Kitaifa
Mradi Bwawa la Nyerere kuongeza uzalishaji umeme
Rufiji. Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) umekamilika kwa asilimia 91.72, huku ukitarajiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme nchini pale utakapokamilika na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mradi huo wenye thamani ya Sh6.6 trilioni, unatarajiwa kuzalisha megawati 2115 za umeme, ambao utasaidia kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme nchini ambalo linatokana na upungufu wa maji kwenye mabwawa yanayotumika kuzalisha umeme.
Desemba 22, 2023 Rais Samia alishiriki hatua ya kufunga njia ya uchepusha maji na kuanza ujazaji wa maji kwenye bwawa la kuzalisha umeme.
Jana, Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko alitembelea mradi huo kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Agosti 30, 2023 kuongoza wizara hiyo.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kutembelea mradi huo, Dk Biteko alimpongeza mkandarasi kwa kasi yake ya kutekeleza mradi huo wa kimkakati pamoja na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kwa usimamizi wake wa mradi huo.
“Nimefurahi kwamba mradi umefikia asilimia 91.72 na mkandarasi analipwa kila anapotoa certificate (hati ya malipo) yake. Kwa hiyo katika malipo yote anayodai, ameshalipwa asilimia 85.5 ya fedha zote ambazo ameziandikia certificate,” alisema Dk Biteko.
Alisema changamoto ya umeme inayotokana na vyanzo vya maji kupungua, inatarajiwa kumalizwa kutokana na kuwepo kwa mradi huo na kwamba muda siyo mrefu wananchi wataanza kupata umeme wa uhakika.
“Tuko kwenye hatua za mwisho kuweza kupata umeme wa maana ili tusaidie Watanzania kupata umeme na kuwasaidia kukuza uchumi wao,” alisema Biteko.
Awali akitoa maelezo kwa Dk Biteko, mhandisi mshauri wa mradi huo, Emmanuel Mwandambo alisema kwa sasa bwawa limefikia ujazo wa mita 164.81 ambayo ni sawa na lita za ujazo bilioni 14.66, sawa na asilimia 47.8 ya ujazo wote.
Mhandisi huyo alibainisha kwamba majaribio ya uzalishaji katika mradi huo yatafanyika Februari 2024 wakati uzalishaji kamili ukitarajiwa kuanza Juni 2024.
“Mradi unaendelea vizuri na bwawa limefikia ujazo wa mita 164.81 na hapa tumefungulia maji ili yaendelee kusupport (kusaidia) ikolojia ya viumbe katika hifadhi hii,” alisema mtaalamu huyo wakati akielezea mradi.