Connect with us

Kitaifa

Bandari ya Uvuvi Kilwa kuibua fursa chekwa kusini

Dar es Salaam. Mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko umetajwa kuwa utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya uvuvi nchini, kwa kuwa utaongeza mazao ya samaki yatakayochochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Imeelezwa kuwa bandari hiyo ya kwanza ya uvuvi Tanzania, mbali na kuwa kichocheo cha uchumi, itaongeza ajira na upatikanaji wa samaki wa kuboresha lishe.

Jana, Rais Samia Suluhu Hassan aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, sambamba na kugawa vifaa mbalimbali vya uvuvi, zikiwemo boti 160 kwa wavuvi na wakulima wa mwani.

Hafla hiyo ilifanyika wilayani Kilwa ambako Rais Samia anaendelea na ziara yake akitokea Mtwara alikofanya shughuli mbalimbali, ikiwemo kufungua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

Ili kupanua fursa hizo, tayari Serikali imebainisha azma yake ya kujenga bandari ya pili ya uvuvi Bagamoyo mkoani Pwani, itakayowahudumia wavuvi wa ukanda wa Pwani na meli za kimataifa za uvuvi zitakazotia nanga nchini.

Bandari Kilwa

Ujenzi wa Bandari ya Kilwa Masoko, mahsusi kwa ajili ya uvuvi, utajumuisha jengo la utawala, eneo la maandalizi ya samaki kwa ajili ya kuwauza ndani na nje ya nchi, kituo cha umeme wa kuhudumia uendeshaji wa bandari na kituo cha maji safi kwa ajili ya kuhudumia bandari.

Pia, itakuwa na kituo cha kuzuia majanga ya moto, kituo cha kuzalisha naitrojeni ya kusafisha maji, eneo la matunzo na matengenezo ya nyavu za uvuvi, matanki ya kuhifadhia mafuta, gati na karakana ya matengenezo ya meli.

Akizungumzia mradi huo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema sambamba na bandari hiyo, wizara yake inatekeleza mradi wa kukopesha boti za uvuvi na vifaa vingine vya shughuli hiyo kwa masharti nafuu ya riba.

“Jumla ya boti 160 zilizogharimu Sh11.5 bilioni, zitatolewa kwa wavuvi na wakulima wa mwani katika Bahari ya Hindi na maziwa makuu, vyama vya ushirika vya wavuvi, vikundi na kampuni za uvuvi,” alisema.

Ulega alisema bandari ya uvuvi inakwenda kuongeza ukuaji wa uchumi na wanakusudia sekta ya uvuvi ichangie kwenye pato la Taifa kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2026.

Waziri huyo alisema hiyo itawezekana kwa kuwavuta wawekezaji kufunga gati katika eneo la Kilwa Masoko.

Alisema gharama ya jumla ya Sh280 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo, ni jambo linaloonyesha dhamira ya Serikali kwenda kuinua sekta ya uvuvi nchini na kuhakikisha inakuwa na mchango kwa maendeleo ya Taifa.

“Meli 10 zenye urefu wa mita 30 zitakuja kuweka nanga hapa, mitumbwi 200 itaweza kupaki hapa na vijana takribani 30,000 wataajiriwa katika bandari hiyo na wengi wao watatoka mikoa ya Lindi na Mtwara,” alisema Ulega.

Waziri huyo alisema bandari hiyo itakuwa na soko litakalotumika na wavuvi wote wa ukanda wa kusini.

Pia, alisema bandari hiyo itakuwa na eneo la kuchakatia samaki na baada ya kukamilika kwake, itaendeshwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Akizungumzia hatua ya Serikali kutoa vifaa hivyo, mkulima wa mwani, Shukrani Shamte aliishukuru kwa kuwapatia mkopo wa boti wenye gharama nafuu, huku akisema boti hizo zitawasaidia kwenye kilimo cha mwani, hasa kwenye kina cha maji mengi na pia kubebea zao hilo kwenda pwani.

