Connect with us

Kitaifa

Zigo linalomkabili Jerry Silaa Wizara ya Ardhi

Dodoma.Vigogo kumiliki ardhi na watumishi wa ardhi kuwa na maslahi katika upimaji, ni miongoni mwa mambo magumu yatakayomkabili Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa.

Kwa mujibu wa wabunge, ugumu wa wizara hiyo unakuja pale ambapo maeneo nyeti nchini yanamilikiwa na wale waliowaita vigogo, hivyo inahitaji moyo wa chuma kuwashughulikia.

Kauli za wabunge kuhusu ugumu huo, zinakuja wiki moja tangu mbunge huyo wa Ukonga jijini Dar es Salaam, aapishwe kushika wadhifa huo ambao awali ulikuwa chini ya Dk Angeline Mabula aliyekuwa akikabiliwa na rundo la migogoro ya ardhi. Kwa mujibu wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 iliyowasilishwa na mtanguzi wake, Mabula inaonyesha hadi kufikia Mei 15 mwaka huu migogoro 2,684 ilikuwa imeshughulikiwa kiutawala.

Jijini Dodoma, migogoro 815 ilipokelewa ambapo 429 sawa na asilimia 52.6 ilipatiwa ufumbuzi na 386 inaendelea kushughulikiwa huku Mkoa wa Dar es Salaam, migogoro 386 ilipokelewa, 201 sawa na asilimia 52 ilipatiwa ufumbuzi na 186 iliyosalia inaendelea kupatiwa ufumbuzi. Tangu alipoapishwa, Silaa ameonekana mara kadhaa kuzungumza na menejimenti ya wizara hiyo na msisitizo wake ni kuomba ushirikiano na kuwataka watumishi wake kumaliza migogoro ya ardhi ndani ya siku 100 na kula sahani moja na wazembe.

Pamoja na mwanzo wa ahadi na msisitizo wa utendaji, inamhitaji moyo wa chuma kwa kuwa nafasi yake hiyo ya kushughulika na ardhi si jambo lelemama, kama anavyoelezwa na wabunge wenzake walipozungumza na gazeti hili.

Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara alisema inahitaji moyo kuwasaidia wananchi wa ngazi ya chini, ilhali maeneo nyeti ya ardhi yanamilikiwa na vigogo.

Waitara aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Tamisemi na Wizara ya Muungano na Mazingira alisema maeneo yenye rutuba na ambayo yalikuwa yakikaliwa na kutumiwa na wananchi wa kawaida yalishachukuliwa na watu wenye fedha na madaraka.

Ingawa si haramu vigogo kuyamiliki, Waitara alisema angalau wawe wameyapata kwa njia halali, kwani aghalabu huyachukua kwa nguvu ya fedha au madaraka. “Maskini ni maskini na bila kuungana atabaki hivyo, ardhi yako unaimiliki kihalali lakini anapewa mtu mwingine na ghafla anajenga au kuiendeleza, ukienda unaambiwa naye ana hati mwisho wa siku unaishia kwenye mgogoro,” alisema. Ujasiri, kujiamini na kufanya kazi bila upendeleo, ndizo mbinu za ushindi zilizotajwa na Waitara katika kuiongoza wizara hiyo, akisisitiza kinyume na hivyo Silaa atakwama.

“Ili hii wizara isiwe fupa gumu Tanzania iweke mkakati wa kuipima ardhi yote,” alisema.

“Namwamini Silaa tangu nasoma naye chuoni, lakini napinga kauli yake kuwa ndani ya siku 100 migogoro itakwisha, haitekelezeki, ajue mingi itakwisha kwa njia ya kisheria ikiwemo mahakamani na lazima iwe na ushirikishwaji hivyo kutoa matamko hakuwezi kuimaliza,” alisema.

Kwa upande wa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Fatma Taufiq alisema kukosekana uaminifu kulikoota mizizi kwa baadhi ya watendaji wa wizara hiyo, ni moja ya maeneo ambayo Silaa anatakiwa kuyaangalia kwa jicho la pekee.

Alisema pia kumekuwepo na tabia ya wapimaji kuhitaji asilimia kadhaa wanapofanya shughuli hiyo. “Watu wanamiliki maeneo yao tangu enzi za mababu zao, unakuja kupima halafu mwananchi mzawa wa eneo hilo unampa asilimia 60 au 40 ya ardhi yote aliyokuwa anamiliki halafu tena analipia, huu mpango si mzuri, namuamini Silaa na tutampa ushirikiano,” alisema Fatma.

Aanze upya

Kumbe mpango wa kamati ya mawaziri wanane, haukuwa mujarabu kulingana na mtazamo wa baadhi ya wanasiasa, wakimtaka Silaa aachane nao na akaanze upya, kama inavyofafanuliwa na mmoja wa wabunge wa Kanda ya Ziwa aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Kufeli kwa kamati ya mawaziri wanane, alisema kumetokana na kufanya kazi bila kuwashirikisha wananchi, waliishia kukutana viongozi na walichokiamua hakikuungwa mkono.

Mbali na ushauri kutoka kwa wabunge wenzake, Silaa alipata baraka za utendaji kutoka kwa mtangulizi wake, Dk Angeline aliyesema yupo tayari kumpa ushirikiano wa kila namna.

Mwanzo na maelekezo

Mwanzo wa uongozi wake katika wizara hiyo umekumbana na maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko aliyemtaka kuhakikisha ardhi inapangwa, kupimwa na kumilikishwa kwa ufanisi ili kuondoa migogoro.

Dk Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati alitaka wizara hiyo isigeuke kuwa mtatuzi wa migogoro, badala yake isimamie jukumu lake ya msingi ambalo ni kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ili kuondoa migogoro.

“Lipo wimbi la kuweka mvutano wa wizara kutoka kwenye sheria yake au ilani ya uchaguzi na kugeuka kuwa wizara ya utatuzi wa migogoro, kuanzia sasa tuwafanye Watanzania wazungumze mipango miji, maendeleo ya makazi na matumizi bora ya ardhi,” alisema Dk Biteko alipofungua kituo cha Taifa cha ubunifu na mafunzo ya taarifa za kijiografia jijini Dodoma juzi.

Continue Reading

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi