Kitaifa
Samia: Kila la kheri darasa la saba, Serikali imejipanga katika miundombinu ya elimu

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewatakia kheri watahiniwa wanaofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi unaofanyika leo na kesho.
Jumla ya watahiniwa 1,397,370 wanatarajia kufanya mtihani huo leo Jumatano Septemba 13, 2023 ambapo kati yao wavulana ni 654,652 sawa na asilimia 46.85 na wasichana 742,718 sawa na asilimia 53.15.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X wa Rais Samia amewataka watahiniwa hao kuwa watulivu akieleza kuwa Serikali imekamilisha maandalizi ya miundombinu ya kuwapokea wote watakaokwenda kidato cha kwanza katika mwaka ujao wa masomo.
“Nawatakia kila la kheri wanafunzi wote wa darasa la saba wanaoanza mitihani yao ya kuhitimu leo. Mmefikia hatua muhimu ya safari yenu ya awali, kuelekea njia mtakazochagua siku za usoni katika kutoa mchango wenu kusukumu mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa letu.
“Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu alivewasimamia toka mwanzo wa safari hii ya elimu hadi sasa, akawape utulivu na afya njema, ili mfanye vizuri mitihani yenu,”amesema.
Jana Jumanne Septemba 12, 2023 Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda aliwataka maofisa elimu na kamati za mitihani kuanzia shule hadi mikoani wafungue macho na kuhakikisha hakuna udanganyifu unaotokea kwenye mitihani.
“Tunaendelea kudhibiti wizi wa mitihani kwasababu ya hatua kali ambazo tumeendelea kuzichukua, udanganyifu hasa wizi wa mitihani hasa ule unaoandaliwa na walimu au wenye shule au Maofisa wa serikali unakwaza mfumo wa elimu.”
“Ukimfundisha wizi wa mitihani unamfundisha mtoto wizi mapema sana na inaharibu weledi katika mfumo wetu wa elimu nchini, mwanafunzi atakayepenya kwa wizi wa mitihani madhara katika uchumi wetu yatakuwa makubwa sana,”amesema Mkenda.