“Tunakuomba utuletee vifaa vingine, wakulima ni wengi, boti tulizoletewa ni chache, mahitaji ni makubwa,” alisema Shukrani wakati akizungumza na Rais Samia kwenye hafla hiyo.

Rais Samia alisema Bandari ya Kilwa itafungua fursa mbalimbali, siyo sekta ya uvuvi pekee, bali pia kwa wananchi wote walio katika mnyororo wa thamani.

Wakati Rais Samia akisema bandari hiyo itazalisha ajira zaidi ya 20,000, Waziri Ulega alitaja ajira zitakazozalishwa ni 30,000.
Rais alitoa wito kwa wananchi wa Kilwa kutumia fursa zitakazojitokeza kwenye miradi hiyo kupata ajira na kukuza vipato vyao.

Uvuvi wa baruti

Rais Samia alitoa onyo kwa wakazi wa Kilwa wanaotumia baruti kwenye shughuli zao za uvuvi, akisema kufanya hivyo kunasababisha samaki kuyakimbia maeneo yao kwa kuwa matumbawe yanakuwa yameharibiwa, hivyo wanakimbilia katikati ya bahari.

“Matumizi ya baruti ndiyo yamewafanya sasa mfuate samaki maeneo ya mbali kwa sababu mmebomoa matumbawe yote, wanakimbilia bahari kubwa. Sasa kama na kule mnaenda kulipua baruti, mjue mnajilipua wenyewe.

“Niwaombe sana wanaosimamia sekta ya uvuvi hapa Kilwa, simamieni hilo, zuieni wavuvi kutumia baruti kwenye maeneo hayo,” alisema Rais wakati wa mkutano huo na wananchi wa Kilwa Masoko.

Uvuvi Bagamoyo

Wakati huohuo, akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi, Rais Samia alisema kutokana na ukubwa wa ukanda wa pwani, Serikali inafikiria kujenga bandari nyingine ya uvuvi ili kukidhi mahitaji ya wavuvi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, nchi yenye bahari na maziwa makuu.

“Bandari hii nilivyoiona na maboti yanayoletwa, inaweza ikatosha kwa upande huu, lakini tunafikiria kupokea meli nyingi sana za kimataifa katika nchi yetu ya Tanzania kwa sababu ukanda wetu wa bahari kuu ni mkubwa sana.

“Kwa hiyo tunafikiria kujenga bandari nyingine ya uvuvi pale Bagamoyo, hali ya uchumi ikituruhusu tunaweza kufikiria kufanya hivyo pia,” alisema Rais Samia, wakati akizungumza na wananchi wa Kilwa Masoko.

Fidia bado

Wakati manufaa ya bandari hiyo yakielezwa, Mbunge wa Kilwa Kusini (CCM), Ally Kassinge alisema wananchi 438 ambao ardhi yao ilichukuliwa kwa ajili ya bandari hawajalipwa fidia zao, licha ya uthamini wa mwaka 2011 na wa tatu uliofanyika mwaka 2022.

“Wananchi 438 wamenituma nikuombe Mheshimiwa Rais, walipwe fidia zao ili waweze kujikimu na kupisha maeneo hayo ili wakatafute maeneo mengine,” alisema mbunge huyo wakati wa hafla hiyo.

Hata hivyo, Rais Samia alijibu hoja hiyo akieleza kushangazwa na suala la fidia, akihoji viongozi wa Kilwa walikuwa wapi kufuatilia jambo hilo ambalo sasa limefikisha miaka 20 bila wananchi kulipwa stahiki zao.

“Hawa wananchi si walikuwa na wawakilishi? Kwa nini madai haya yamekaa muda wote huo bila kushughulikiwa? Leo mnataka Rais aje kushughulikia mambo ya miaka 20 nyuma, inashangaza kidogo,” alisema Rais Samia.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi