Kitaifa

Mbowe ajitosa maridhiano, Katiba

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema chama chake hakijanufaika zaidi na maridhiano kama kilivyonufaika Chama cha Mapinduzi (CCM), Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mbowe pia amesema uamuzi wa Serikali wa kutoa elimu ya Katiba kwa miaka mitatu ni kuonyesha hawana dhamira na jambo hilo.

Akizungumza na Mwananchi, Mbowe alisema waliopoingia kwenye maridhiano na CCM waliamini chama hicho kimebadilika na kina dhamira ya kweli ya kuleta mageuzi na kukuza demokrasia, lakini kwa kinachoendelea wamepoteza fursa muhimu ya kuijenga nchi.

“Ukweli ni kuwa maridhiano yamemsaidia zaidi Rais Samia kwa kujijengea heshima kubwa kwa washirika wa kimataifa na wadau mbalimbali, sisi tuliamini wenzetu wana dhamira ya dhati, kumbe wanatuhadaa, katika mazungumzo ya maridhiano hakukuwa na eti Serikali itatoa elimu ya Katiba kwa miaka mitatu,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM – Bara, Anamringi Macha amesema maridhiano hayakuibeba Serikali wala CCM kama anavyosema Mbowe, bali yana masilahi kwa Taifa ndiyo maana walishiriki kikamilifu.

Alitoa mfano wa Agosti 30, mwaka huu, vyama vya siasa vilikutana kujadili baadhi ya mambo yaliyopitiwa na kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia, hususan katika uchaguzi, lakini Chadema haikupeleka wajumbe.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Mbowe imekuja wakati kukiwa na taarifa za kukwama na mgawanyiko wa maridhiano baina ya vyama hivyo viwili, ambapo kuna wanaotaka yaendelee na wengine wakiyakataa.

Wapo baadhi ya makada wa Chadema wanaona CCM haina dhamira ya dhati kukuza demokrasia, bali inayatumia kuhalalisha utawala wao ndani na nje ya Tanzania

Wengine wanaamini yamesaidia kutuliza joto la siasa lililokuwapo miaka sita iliyopita chini ya utawala wa hayati John Magufuli kwa kuwa kesi nyingi za kisiasa walizofunguliwa wenzao zimefutwa, waliokimbia nje ya nchi wamerejea na mikutano ya hadhara ya kisiasa inaendelea.

Alipoulizwa juu ya kuendelea kwa mazungumzo ya maridhiano ambayo vikao vya mwisho vilifanyika Mei 31, mwaka huu, Mbowe alisema CCM na Serikali wanayoiongoza ndiyo yenye kujua hatima yake, lakini Chadema wako tayari kila wakati ila hawataki ghiliba.

Hata hivyo Mwananchi, limedokezwa kuwa licha ya msimamo imara wa Mbowe kutaka kuendelea kwa maridhiano, amekuwa akipata wakati mgumu ndani ya Kamati Kuu na makada wengine.

Mbinyo huo ulisababisha chama hicho kuunda timu ya kutathimini faida za maridhiano hayo ambayo iko chini ya Katibu Mkuu John Mnyika, ambayo taarifa yake bado haijawekwa wazi.

Mwananchi, liliwasiliana na Mnyika juu ya walipofikia juu ya maridhiano ambapo hakuwa tayari kuyaweka bayana akidai kuwa Mbowe ndiye atazungumzia kwa kina baada ya kumaliza mikutano ya hadhara wanayoifanya kanda ya Serengeti.

Makada wa Chadema wanaamini kuwa miongoni mwa matunda ya maridhiano yaliyopaswa kupatikana ni kuondolewa bungeni kwa wabunge 19 wa viti maalumu waliofutiwa uanachama ambao kesi yao inaunguruma mahakamani wakipinga kufukuzwa chamani.

Mbowe mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuwa maridhiano ni mchakato unaohitaji muda, uvumilivu na hekima sambamba na kuwahusisha watu wengi zaidi.

Hata hivyo, uamuzi wa Serikali wa kutumia miaka mitatu katika kutoa elimu ya Katiba, umeongeza fukuto kwenye maridhiano ya CCM na Chadema ambapo Mbowe anaamini hakuna dhamira ya dhati kuelekea jambo hilo.

Alisema kauli ya Serikali inaiweka kwenye wakati mgumu wa kuaminika, hivyo Chadema watabadili njia ya kudai Katiba mpya.

Alisema mchakato wa Katiba mpya uendelee katika hatua mbalimbali, huku mabadiliko mengine yakifanyika ili kukidhi mahitaji ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwakani.

“Rais amezungumza Januari 3, mwaka huu akatoa ahadi ya Katiba, tumefanya vikao vya mwaka mzima halafu Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Damas Ndumbaro anasema tuna miaka mitatu ya kutoa elimu kwa wananchi.

Mbowe alisema kauli ya Serikali inaashiria kuvilazimisha vyama vingine kutafuta njia zisizo za kistaarabu kufanikisha kupatikana kwa Katiba mpya.

“Waziri hakutoka mwenyewe, ametumwa na Serikali, ina maana muda wote walikuwa wanatuongopea, si kwenye maridhiano tu wanaongopea wananchi, jumuiya za kitaifa na kimataifa,” alisema.

Warioba apinga miaka mitatu

Naye Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatua ya Serikali ya kutaka kuanza kutoa elimu ya Katiba mpya kwa miaka mitatu, akisema ni muda mrefu.

“Tumefikia mahali kama kuna utashi wa kisiasa, tunaweza kuamua mabadiliko haya. Inanipa wasiwasi, tunataka kuanza upya mchakato huu. Unaona mijadala hii ya Katiba inavyoingilia shughuli zetu za maendeleo, nadhani imefika wakati tufanye uamuzi,” amesema Jaji Warioba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akizungumza juzi katika mahojiano na kituo cha Azam TV yaliyofanyika nyumbani kwake wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam, alisema wakati akiwa mwenyekiti wa tume hiyo, wananchi walishiriki na walitoa elimu ya kutosha kuhusu Katiba mpya.

Alisema walitoa machapisho kueleza yaliyo katika Katiba na kuyasambaza katika maeneo mbalimbali, ikiwemo vijijini, hivyo huwezi kusema wananchi hawana elimu kuhusu mchakato huo.

“Kwa jinsi walivyoipanga sioni kama wanaweza kutoa mwanga zaidi kuliko walionao hivi sasa, Kamati ya Mukandala (Profesa Rwekaza), imechukua maoni ya kutosha na wananchi wanajua. Mimi natafsiri Serikali ingesema hatuwezi kupata Katiba mpya sasa hivi, wangesema mapema kuliko hivi.

Alichokisema Ndumbaro

Siku chache zilizopita, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro aliwataka Watanzania wawe na subira ya miaka mitatu ndipo uanze mchakato wa mabadiliko ya Katiba.

Msingi wa kauli ya Dk Ndumbaro ambaye Alhamisi, Rais Samia Suluhu Hassan alimhamisha kuwa Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, ni kuanza kutolewa elimu kwa umma kuhusu Katiba iliyopo kwa kipindi cha miaka mitatu ndipo mchakato wa mabadiliko uanze.

Katika mkutano na mawaziri wakuu wastaafu na mawaziri wa Katiba wastaafu Agosti 28, mwaka huu, Dk Ndumbaro alisema zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hawaijui Katiba iliyopo.

Kwa sababu hiyo, alisema wizara hiyo (Katiba na Sheria) imeanzisha Mkakati wa Taifa wa elimu ya Katiba kwa umma (Mteku 2023/2026), utakaotekelezwa kwa miaka mitatu kuhakikisha elimu ya Katiba inawafikia wananchi wote.

Mtazamo wa Dk Kabyemela

Akizungumzia maridhiano, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Matrona Kabyemela alisema kama maoni yanayotolewa yatazingatiwa, maridhiano yataiweka sehemu nzuri Serikali.

Hata hivyo, aliyataja maridhiano ndiyo yaliyoifungua Tanzania na kuwafanya watu wawe na fursa ya kutoa maoni.”Maridhiano ni hulka ya wanawake (Rais Samia) huwa hatupendi kutengeneza matabaka na uadui,” alisema.

Kuhusu elimu ya Katiba, alisema ni vigumu kuharakisha mchakato huo, ikiwa kuna ukweli kwamba wananchi wengi hawaijui.

“Katiba ni mkataba kati ya wananchi na watendaji, ni muhimu wakaelewa kinachobadilishwa” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi