Kitaifa
Fahamu hatari ya matumizi ya vyombo vya plastiki

Dar es Salaam. Ni jambo la kawaida katika jamii kutumia vyombo vya plastiki katika shughuli mbalimbali.
Lakini je, kuna matumizi sahihi ya vyombo hivyo, ni vitu gani watu wasifanye wanapovitumia na kwa nini?
Majibu ya hayo yanatolewa na mtaalamu wa masuala ya plastiki, Muddy Kimwery ambaye ni mratibu wa kampeni na mawasiliano wa Taasisi ya Nipe Fagio.
Taasisi hiyo inajishughulisha na usimamizi wa mazingira na utengenezaji wa mifumo ya taka ngumu.
Katika mahojiano na Mwananchi, anasema matumizi sahihi ni kuhakikisha chombo husika kinatumiwa pasipo kuwekwa kwenye moto au joto kali.
Anatoa mfano, kwamba unaweza kutumia kikombe cha plastiki kunywea maji ya baridi, lakini ni hatari kukiweka chombo cha plastiki kwenye oveni.
“Plastiki ikiwa karibu na moto au joto kali huyeyuka na kutoa chembechembe ndogo ambazo ama unaweza kuzinywa na maji au kuzila pamoja na chakula na kusababisha madhara kiafya,” anasema.
Kimwery anasema baadhi ya madhara hayo ni kupata saratani na magonjwa mengine kama ya afya ya uzazi.
Anasema kuna tafiti zimeonyesha chembechembe hizo za plastiki pia huonekana kwenye mzunguko wa damu wa binadamu kutokana na matumizi mbalimbali.
Mtaalamu huyo anasema chembechembe hizo zipo kwenye chupa za plastiki za vinywaji, vifungashio vya chakula vya plastiki, mifuko na sehemu nyingine.
Anasema utatuzi ni kuepuka kutumia plastiki na badala yake vitumike vyombo vya bati, udongo au chupa ambavyo licha ya kulinda afya ya mtumiaji, pia huepusha uharibifu wa mazingira.
Alama kwenye plastiki
Kimwery anasema kuna alama kwenye plastiki, akitoa mfano wa namba moja, mbili na kuendelea.
Anasema namba hizo zina maana ambayo mtumiaji anapaswa kuielewa, akifafanua chombo chenye namba saba hakipaswi kutumiwa karibu na moto.
Mtaalamu huyo anasema namba huendana na malighafi iliyotumika kutengeneza plastiki husika.
Anaeleza, namba moja ni plastiki nyepesi zinazojulikana PET (Polyethylene Terephthalate), zinazotumika zaidi kwenye vinywaji, akitoa mfano wa maji ya kunywa na soda.
Anasema mbili ni plastiki nzito kidogo, zinaweza kuwa nyeupe au zenye rangi zijulikanazo HDPE (High-Density Polyethylene), ambazo hutumika kwa bidhaa kama vifungashio vya dawa za chooni, majagi na mazoleo. Anasema namba hizo zipo nyingi na kwa shughuli tofauti.
Bodi ya maziwa
Kwa upande wake, Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), imetoa tahadhari kwa chupa za plastiki kutumika kuhifadhia bidhaa hiyo.
TDB inasema licha ya maziwa kuwa na virutubishi muhimu vya protini, mafuta, vitamini, madini na maji, ubora hupotea kutokana na namna vitu vingine vinavyoongezwa.
Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk George Msalya aliiambia Mwananchi kuwa, vyombo vya plastiki vizito (FGP) pekee ndivyo vilivyoidhinishwa kubeba na kuhifadhi vyakula.
Alisema chupa za plastiki zinazoweza kuharibika kwa urahisi baada ya kuoshwa kwa maji yaliyochemshwa kwa nyuzi joto 100 huleta tatizo kubwa la kiafya, kwa watumiaji wa maziwa.
“Maziwa yana nyuzi joto 37 yenye uwezo wa kuifanya chupa iathirike na kwa kumomonyoka kwa chembechembe zilizotengeza chupa hiyo huchochea tatizo la saratani kwa watumiaji wa bidhaa hiyo. Hivi karibuni imeelezwa matumizi hayo yanaweza kuchangia vifo,” alisema.
Alisema chupa ambazo zimepigwa marufuku kuhifadhi maziwa ni zinazotumika kuhifadhia maji ya kunywa, sipokuwa kontena nzito za plastiki ambazo zimepakwa rangi maalumu hazina athari za kiafya kwa watumiaji wa bidhaa hiyo.
Alisema vyombo vya aluminiamu au bati vinapendekezwa kutumika kuhifadhia maziwa, japokuwa malighafi zake hazijatengenezwa kiasili.
“Bidhaa za kuhifadhia maziwa tunaagiza kutoka nje, hili ndilo eneo tunalotaka uwekezaji kwa sababu hatuna viwanda vya ndani vya kuvitengeneza,” alisema.
Hali ilivyo
Vyombo vya plastiki kama vikombe, sahani na majagi vimekuwa vikitumika kuhifadhia au kubeba chakula, mara nyingi kikiwa cha moto.
Pamoja na kuhifadhia vyakula, wengine hutumia mifuko ya nailoni kufunikia chakula kikiwa jikoni au kuchemsha vyombo vya kuwalishia watoto maziwa kwa minajili ya kuua bakteria, jambo ambalo kitaalamu inaelezwa si sahihi.
Kauli ya mtaalamu
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Crispin Kahesa anasema vyombo vya plastiki vimetengenezwa kwa kemikali na matumizi ya vyombo hivyo yamewekewa maelekezo.
Dk Kahesa anasisitiza chupa za maji, chupa za maziwa za watoto, bakuli na vikombe vya plastiki, vinatakiwa kutumika kwa uangalifu.
“Watu watumie vitu kulingana na matumizi yake, yakiwa ndivyo sivyo lazima kuwepo athari, miongoni mwa kemikali zinazotumika kutengeneza vyombo hivyo zinahusishwa na saratani, pia kemikali hizo zina uwezo wa kuuvuruga mwili na kusababisha maradhi yasiyo ya kuambukiza,” alisema.
Plastiki anazozungumzia Dk Kahesa ni zisizoweza kuhimili joto la juu, na zinazohimili zinahitaji uangalifu kwenye matumizi.
Baadhi ya wananchi hawana uelewa
Akizungumza na Mwananchi, Selina Masanja, mkazi wa Mtoni Kijichi, alieleza hakuwahi kufahamu kwamba plastiki inatakiwa kutumika kulingana na viwango.
“Binafsi sijawahi kujua kwamba hivi vyombo vya plastiki tunavyotumia vinaweza kuwa na madhara kiafya. “Pia sikuwahi kufahamu kwamba plastiki nayo ina viwango vyake, tangu utotoni tunaishi tukitumia plastiki na sijawahi kuona mtu aliyeumwa.
“Ni kweli huwa tunaweka vitu vya moto kama chai, maziwa na kahawa na ndiyo maisha yetu ya kila siku, ila hatuna sababu ya kubishana, wao wataalamu ndio wameona hivyo,” alisema Selina.
Kwa upande wake, Mwanaidi Seleman ambaye ni mama lishe alisema hafahamu kuhusu madhara, ila hatumii vyombo vya plastiki kwenye biashara yake kwa sababu havina mwonekano mzuri kwa wateja.
Alisema kwa biashara ya chakula vyombo vya udongo na vilivyotengenezwa kwa malighafi ya plastiki ngumu (mfupa), ndivyo vinatumika hivi sasa.
Alisema hana uelewa wa matumizi sahihi ya vyombo vya plastiki na kwamba, vya udongo havidumu kwenye familia nyingi.
Mwanaidi alisema kwa maisha ya Watanzania wengi, hasa waishio katika mazingira duni, si rahisi kukuta mtu ana chombo maalumu kwa ajili ya kuhifadhia maziwa, wengi huweka kwenye chupa za plastiki.
Naye Baraka Majaliwa, mfanyabiashara wa duka la vyombo alisema licha ya vyombo vingi vya plastiki kuwa na alama ya mwongozo wa matumizi, ni wachache ambao wanazingatia hilo.
“Nimeuza vyombo kwa muda mrefu, lakini ni mara chache mteja anakuja akiwa na uelewa wa matumizi sahihi ya hicho anachonunua.
Ukiachana na plastiki, wapo wanaonunua vyombo vya udongo na hawafahamu kwamba vinaweza kutumika kupashia chakula,” alisema
