Kitaifa
Serikali yatumia Sh27.83 bilioni kulipa fidia ajali, magonjwa kazini
Arusha. Serikali imesema gharama za fidia za ajali na magonjwa yanayotokana na kazi zimeongezeka kutoka Sh13.19 bilioni kwa kipindi kilichoishia Juni 2021 hadi kufikia Sh27.93 bilioni Juni 2023.
Aidha imesema masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ni suala la msingi ili kulinda nguvu kazi ya Taifa na mtaji wa mwekazaji hivyo basi tungependa kuona kuwa kila muwekezaji anazingatia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Septemba 10,2023 na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu) Mhandisi Cyprian Luhemeja,akizungumza katika mafunzo ya masuala ya usalama na afya mahala pa kazi kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (Osha)
“Kwa taarifa ya baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii hapa nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja Julai 2020/21, ajali zilizoripotiwa zilikuwa 1,889 na kati hizo vifo vilikuwa 75. Sambamba na hayo gharama za fidia zimeongezeka kutoka Sh13.19 bilioni kwa kipindi kilichoishia Juni 2021 hadi kufikia Sh27.93 Bilioni kwa kipindi kilichoishia Juni 2023,”amesema.
Amesema takwimu za Shirika la Kazi Duniani(ILO) zinaonyesha kwa mwaka wafanyakazi milioni 2.3 wanakufa kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kati ya hizo takwimu vifo vinavyotokana na ajali ni takribani wafanyakazi 350,000 na magonjwa yatokanayo na kazi ni yanakadiriwa kuwa milioni 1.95.
“Tafsiri yake ni kwamba watu 6,400 hupoteza maisha kila siku duniani kutokana na magojwa na ajali zitokanazo na kazi, masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ni suala la msingi ili kulinda nguvu kazi ya Taifa na mtaji wa mwekazaji hivyo basi tungependa kuona kuwa kila muwekezaji anazingatia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi,”amesema
Waziri,Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako amesema ni muhimu nguvu kazi ya taifa kulindwa kwa kuwekwa mifumo ya kudhibiti vitaharishi na kulinda usalama na afya mahali pa kazi kwa wafanyakazi kote nchini.
“Ni muhimu kuhakikisha tunaweka mifumo endelevu ya kulinda usalama na afya mahali pa kazi, mifumo hii ni dhahiri kwamba inahitaji fedha ndiyo maana tuko na nyie wajumbe wa kamati muhimu ya bajeti ambayo inasimamia masuala ya bajeti ili tunaposema tunaomba fedha za kudhibiti mifumo ya usalama mahala pa kazi muwe na uelewa wa kina,”amesema Profesa Ndalichako
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Daniel Sillo amesema kunapokuwa na jamii au wafanyakazi wenye afya bora sehemu ya kazi hata tija na ufanyaji kazi na matokeo yanayotarajiwa yatapatikana.