Kitaifa
Pwani wasema upatikanaji rasilimali fedha, watu vitafanikisha utekelezaji mradi
Kibaha. Wadau wa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto mkoani Pwani (MMMAM ) wamesema upatikanaji wa rasilimali za kutosha za fedha, watu na vifaa ni suala la muhimu zaidi katika kufanikisha utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya Mtoto (PJT -MMMAM) ulioanza kutekelezwa nchini kwa kipindi cha miaka mitano (2021/2022 – 2025/26.) ukilenga watoto wenye umri wa miaka 0 -8 kufikia hatua utimilifu za ukuaji.
Program hiyo pia itasaidia kuboresha uratibu wa huduma kwa kuimarisha utekelezaji wa sheria na sera zinazohusu masuala ya MMMAM ikiwa ni pamoja na sheria ya Mtoto ya mwaka 2008, Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014, sera ya afya ya mwaka 2007 ili kushughulikiwa kikamilifu mahitaji yote ya maendeleo ya watoto wenye umri wa miaka 0-8 ili kufikia hatua timilifu za ukuaji.
Wakizungumza Septemba 2, 2023 kwenye kikao cha maandalizi ya uzinduzi wa Programu hiyo Mkoani Pwani Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Maendeleo ya Vijana (YPC), Israel Ilunde amesema mpango huo ni muhimu na kushauri rasilimali ikiwemo fedha zitengewe kila wizara, kila sekta ikiwemo binafsi na asasi za kiraia na zielekezwe namna ya kutumia katika kulea na kutunza watoto wa umri wa miaka 0 – 8.
“Juhudi za wadau wa maendeleo na rasilimali fedha na vinginevyo zielekezwe kutekeleza afua zilizopangwa katika Programu hii kwa wakati na ufanisi wa hali ya juu ili kufikia malengo, natoa wito wadau wenzeru wengine kusaidia kufanikisha maono ya program hii wajielekeze kuchangia utekelezaji kwa kufanya kazi kwa karibu na Serikali,” amesema Gaidoni Haule kutoka asasi ya Pasada.
Awali Mkurugenzi wa Asasi ya Anjita wanaotekeleza mpango huo mkoani Pwani Janeth Malela amesema mpango PJT -MMMAM umelenga kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya awali ya watoto wenye umri wa miaka 0-8 kwenye maeneo matano ya afya bora, lishe ya kutosha kuanzia ujauzito, malezi yenye muitikio,fursa za ujifunzaji wa awali, ulinzi na usalama kwa watoto,
Afisa maendeleo ya jamii anayeshughulika na watoto mkoani Pwani, Rachel Chuwa ameeleza changamoto zilizopo kwa jamii kwenye mfumo wa malezi ni pamoja na ubize wa wazazi na walezi wengi wamekua bize kutafuta kipato kiasi cha kuwachukua muda mchache kulea watoto nyumbani.
“Hapa Pwani bado wazazi na walezi wapo bizee mnoo kutafuta kipato unakuta mtu kutoka alfajiri amemuacha mtoto mdogo mfano wa miaka minne na mdogo wake miaka miwili wanaleana, hapa ratiba ya chakula haipo sawa, usafi na hata ujifunzaji anaweza kushinda kwenye video na TV na kuangalia vipindi visivyo na maadili hivyo Program hii itasaidia jamii pia kuelewa malezi yenye muitikio, ” amesema.
Takribani robo tatu sawa na asilimia 66 ya watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano walio kusini mwa jangwa la Sahara inadaiwa wapo kwenye hatari ya kutokufikia hatua timilifu za ukuaji kutokana na kukosa malezi bora na yenye muitikio, umasikini, utapiamlo pamoja na matatizo mengine ya kijamii na kiuchumi.