Connect with us

Kitaifa

Siri madai vigogo kuhongwa na kampuni Acacia zavuja

Dar es Salaam. Unaweza kusema ni fumbo au kitendawili baada ya kuvuja kwa barua pepe (Mwananchi halijazithibitisha) na kuchapishwa kwa habari inayoelezea tuhuma za rushwa kwa kikosi kazi cha Tanzania kilichokuwa kikihudumu maeneo ya migodi iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia.

Acacia ndiyo kampuni iliyokuwa ikimiliki migodi mitatu mikubwa ya dhahabu (Bulyankulu, Buzwagi na North Mara) kabla ya kununuliwa na kampuni Barrick, hatua iliyosukumwa na uwepo wa mgogoro wa muda mrefu kati yake na Serikali ya Tanzania.

Kikosi kazi (NTF) kinachozungumzwa ni kile ambacho huundwa na Rais mara nyingi kikijumuisha maafisa wa Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa, kazi zake zikijumuisha kupambana na uhalifu mkubwa kama vile ugaidi na ufisadi na mkuu wake huripoti moja kwa moja kwa Rais wa nchi.

NTF kazi yake ni kulinda miundombinu nyeti ya Serikali na ile ya sekta binafsi nchini na katika sakata hili inaelezwa kuwa kilihusika na kutoa huduma kwa Acacia, ambapo kulingana na mahitaji ya kampuni hiyo, NFT ilikuwa na vitengo vitano, kila kimoja kikiwa na maofisa watatu mpaka saba.

Barua pepe zilizovuja na habari iliyochapishwa katika mtandao wa habari wa The Globe and Mail zinaeleza kuwa kuanzia mwaka 2008 hadi 2015 kampuni ya Acacia ilikuwa ikitumia hadi Dola za Kimarekani 1.2 milioni (Sh3bilioni) kwa mwaka kwa ajili ya kulipa na kuhudumia NTF.

Barua pepe hizo zinaibuka wakati ambao kuna kesi inaendelea katika Mahakama Kuu ya Haki ya nchini Uingereza ambapo Watanzania 10 wanalishtaki soko la dhahabu kwa kutoa ithibati kwa dhahabu zinazouzwa na Barrick Gold, ambayo sasa imechukua umiliki wa Acacia, kwa madai kuwa dhahabu hizo zinapatikana kwenye mazingira yaliyojaa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kulingana na baruapepe hizo ambazo mtiririko wake sio wa moja kwa moja fedha zinazotajwa zilikuwa zikilipwa kwa maofisa hao wa Serikali kwa ajili ya kujikimu, kulipia malazi, chakula na mafuta ya gari.
Kiwango hicho kinaelezwa kilianza kuwa kikubwa kuliko kilichokubaliwa na Serikali kuanzia mwaka 2008.

Kulingana na barua pepe hizo ambazo Mwananchi limeona nakala yake inaonekana Acacia ilikuwa na wasiwasi juu ya jinsi ya kusitisha malipo hayo bila kuharibu uhusiano wake na kikosi kazi hicho cha Serikali lakini wengine walidai kuwa yanakiuka sera za kampuni zilizowekwa kupambana na rushwa na ufisadi.

Nick Rowell, moja ya viongozi waandamizi wa kampuni hiyo, kwenye barua pepe hizo aliwaambia wenzake kuwa malipo hayo kwa maofisa wa NTF yaliifanya Acacia “kutokuendana na sera yake juu ya kuzuia rushwa.” Kwenye barua pepe yake ya awali, Rowell alitaka malipo hayo “yasitishwe mara moja.”

Kiongozi mwingine mwandamizi wa kampuni hiyo, Peter Geleta, alieleza kwamba baadhi yao wamekuwa wakilalamikia kuhusu malipo hayo kwa miezi 18, akisema, “Na ni wazi kwangu kwamba baadhi ya watu wetu wenyewe wamekuwa wakiulinda utaratibu huu.”

Hata hivyo, kulikuwa na hofu kwa baadhi ya viongozi wa kampuni hiyo juu ya namna malipo hayo yanavyoweza kusitishwa, huku wengine wakigusia ukubwa na nguvu ambazo kikosi kazi hicho kinazo, kikiwa na mafungamano na vigogo kwenye nafasi nyeti serikalini.

Mshauri wa masuala ya ulinzi wa Acacia, A.D Firth, alisema kuwa kikosi kazi hicho kilikuwa kikilinda maslahi ya kampuni kwa muda mrefu na hivyo, mabadiliko yoyote kati ya Acacia na kikosi kazi hicho yanapaswa kufanywa kwa umakini mkubwa, sio tu kwa sababu za kisiasa bali pia kiutendaji.
“Mabadiliko yoyote ya kimahusiano (kati ya Acacia na kikosi kazi) ni lazima yafanyike kwa umakini mkubwa siyo tu kwa sababu za kisiasa bali pia kiutendaji.”

Barua pepe hizo zinaonyesha kuwa malipo kwa kikosi kazi hicho yalikuwa yakiongezeka kwa kiasi kikubwa na hayakuwa yakijumuishwa kwenye bajeti ya ulinzi ya Acacia. Hii inaashiria kuwa malipo hayo yalikuwa yakiendelea bila udhibiti.

Mwananchi lilipomtafuta Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Eliezer Feleshi kuzungumzia suala hilo hakupatikana kwa njia ya simu na alipotafutwa Wakili Mkuu wa Serikali Dk Boniphace Luhende kwa ajili ya ufafanuzi alijibu kwa ufupi kuwa jambo hilo haliwahusu.

Hata hivyo miongoni mwa viongozi wa zamani wa Acacia kampuni hiyo Asa Mwaipopo alipotafutwa ili kuzungumzia sakata hilo alisema haitakuwa sawa yeye kuzungumzia jambo hilo bila idhini ya waajiri wake wa zamani.

“Hili ni suala la kikampuni na kwakuwa anwani yao bado ipo ni vyema wakatafutwa wao kwakuwa mimi sina cheo chochote katika ofisi hiyo tena hivyo sio sawa mimi kuzungumza chochote,” alisema Mwaipopo ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Acacia Tanzania.

Mwaipopo alikiri kuona taarifa na maoni ya watu kuhusu sakata hilo lakini alisema yeye kutoa maoni yoyote kwa kitu kinachoendelea mahakamani ni kuingilia utendaji wa chombo hicho cha utoaji haki.
Awali gazeti dada la The Citizen lilimtafuta Mkurugenzi mwingine wa zamani wa Acacia, Deo Mwanyika alisema hayupo katika nafasi nzuri ya kuzungumza na kushauri atafutwe Mwaipopo.

Barrick yakinga kifua

Ilipotafutwa na The Globe and Mail, Barrick Gold, ambayo ilitwaa hisa zote za Acacia Tanzania na sasa kuendesha migodi ya Bulyanhulu na North Mara kwa ubia na Serikali kupitia kampuni ya Twiga haikuwa tayari kujibu maswali kuhusu barua pepe hizo za ndani ikisema Acacia ilikuwa na bodi na menejimenti huru hadi 2019.

Akizungumza kile kinachohusishwa na malipo ya fedha hizo kulinda uvunjifu wa haki uliokuwa ukifanywa na Acacia, msemaji wa Barrick Gold, Kathy du Plessis, alisema tuhuma za kuwa Acacia ilikuwa na uhusiano uliopitiliza na vyombo vya dola nchini hazina maana.

“Tuna imani kuwa hata tuhuma zilizotolewa katika mahakama ya London kwa kesi inayoendelea haina maana na tunatarajia kuwa mwishoni mahakama itatupilia mbali jambo hili,” alisema Du Plessis akijibu tuhuma za mawakili wanaowawakilisha walalamikaji Watanzania aliyesema malipo kwa NTF yalisababisha uhusiano usio wa kawaida.

“Malipo kwa NTF yalikuwa sahihi, kikosi kazi hicho kilisaidia kutoa huduma ya kudhibiti uhalifu mkubwa,” alinukuliwa Du Plessis ambaye alisema kusitishwa kwa malipo hayo Novemba 2015 hakuhusiani na wasiwasi wa kukiuka sera za Acacia bali changamoto za kiuchumi.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi