Kitaifa

WhatsApp yakanusha kusudio la kurusha matangazo wakati wa ‘kuchat’

Dar es Salaam. Will Cathcart, mkuu wa kampuni cha WhatsApp, inayomilikiwa na kampuni mama ya Meta ambayo inamiliki mitangao ya kijamii ya WhatsApp, Intragram, Facebook na Threads, amekanusha ripoti zilizosambaa kuwa na kusudio la kutambulisha matangazo, kama njia ya kuongeza mapato.

Awali, ripoti ya FT iliyotolewa leo Septemba 15, 2023; ilieleza kuwa kampuni hiyo inakusudia kuanza kuweka matangazo kupitia programu yake ya WhatsApp kama njia ya kuongeza mapato.

Hata hivyo, saa moja baadaye, bosi huyo wa WhatsApp, aliandika katika akaunti yake ya mtandao wa X (awali Twitter), huku akiambatanisha taarifa ya FT, akionyesha kujitenga na madai hayo na kuyaita kuwa ni ya uongo.

“Hii taarifa ya FT ni ya uongo. Hatufanyi hivi. Pia inaonekana kama umeandika vibaya jina la Brian…” Kanusho hilo la Cathcart limeeleza.

Kwa mujibu wa Reuters, awali FT iliripoti kuwa timu za Meta zimekuwa zikijadili iwapo zitaonyesha matangazo katika mtandao wao, wakati wa mazungumzo ya WhatsApp, lakini hakuna maamuzi ya mwisho ambayo yamefanywa, kwa mujibu wa vyanzo vilivyo karibu na mpango huo.

Taarifa hiyo pia pia imesema kuwa Meta ilikuwa inafikiria kuweka ada ya kujisajili kwa mtu atakayetaka kutumia programu hiyo bila matangazo, madai ambayo pia yamekanushwa na WhatsApp.

Kwa mujibu wa Reuters, WhatsApp imesema: “Hatuwezi kuingilia mazungumzo ya watu, siyo kusudio letu hata kidogo, hatujalifanyia kazi wala kujaribu kwani sio mpango wetu.”

Hata hivyo, hivi karibuni WhatsApp imetangaza kuzindua kipengele chake cha chaneli za WhatsApp nchini India.

Kampuni hiyo imesema itasambaza kipengele hicho kipya kwa zaidi ya nchi 150, ambacho kitaongeza faragha kwa watumiaji wake kama vile mashirika, timu za michezo, wasanii na viongozi ambao watumiaji wanaweza kuwafuatilia, japo kwa sasa chaneli hizo mpya, hazipatikani kwa kila mtu.

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi