Connect with us

Kitaifa

Kivumbi cha demokrasia nchini

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amevunja ukimya kuhusu hali ya kisiasa nchini kwa kueleza masuala yanayomkera katika uendeshaji wa demokrasia na utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi.

Rais Samia alieleza hayo juzi Septemba 11, 2023 alipofungua mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wa demokrasia wa kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi na hali ya kisiasa, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa siku tatu unaohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wajumbe zaidi ya 700, unawapa nafasi ya kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali baada ya kusikiliza mawasilisho yanayotolewa.

Katiba mpya

Rais Samia alitumia fursa hiyo kuzungumzia mchakato wa Katiba mpya, akiweka bayana kuwa anakubaliana na utaoji wa elimu ya Katiba kwanza, suala ambalo majuzi liliibua mjadala mkali lilipoelezwa kwa mara ya kwanza na aliyekuwa waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro.

Rais alisema maoni yote yaliyotolewa na makundi tofauti yanafanana na wengi walizungumzia suala hilo, kila kundi likitaka jambo hilo litekelezwe kwa namna tofauti.

“Wote wamesema Katiba na wote tukasema tunakubaliana na marekebisho ya Katiba, lakini jambo hili ni mchakato, Katiba si jambo la vyama vya siasa, ni ya Watanzania wote, awe na chama, awe hana, awe na dini au hana,” alisema Rais Samia.

Akijenga hoja ya elimu, Rais Samia alisisitiza kwamba matengenezo ya Katiba yanahitaji tafakuri kubwa kwa kuwa yanahusisha Watanzania wote na kwamba hawawezi kutoka na kuanza kuandika Katiba haraka ilimradi ikamilike.

“Tunataka tukifanya marekebisho, yatuchukue muda kitabu chetu kile kiende. Lakini Katiba ni kitabu tu, tunaweza kutengeneza Katiba, kitabu kizuri, tukakipamba, tukakiweka. Wangapi wanakielewa hicho kitabu?” alihoji Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi alisisitiza kwamba elimu ya Katiba kwa wananchi ni muhimu kwa sababu wanahitaji kujua yaliyomo ndani ya Katiba ya sasa kabla ya kuwataka watoe maoni yao kuhusu kitu ambacho hawakifahamu.

“Unakwendaje kumuuliza Mtanzania maoni yake wakati kitu hakijui? Tunaanza na elimu ya Watanzania wajue kitu gani kimo kwenye Katiba. Wajue hicho ni kitu gani, kinasemaje…Viongozi wa kisiasa tunadhani tuna haki ya kuburuza watu, tunachokisema sisi watu wote wafuate,” alisema.

Kauli hiyo ya Rais Samia inapigilia msumari msimamo uliotolewa na aliyekuwa Dk Ndumbaro alisema kwamba Serikali inakusudia kutoa elimu ya Katiba kwa miaka mitatu kwanza ili kuhakikisha wananchi wanaifahamu Katiba ya sasa.

Mbali na elimu, Rais Samia aliuhusianisha umuhimu wa elimu ya Katiba na utashi wa kuiheshimu, akisema huwezi kuheshimu kitabu hadi ujue maana yake na ndani yake kuna nini.

Katika hili alisema “Katiba siyo kitabu, bali ni morality and ethical standards” (viwango vya maadili).

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa diaspora Tanzania, Lee Saydou alisema Katiba za mataifa mengine haziwezi kuwa sawa na ya Tanzania kwa sababu haziendani na maadili ya Taifa hili, hivyo ni muhimu kulinda maadili ya Kitanzania.

“Niwaombe Watanzania wenzangu, tuwe wavumilivu, tuungane na Rais wetu katika kuelekea kupata Katiba mpya,” alisema Saydou.

Maadili ya uchaguzi

Katika hatua nyingine, Rais Samia alisema Sheria ya Vyama vya Siasa imebainisha mambo ambayo vyama vya siasa vimekubaliana kuwa yatakuwa ndiyo maadili yao.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuheshimu sheria za Serikali, kuheshimu maisha binafsi ya mtu, kuepusha fujo na vurugu, kuepusha uvunjifu wa amani na uharibifu wa mali, kuepuka vitendo vya ubaguzi na kutosema taarifa za uongo.

“Tunapokwenda kwenye uchaguzi, Serikali tunajipanga kuhakikisha kwamba haya yanakwenda kutekelezwa kikamilifu na vyama vya siasa vijipange kuhakikisha kwamba kila chama kinakwenda kutekeleza ipasavyo,” alisema.

Katika eneo hilo, Padri Charles Kitima, Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alisema katika eneo la maadili bado kuna matatizo na panatakiwa kufanyiwa marekebisho.

Alisema mwakani kuna uchaguzi wa Serikali za mitaa, hivyo muda wa kufanya mabadiliko ni sasa tena kwa haraka na kuwa Rais Samia amesema yuko tayari kupokea maoni yote.

“Sisi tunategemea maoni yatakayotolewa yakafanyiwe kazi ili kurekebisha, kwa sababu tumeona hatari kubwa ya uharibifu wa shughuli ya uchaguzi wa mwaka 2019 na mwaka 2020 ambapo wananchi walinyimwa uwakilishi katika halmashauri na katika Bunge,” alisema.

Alisema wananchi wamekuwa hawana uwakilishi ndiyo maana katika kutatua matatizo ambayo yamejitokeza kama vile Loliondo, hakuna watu wa kuwasemea. Pia, alisema wabunge wanashindwa kutetea ubinafsishaji wa rasilimali kwa sababu walipitisha.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasini alisema kauli ya Rais Samia ya kufufua mchakato wa Katiba mpya inatia matumaini na kwamba itawasaidia namna kwenda kwenye chaguzi zijazo.

