Kitaifa
Rais Samia awaapisha majaji, viongozi aliowateua
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewaapisha majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, pamoja na viongozi wengine aliowateua kushika nyadhifa mbalimbali Serikalini.
Septemba 3, 2023, Rais Samia aliteua majaji 24, wanne wakiwa wa Mahakama ya Rufani na 20 wakiwa majaji 20 Mahakama Kuu.
Vilevile, aliwateua Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Said Mussa. Mwingine ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG), Profesa Kennedy Gastorn.
Hafla ya kuwaapisha wateule hao imefanyika leo Septemba 14, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Jaji Mkuu, Profesa Juma amesema tangu ulipoingia umeteua jumla ya majaji 19 wa Mahakama ya Rufani na majaji 63 wa Mahakama Kuu.
“Tunakushukuru, hiyo ni idadi kubwa sana, ni uwezeshaji mkubwa na wakati huu tunaweza kuanza kujilinganisha na nchi nyingine kwa kusema kwamba tunaanze sasa kujipima kuangalia tuna majaji wangapi kwa kila watu 100,000 au watu milioni moja,” amesema.
Amesema idadi ya majaji wa Mahakama Kuu sasa ni 105 na kwamba Jaji Kiongozi anasema ni idadi nzuri na atapanga safu katika mikoa mbalimbali kwa nafasi bila kuwa na presha yoyote.
Profesa Juma amesema majaji ni gharama kubwa, hivyo kuteuliwa kwa majaji hao ni kujitoa kwa Rais Samia katika kuhakikisha idadi yao inaongezeka.
Amesema wanajaribu kuangalia kwa picha kubwa matokeo ya ongezeko la majaji kuwa ni kusogeza huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
“Kwa hiyo majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu tujione katika picha hiyo, kwamba tunalenga kusogeza huduma kwa wananchi,” amesema Jaji Mkuu.
Amebainisha kwamba Mkoa wa Singida ambao una watu 2,858,000 lakini hauna Mahakama Kuu, wanategemea majaji wanne waliopo Mkoa wa Dodoma wenye watu 3,085,625.
Baada ya kupata majaji wapya, Jaji Kiongozi atakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi tutakapofungua Mahakama Kuu Singida kuweza kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na mikoa mbalimbali,” amesema.
Mikoa ambayo haina Mahakama Kuu ni Pwani, Geita, Simiyu, Njombe, Songwe na Katavi na Pemba. Amesema fedha zimepatikana kwa ajili ya kujenga Mahakama Kuu kwenye mikoa hiyo na tayari majaji wamepatikana kwa ajili ya kuhudumia maeneo hayo.
Kwa upande wa majaji wa rufani, Jaji Mkuu amesema watakuwa na uwezo wa kuongeza majopo ya majaji wa kusikiliza mashauri, angalau majaji watatu, siyo tu Mahakama ya Rufani, bali pia katika vituo 17 ambavyo mahakama hiyo inatoa huduma.