakuwa na umeme, huwezi kumpaka rangi ya jeli inayokaushwa kwa kifaa cha umeme,” alisema.
Kilio kikuu ni kwa fundi kinyozi Mohamed Hamduni, mkazi wa Kata ya Nyegezi jijini Mwanza, aliyesema changamoto hiyo inafanya hali ya maisha kwa vijana waliojiajiri kama yeye kuwa ngumu kwa kuwa wengi wanategemea umeme kuzalisha.
“Jumapili nimekula hasara, umeme ulikatika tangu asubuhi umerudi usiku, wanafunzi walikuwa wanafungua shule Jumatatu, kwa hiyo pesa zote za wanafunzi waliotaka kunyoa zimenipita kwa sababu ya umeme,” alisema.
Waziri wa Nishati atoa neno
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alisema amewaelekeza viongozi wa Tanesco kutohudhuria kongamano la kimataifa jana, bali wafuatilie changamoto za kupunguza maumivu ya upatikanaji wa umeme nchini.
“Rais, makamu wa rais na wewe (Waziri Mkuu) mmenielekeza kwa muda mrefu toka nimeteuliwa kwamba, tufanye kila tunaloweza kuhakikisha maumivu ya upungufu wa umeme tunayamaliza.
“Tunafahamu ya kwamba ukuaji uchumi ni mkubwa kwa watu wetu, lakini vyanzo vyetu vya umeme bado ni vilevile, lazima tuongeze vyanzo vipya ili kuwa na uhakika kwa ajili ya shughuli zetu za kiuchumi…ndiyo maana utaona katika mkutano huu baadhi ya watu wetu wa wizarani, tumewaambiwa hapa msije kwa sababu sisi tunataka umeme,” alisema Biteko, kwenye kongamano la nishati mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Nini kimetokea?
Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Martin Mwambene alisema kutokana na maji kupungua katika mabwawa, inawalazimu kufanya uzalishaji wa umeme kwa awamu, hususan nyakati za mchana na usiku hupunguza kiwango ili kuruhusu uhimilivu wa maji.
Alisema “ili gridi ya taifa isitoke unapaswa kuendana na matumizi ya siku husika, usipofanya hivyo unaweza kusababisha gridi kutoka na ikitoka kuirejesha utatumia saa kadhaa na hii ndiyo sababu tunatoa umeme kwa ratiba kwa baadhi ya maeneo.”
Mwambene, ambaye hakutaka kueleza kiwango cha upungufu, alisema mabwawa matatu ya Mtera, Kidatu na Kihansi uzalishaji wake umepungua.
“Mtera inazalisha megawati kama 70, Kidatu megawati kama 200 na Kihansi kwenye megawati 180. Maji ya Kidatu yanaanzia Mtera na Mtera mara ya mwisho kufurika ni 2021 na tangu wakati huo maji yanapungua.”
Mei 31, mwaka huu akizungumza katika Bunge la Bajeti, aliyekuwa Waziri wa Nishati, January Makamba aliliambia Bunge kuwa mahitaji ya nishati ya umeme yameongezeka mara nane katika mwaka uliomalizika Juni 30.
“Tuna upungufu wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme, baadhi ni chakavu, mingine imezidiwa na matumizi ikatumika tofauti na ilivyokusudiwa,” alisema Makamba.
Alisema mipango ya wizara hiyo ni kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati 1,872 mwaka 2023 hadi 5,810 mwaka 2025/26 ili kukidhi mahitaji hayo.
Pia alisema wanapanga kuongeza idadi ya njia za kusafirisha umeme, kutoka kilomita 6,110.28 kwa sasa hadi kilomita 10,670.65 mwaka 2025/26.
Suluhisho nishati jadidifu
Wakati hali ikiwa hivyo, Serikali imesema imeanza kuwekeza nguvu katika uwekezaji wa nishati jadidifu, ikiwa ni msukumo wa kidunia katika udhibiti wa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, hadi kufikia jana, ilikuwepo miradi saba ya umeme jua na upepo ya megawati 750 hadi 1,000 inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuongeza mchango wake katika gridi ya Taifa kutoka wa asilimia 0.5 ya sasa hadi kufikia asilimia 20 ifikapo mwaka 2025.
Baadhi ya miradi inayoendelea ni pamoja na wa megawati 100 wa upepo (Makambako), megawati 100 wa upepo (Ismani), megawati 60 za umemejua (Dodoma) na megawati 100 za umemejua (Manyoni).
Katika mwelekeo huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekaribisha kampuni za kimataifa kuwekeza katika sekta hiyo ya nishati hapa nchini, alipozungumza katika kongamano la Nishati jijini Dar es Salaam.
“Kongamano hili linatafuta ufumbuzi kwa kushirikisha wataalamu. Tunayo miradi ya kimkakati saba inayozalisha umeme, tumepanua sana wigo katika umeme wa gesi, lakini bado tunataka kupanua wigo zaidi kwenye umemejua, upepo na hii ndiyo fursa ya kuelekea huko. “Taasisi za kifedha ziko hapa kwa ajili ya kuwahakikishia wawekezaji wa ndani katika eneo la mahitaji ya kifedha,” alisema Majaliwa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, Serikali inahitaji angalau asilimia 78 ya ushiriki wa kampuni binafsi katika uwekezaji wa miradi ya nishati jadidifu yenye thamani ya Sh89 trilioni, huku ikiwakaribisha katika fursa za uwekezaji wa jumla ya megawati 490 ambazo ni upepo (megawati 150), umemejua (megawati 205) na joto ardhi (megawati 135).