Kitaifa
‘Polisi waachwe wasifanye kazi kwa maelekezo kwenye chaguzi’
Moshi/Dar. Wakati Rais Samia Suluhu akiahidi kulitafutia Jeshi la Polisi Sh125 bilioni ili lisimamie vizuri uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na uchaguzi mkuu, wadau wameainisha mambo linalopaswa kufanya na wasiyostahili kuyafanya.
Wadau hao wakiwemo wasomi, wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu, wametaka jeshi hilo litimize wajibu wa kikatiba na kisheria wa kulinda raia na mali zao, na lisigeuke kuwa mwamuzi wa ndondi ambaye ana bondia wake mfukoni.
Kulingana na wadau hao, dalili zinaonyesha uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na uchaguzi mkuu 2025 utakuwa na ushindani mkubwa kwa vyama na wagombea, hivyo polisi wasiwe chanzo cha vurugu kwa kupendelea upande wowote.
Wakili David Shillatu ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha Mawakili nchini (TLS), kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga alienda mbali na kusema Jeshi la Polisi lina wajibu mkubwa kuhakikisha chaguzi hizo zinakuwa za haki na huru. “Kama alivyosema Rais, polisi wana dhamana ya kuhakikisha huu uchaguzi unapita salama. Niwasihi sana wafanye majukumu yale tu yanayowahusu na wasiwe na upendeleo katika maamuzi yao,” alisema.
Chaguzi hizo mbili zinaenda kufanyika huku wadau wakiwa na kumbukumbu ya kile kilichotokea katika chaguzi kama hizo zilizopita, huku jimbo la Kawe kukiwa na taarifa za kukamatwa watu walioshukiwa kuwa polisi wakiwa na vibegi vye kura.
Septemba 4, 2023, akizungumza katika mkutano wa watendaji wakuu wa jeshi hilo, makamanda wa polisi wa mikoa na wakuu wa vikosi jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema atahakikisha fedha hizo zilizoombwa na IGP, Camilius Wambura zinapatikana.
“Mwakani tuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, nitataka Jeshi la Polisi liwe makini katika maeneo mbalimbali kuhakikisha haki inatenddeka na kusimamia usalama katika chaguzi zetu ili zimalizike kwa njia salama.
“Nilimwambia IGP Wambura, akasema sawa ila akasema ana changamoto, akaniletea bajeti ya karibu Sh125 bilioni ambayo nakwenda kupekua ikiwezekana nipate yote ili changamoto zote ziondoke muweze kufanya kazi vizuri”
“Tegemeo letu ni nyie, ndio mnalinda mali na usalama wetu, hatuna jeshi lingine. Nakwenda kuihangaikia bajeti hiyo ili niwawezeshe mkasimamie vyema chaguzi zetu. Nasema kila siku Tanzania ni moja, hakuna nyingine,”alisema Rais Samia.
Hiyo ilikuwa ni kauli ya pili ya Rais kuhusiana na uchaguzi, awali Septemba Mosi akiwa Ikulu ndogo Zanzibar, alisema amemteua Mohamed Mchengerwa kuwa waziri wa Tamisemi kutokana na kivumbi cha uchaguzi mwakani.
“Sasa nimempeleka Tamisemi. Mwakani kuna kivumbi na mimi nakujua. Najua unaweza. Kivumbi kile kinafanana na kifua chako. Kwa hiyo nimekupeleka Tamisemi ni kazi kazi ili mwakani tupite vizuri,”alisema.
Chaguzi hizo mbili zinaashiria kuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa zinafanyika katika mazingira tofauti na chaguzi za 2019 na 2020 zilizofanyika wakati mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ikiwa imezuiwa, isipokuwa ya kampeni.
Itakumbukwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, kipande cha video kilisambaa mitandaoni kikimuonyesha ofisa mmoja wa polisi akimwambia aliyekuwa mgombea ubunge katika jimbo la Hai (Chadema), Freeman Mbowe kwamba hatashinda kwenye uchaguzi huo.
Kutokana na kauli hiyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) wa wakati huo, Simon Sirro alituma timu yake kutoka Makao Makuu ya jeshi hilo kwenda mkoani Kilimanjaro kufanya uchunguzi wa video ya ofisa huyo ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yake.
Nini polisi wafanye, kipi wasifanye
Wakizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu kwa nyakati tofauti, baadhi ya wadau wametaja mambo ambayo polisi waliyafanya katika baadhi ya maeneo nchini na kuwa kiini cha vurugu, au kufanya wadau waone lilikuwa na mkono kuvuruga matokeo.
Ni kutokana na uzoefu wao, wametaja baadhi ya mambo ambayo kama polisi watayafanya au kutoyafanya, chaguzi hizo zinaweza kuwa huru na haki kulinganisha na chaguzi za serikali za mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020.
Moja ambalo linaelezwa ni polisi wenye sare na silaha kuwepo ndani ya vituo vya kupigia kura, na wakati mwingine polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), zaidi ya wawili kuingia ndani ya kituo cha kupigia kura au wakati hatua ya kuhesabu kura.
Hii kwa mujibu wa wadau waliozungumza na gazeti hili, wanadai polisi wanapaswa wewe nje ya kituo na wasiwe na sare ili kuepuka kuwatia hofu wapiga kura, lakini kitendo cha kuingia ndani ya vituo huwa kunajenga hisia ya michezo michafu.
Kuna maeneo, wadau walieleza kuwa baadhi ya askari waliokuwepo vituoni waliwanyang’anya mawakala wa vyama nakala za karatasi za matokeo ya kura, na baadaye kusimamia kubandikwa karatasi zenye matokeo tofauti.
Mambo mengine ambayo hawapaswi au wanapaswa kuyafanya ni kulinda mikutano ya hadhara ya kampeni na si kuisimamia, ambapo katika baadhi ya maeneo polisi wanadaiwa kuwaelekeza wagombea wasieleze baadhi ya mambo.
Basili Lema ambaye ni Katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro, alitolea mfano uchaguzi mkuu 2010, baadhi ya maofisa wa polisi walikuwa wanapanda majukwaani na kuwataka wagombea wao wasizungumzie kashfa ya Richmond.
“Polisi wetu wakifanya mambo ndani ya sheria wala hutasikia manung’uniko. Tatizo ni kufanya upendeleo wa wazi kwenye chaguzi. Kuna jambo likifanywa na upinzani ni kosa, lakini hilohilo likifanywa na CCM sio kosa,”alisema.
Renatus Muabhi aliyekuwa Katibu mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), alisema polisi hawapaswi kuwa wasafirishaji wa masanduku ya kura, badala yake liwe jukumu la wasimamizi na mawakala na wao watoe tu ulinzi.
“Kuna lingine ambalo hawapaswi kulifanya. Ni hili la kuingilia mamlaka ya Tume ya Uchaguzi kuvibadilishia vyama maeneo ya kufanyia mikutano kwa sababu mbalimbali. Hili sio lao. Kama kuna mgogoro wa eneo waiachie Tume,”alisema.
Pia alitolea mfano wakati wa kuchukua fomu za kugombea katika ofisi za wasimamizi ambapo baadhi ya polisi wanachukua jukumu la kuelekeza namna ya kujaza fomu na hudhibiti urejeshaji kwa wagombea upinzani.
“Unakuta mnarudisha fomu polisi wanawafukuza wanawaambia kaeni mbali kule nje mita 100 au 200. Mnakaa nje mpaka muda wa mwisho unafika unaona msimamizi anabandika fomu ya mgombea mmoja na nyie mpo. Si sawa,”alidai.
Walichokisema wadau wa demokrasia
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie alisema kitu kikubwa ambacho Jeshi la Polisi linapaswa kufanya wakati wa mchakato wa uchaguzi ni kutoa ulinzi bila kubagua vyama vya siasa.
“Kuna mifano halisi ambayo kwa kweli Jeshi la Polisi limefanya vizuri kwenye mikutano ya Chadema. Chama hicho kimekuwa kikifanya mikutano yake kanda ya Ziwa, unaona kabisa polisi wanatoa ulinzi, hakuna chochote tunachoona ni tofauti,” alisema.
Kuhusu mambo wasiyotakiwa kufanya, Dk Loisulie alisema ni upendeleo hasa kwa kutumia maneno yaliyozoeleka kwamba “intelijensia imetuambia” ili mradi kukwamisha shughuli za vyama vya upinzani.
“Kusimamia ulinzi na usalama bila upendeleo inawezekana tu pale ambapo sheria zetu zimebadilishwa ili kuakisi hali halisi ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, kama bado sheria hazijabadilishwa, maana yake mazingira hayatakuwa sawa kwenye huo uchaguzi. “Kama chama tawala kitaridhia Jeshi la Polisi lifanye kazi yake na kikaacha utegemezi, litafanya kazi yake vizuri. Jeshi la Polisi halina tatizo katika kusimamia chaguzi, lakini kama mambo haya hayajawekwa sawa, malalamiko yataendelea kuwepo,” alisema.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kubadilika kulingana na mabadiliko ya nyakati, kwa kuwashauri wa mamlaka za juu badala ya kupokea maelekezo.
“Wanasiasa siyo wajuzi wa masuala ya ulinzi, amani na usalama, wao matakwa yao ni kushinda uchaguzi na kuendelea kuwa madarakani, kwa hiyo hivi ni vitu viwili ambavyo mara nyingi huwa vinashindana.
Migogoro mingi Afrika inatokea kwa sababu hiyo,” alisema Dk Kristomus.
Alisisitiza kwamba jeshi hilo lijipe wajibu wa kuwaeleza wakubwa kwamba kutakuwa na hatari fulani endapo watafanya vile wanavyotaka mambo yafanyike, hasa kwenye suala la amani na usalama wa nchi.
“Jeshi la Polisi litambue kwamba siasa na ustawi wa Taifa ni mambo tofauti, sote tuna jukumu la kupigania ustawi wa Taifa kwa siku za mbeleni. Tukitumikia sana masilahi ya kisiasa, tutaliharibu Taifa la baadaye,” alisisitiza mwanazuoni huyo.