“Matarajio yetu sisi wanasiasa na Watanzania kwa ujumla, ni kwamba mchakato wa Katiba utakapoanza, tuwe na tume huru ya uchaguzi itakayosimamia uchaguzi ili kila mtu aone kura yake inakwenda kwa mtu aliyemkusudia,” alisema Selasini.

Aliongeza kuwa Tanzania haiwezi kupata maendeleo kama wananchi watakuwa na viongozi ambao hawakuchaguliwa kihalali na wananchi.

Akisisitiza, Selasini aligusia mapendekezo yaliyotolewa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), akisema ni mazuri na yatasaidia kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi.

Uhuru wa maoni

Miongoni mwa mambo aliyoyatilia mkazo Rais Samia, ni kila mtu kuwa na uhuru wa kutoa maoni yake, hata hivyo alionya kwamba hakuna uhuru usiokuwa na mipaka.

Alitumia fursa hiyo kuwataka wanasiasa wazingatie sheria na utu wakati wakitoa maoni yao.

Alisisitiza kwamba Serikali iliamua kuruhusu mikutano ya hadhara ili vyama vya siasa vikajiimarishe kwa wananchi kwa kueleza sera zao zitakazowashawishi wananchi ili wavichague vyama vyao kwenye chaguzi zijazo.

“Hatukutoa fursa hii watu wakasimame kutukana, watu wakasimame kukashifu, watu wakasimame kuchambua dini za watu. Lakini sishangai haya kutokea, kwa sababu hakuna ya kuzungumza. Walianza na Katiba, ikaja bandari, sasa wameanza tena Katiba,” alisema.

Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kutumia fursa ya mikutano ya hadhara kujiimarisha ili vinapokwenda kwenye uchaguzi vifanye vizuri.

Rais Samia, alisema uendeshaji wa nchi hii unahitaji ushiriki wa kila mtu na kwamba hakuna aliye na hatimiliki ya nchi hii.

Alisema ili nchi hii iendeshwe vizuri, inahitaji ushiriki wa kila mmoja katika kutoa mawazo.

“Tunatofafautiana kiwango cha akili pia, kila mtu ana mawazo yake. Tutatofautiana maoni, inakubalika, sasa katika tofauti hizo, tusiende kutengeneza mambo ambayo yataiharibu nchi yetu. Nchi yetu, Mungu katupa baraka,” alisema Rais Samia.

Hii ina maana gani? Katibu Mkuu wa chama cha DP, Abdul Mluya alisema kauli hiyo ya Rais Samia, imewakumbusha wanasiasa wajibu wao kwenye masuala ya kisiasa na kisheria na pia imekuja na maonyo kuhusu namna ya kufanya siasa za kistaarabu.

“Hotuba yake imeonyesha jinsi gani Serikali iko tayari kupokea maoni hususani yale yaliyotoka kwenye Kikosi Kazi na mengine yanayotolewa na wadau wa demokrasia nchini na kwamba watayafanyia kazi kwa masilahi ya Taifa,” alisema.

Mluya alisema Rais Samia amezungumza kwa uchungu kama mama, kuhusu baadhi ya wanasiasa kutoheshimiana, jambo ambalo alisema ni kinyume cha sheria za Tanzania na utamaduni wa Watanzania.

Ushiriki wa Chadema

Swali lililoibuka vichwani mwa waliofuatilia mkutano huo ni Je, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza kushiriki shughuli zinazoandaliwa na Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania?

Hilo lilijitokeza baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Zanzibar, Said Issa Mohammed kuonekana katika mkutano huo jana, licha ya chama chake kuweka bayana kisingeshiriki.

Ushiriki wa Mohammed umeibua maswali na mijadala huku baadhi ya wanachama wa Chadema wakitaka achukuliwe hatua kali.

Msingi wa mijadala hiyo ni msimamo wa Chadema wa kutoshiriki shughuli zozote zinazoratibiwa na baraza la vyama vya siasa nchini tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu 2020.

Kufuatia mjadala huo, Mwananchi lilimtafuta Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ambaye alisema “alikuwa kwenye Kikosi Kazi cha Zanzibar, hivyo huenda kaenda mwa mwaliko huo labda…,” ni vyema mkamuuliza amekwenda kwa mwaliko upi hasa.”

Akizungumza na Mwananchi, Mohamed katika ukumbi wa Julius Nyerere kunapofanyikia mkutano huo kujua ushiriki wake, Mohammed aliungana na Mrema akisema “msimamo wa Chadema bado upo palepale haujabadilika. Mimi hapa sijaja kama mwakilishi wa Chadema, nimekuja kupita Kikosi Kazi cha Zanzibar ambako huko tunashiriki,” alisema.

“Kwa hiyo isionekane mimi nimekuja hapa kukiwakilisha chama, hapana,” alisisitiza.

Kikosi Kazi cha Zanzibar chenye wajumbe 11 akiwemo Mohammed, kiliundwa na Rais Hussein Ali Mwinyi na alikizindua Oktoba 2022.

Wajumbe wa Kikosi Kazi hicho wanatoka vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na wasomi na mwenyekiti wake ni Dk Ali Uki na makamu mwenyekiti ni Balozi Amina Salum Ali.

Waliohudhuria

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.

Wengine ni viongozi wa vyama vya siasa nchini, asasi za kiraia, viongozi wa dini, waliokuwa wajumbe wa Kikosi Kazi cha Rais, wajumbe wa kikosi kazi cha Zanzibar, mabalozi wanaowakilisha nchini zao hapa Tanzania, Wajumbe kutoka Jukwaa la Wahariri na msajili wa zamani wa vyama vya siasa, John Tendwa.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi