Kitaifa
Rais Samia kuwahutubia vijana wa Afrika mkutano AGRF
Dar es Salaam. Marais saba kutoka Afrika wamethibitisha kuwa kesho Septemba 7, 2023 watashiriki majadiliano ya Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) linaloemdelea jijini hapa.
Jukwaa hilo ambalo lilianza Septemba 5 mwaka huu linatarajiwa kukamilika Septemba 9 ambapo fursa mbalimbali katika kilimo zinazopatikana Tanzania zinawekwa wazi kwa washiriki.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya utaratibu utakavyokuwa katika kikao hicho cha marais.
“Marais waliothibitisha kushiriki ni saba, Labda na wengine wataendelea kujitokeza kwa sababu mkutano ni kesho, inawezekana wakaongezeka au wakaja kwa uwakilishi,” amesema Msigwa.
Msigwa amesema marais hao watafanya majadiliano, kila mmoja kutoa hotuba yake, kupokea taarifa mbalimbali na badaye maazimio ya mkutano huo yatawasilishwa.
“Jioni wageni wataalikwa Ikulu ambapo tuzo ya mzalishaji wa Chakula Afrika itatolewa ikiwa ni kutambua mchango wa uzalishaji wa chakula Afrika,” amesema Msigwa.
Kabla ya mkutano huo, asubuhi ya kesho Rais Samia Suluhu Hassan asubuhi atahutubia vijana na kupokea taarifa juu ya namna vijana wa Afrika wanajihusisha na kilimo na kutumia fursa mbalimbali za kilimo.
“Baada ya taarifa hiyo na yeye atatoa muelekeo wake juu ya namna anavyoona bara la Afrika linavyoweza kusaidia vijana kupata ajira kupitia kilimo,” amesema Msigwa.
Akizungumzia mkutano wa AGRF, Msigwa amesema mkutano huo ni wa kimkakati kwani unaiunganisha Tanzania na wadau kutoka bara la Afrika na wale wa nje ya bara la Afrika katika ajenda ya kukuza kilimo.
“Tunafahamu uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Serikali katika sekta hii na sasa bajeti inakaribia Sh1 trilioni kwa ajili ya kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo ambayo inakenga kuwatoa wakulima katika kilimo cha mazoea cha kutegema mvua,” amesema Msigwa.
Amesema pia mageuzi hayo yamelenga kuwasaidia wakulima kutumia mbegu bora, kuwa na hifadhi nzuri ya mazao, kusaidia vinana kwenda katika kilimo ambapo watapata manufaa baada ya kazi ambazo walikuwa wanafanya na hawajafanikiwa.
Bajeti ya Wizara ya Kilimo imekuwa ikipaa kwa miaka mitatu mfululizo ambapo kwa mwaka 2022/23 imepanda kutoka
Sh751.12 bilioni hadi kufikia Sh970.78 bilioni mwaka 2023/24 sawa na ongezeko la asilimia 29.24.