Kitaifa
Lissu, viongozi wengine Chadema washikiliwa na polisi Arusha
Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu na viongozi wengine wa chama hicho kwa mahojiano kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko bila kibali na kuzuia polisi kufanya kazi yao.
Lissu amekamatwa wilayani Karatu mkoani Arusha ambapo leo Jumapili Septemba 10, 2023 alitarajia kufanya mkutano wa hadhara katika viwanja wa Mazingira Bora.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Justine Masejo amesema Lissu na viongozi wengine watatu wanashikiliwa kwa mahojiano na baadae taratibu za kisheria zitaendelea.
Lissu kabla ya kutiwa mbaroni tangu asubuhi hoteli aliyofikia Karatu ya Ngorongoro creater ilikuwa imezingirwa na polisi na hoteli nyingine ya Panorama ambayo walifikia viongozi wengine nayo ilizingirwa na polisi.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Arusha, Elisa Mungure pia ameeleza kukamatwa kwa Lissu, walinzi wake na viongozi wengine huku akidai walikuwa njiani kupelekwa Arusha kwa mahojiano.
Taarifa zaidi za tukio hili zitaendelea kutolewa