Connect with us

Kitaifa

Alama za vidole kudhibiti wimbi la watumiaji ARV

Mbeya. Matumizi ya mfumo wa teknolojia ya usajili alama za vidole kwa watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU), umeelezwa utarahisisha upatikanaji taarifa sahihi na kupunguza udanganyifu wa kujisajili kituo zaidi ya kimoja kwa lengo la kupata dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo (ARV).

Hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni kuboresha utoaji huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi ambao awali walikuwa na changamoto ya kukosa huduma pindi wanapokuwa nje ya vituo husika, na kuwalazimu kufungua kadi upya na kuandika majina ya udanganyifu kwa lengo la kupima na kuanza kutumia ARV.

Mfumo huo umeanzishwa rasmi nchini na Serikali ikishirikiana na Marekani kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani (PEPFAR), wenye nia ya kuwasaidia waathirika wa ugonjwa huo kupata dawa wakiwa nje ya vituo husika vya kutolea huduma.

Grace Mwinamila, anayetumia ARV alisema mfumo huo utaisaidia Serikali kupata takwimu za kweli, kwani kitendo cha wagonjwa kuhama zaidi ya kituo kimoja ni changamoto kubwa katika sekta ya afya.

“Tunaishukuru Serikali ya Marekani kwa kuendeleza mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kuboresha huduma za kupata dawa maeneo mbalimbali nchini na utasaidia wagonjwa kutoacha matumizi ya dawa,” alisema Grace.

Mfumo huo umeonyesha kuleta matokeo makubwa ambayo yatarejesha matumaini kwa waathirika kutoacha matumizi ya dawa na badala yake kuona ni njia rahisi ya kuwepo kwa taarifa katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu faida ya mfumo wa usajili alama za vidole, Mratibu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Iringa, Emmanuel Petro alisema utasaidia kuondokana na tabia ya udanganyifu kwa baadhi ya watu wanaotumia ARV.

“Wapo wagonjwa anajisajili kwenye vituo viwili tofauti na sababu huenda akawa nje ya kituo dawa zikamuishia, sasa kuanza kwa mfumo huo anapofika Mkoa mwingine akifika kujiorodhesha upya taarifa zake zitasoma kwenye mfumo na mtoa huduma atagundua amesajiliwa wapi na aina ya dawa anazotumia.

“Mfumo huo utakuwa rafiki na hata kusaidia Serikali kupata takwimu sahihi za wagonjwa, tofauti na sasa unakuta mgonjwa mmoja kafungua kadi maeneo mawili mpaka matatu tofauti, mkifanya tathmini mnaona ni mteja mpya kumbe katoka mkoa au mahali pengine,” alisema Emmanuel.

Hali ya maambukizi

Emmanuel amesema kwa takwimu za kipindi cha 2016/17 kitaifa hali ya maambukizi ilikuwa asilimia 4.7, huku Mkoa wa Mbeya ukiwa na asilimia 9.2 na Songwe asilimia 5.8, huku kundi kubwa la mabinti balehe wakiwa wanatumia dawa.

Asema kundi kubwa la mabinti na vijana balehe walio na umri kati ya miaka 15-24 ni asilimia 40 ya maambukizi, hali ambayo imesababisha Serikali kwa kushirikiana na wadau kuja na mipango mikakati, ikiwamo miradi mbalimbali ya Dreams na Tumaini inayosimamiwa na HJFMRI kwa ufadhili wa PEPFAR.

“Wadau hao wamekuwa na mchango mkubwa kwa Serikali ya Tanzania katika kupunguza afua za maambukizi ya Ukimwi na VVU, ikiwamo kuanzishwa kwa klabu, ujasiriamali kwa vijana wanaoishi na maambukizi katika maeneo ya mipakani, hususan mji wa Tunduma,” alisema.

Amesema jitihada hizo zinasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza hali ya maambukizi kwa mabinti, kwani wengi wamejitambua hali zao na kuzingatia elimu ya matumizi ya ARV.

Emmanuel alisema kupitia programu mbalimbali za uelimishaji rika na mfumo wa kuwasajili kwa alama za vidole, utasaidia kupunguza maambukizi, kwani wagonjwa watakuwa huru kuishi maeneo mbalimbali kwa kupatiwa huduma ya dawa na sio mpaka kusafiri kwenye kituo ambacho alifungulia kadi.

“Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali ya Marekani kwa kuendelea kuwekeza nchini kwenye mapambano ya VVU kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-24, kundi ambalo limeathirika kwa kiasi kikubwa na maambukizi.

Mikakati ya Tacaids

Mikakati ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), ni kuendeleza kampeni ya mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU kwa kundi la vijana, hususan maeneo ya mipakani, lengo ni kuona zinatafutwa asilimia 95 tatu za kupunguza maambukizi mapya.

“Tunatoa elimu ya matumizi ya dawa za ARV, mipira ya kiume (kondomu) wakati wa kujamiiana, jambo ambalo limekuwa na mapokeo mazuri sambamba na kuona vijana wanajikita katika shughuli za kiuchumi kupitia mradi wa Dreams.

Mikakati ya Serikali

Katika kuhakikisha huduma za dawa zinakuwa rafiki, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Marekani kupitia ufadhili wa PEPFAR, imekuja na mipango mikakati ya kutoa vifaa vya usajili wa alama za vidole kwa wagonjwa wanaotumia ARV ambao unatekelezwa na Taasisi ya Walter Reed Army Institute of Research (WRAIR), kupitia HJFMRI.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mkazi wa WRAIR kutoka ubalozi wa Marekani nchini, Mark Breda alikabidhi vifaa vya usajili wa alama za vidole katika Hospitali ya Rufaa Mkoa ambavyo vitasambazwa katika vituo vya afya 392 mikoa ya Songwe, Rukwa, Katavi na Mbeya.

Breda alisema kuwa vitasaidia upatikanaji wa taarifa za wagonjwa kwa watoa huduma kwenye vituo vya afya ambavyo vimeelekezwa, hususan kujua kituo ambacho mlengwa amefungulia kadi ya kuchukua dawa.

Amesema awali wagonjwa wengi walikuwa wakipata changamoto ya kupata huduma wanapokuwa kwenye mikoa mingine kwa kile kilichoelezwa kukosekana kwa taarifa zao na aina ya dawa wanazotumia.

“Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuchangia afua za watu wanaoishi na maambukizi na uwepo wa mfumo huu utasaidia upatikanaji wa taarifa za wagonjwa na dawa kwa njia rahisi tofauti na sasa,” alisema.

Akizungumzia faida za uwepo wa mfumo huo, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Elizabeth Nyemi alisema utasaidia watoa huduma maeneo mbalimbali nchini kubaini taarifa za wagonjwa ambao watafanya udanganyifu.

“Sasa tunakwenda kuboresha huduma za upatikanaji wa taarifa sahihi za wagonjwa wanaotumia ARV kupitia mfumo wa usajili wa alama za vidole ambazo zinasaidia kujua mgonjwa katika mkoa gani na anatumia aina gani ya dawa.

“Pia itaongeza umakini kwa watumiaji dawa, kwani hawataacha kutokana na kuishiwa wakiwa mbali na vituo wanavyozichukulia, kwani popote walipo kutakuwa na taarifa zao na watahudumiwa,” alisema.

Dk Elizabeth alisema kumekuwepo na changamoto kwa baadhi ya wagonjwa kuhama vituo, wakiwamo wasichana wenye umri kati ya miaka 15 -24, jambo ambalo limewalazimu kama hospitali kwa kushirikiana na wadau kuwaundia klabu za kuwakutanisha. “Tumeona njia pekee ya kuwapatia elimu ya matumizi sahihi ya dawa ni kuwakutanisha pamoja mara kwa mara, hali ambayo imesaidia kwa kiwango kikubwa kuwarejesha kwenye matumizi sahihi ya dawa,” alisema, huku akiweka bayana tayari vifaa 60 vya alama za vidole vimeshasambazwa kwenye vituo vya afya.

Mkurugenzi wa Shirika la Walter Reed Tanzania, Dk Magnus Ndolichimba alisema wataendelea kuboresha huduma kwa watu wanaotumia ARV, hususan kwa mabinti balehe.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi