Connect with us

Kitaifa

Kitanzi kipya cha mawaziri

Dar es Salaam. Changamoto katika wizara walizopangiwa mawaziri aliowateua Rais Samia Suluhu Hassan juzi, zinatajwa kuwa kitanzi kinachowasubiri baada ya kuwashinda watangulizi wao.

Licha ya changamoto hizo, wananchi nao wana matarajio lukuki kwa wateule hao kwenye utatuzi wa kero mbalimbali, kama kukatika kwa umeme, migogoro ya ardhi na matatizo mengine ya kijamii.

Mawaziri hao wapya na wengine waliohamishwa wizara, leo wataapishwa na Rais Samia katika Ikulu ndogo ya Zanzibar kuanza majukumu hayo.

Mzigo wa jumla ni jinsi mawaziri hao watakavyokwenda kutafsiri 4R za Rais Samia, ambazo amekuwa akizisisitiza wasaidizi wake kuzitumia katika kuwatumikia wananchi, akimaanisha kusameheana, kuvumiliana, kuleta mabadiliko na kujenga nchi kwa pamoja.

Katika mabadiliko hayo ya juzi, Rais Samia ameanzisha nafasi ya naibu waziri mkuu na kuifuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na badala yake kuunda wizara mbili mpya; ya Ujenzi na ya Uchukuzi.

Rais Samia amemteua Doto Biteko kuwa naibu waziri mkuu na waziri wa Nishati, ikiwa ni mara ya tatu kwa mamlaka ya Rais kuunda nafasi hiyo kwa nyakati tofauti, baada ya kushikwa na Dk Salim Ahmed Salim (1986 – 1989) na Augustine Mrema mwaka 1993.

Biteko, ambaye kitaaluma ni mwalimu mwenye shahada ya uzamivu, anachukua wadhifa huo kipindi ambacho Serikali inapambana na watendaji wanaofanya kazi kinyume cha utaratibu, kwa mujibu wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hivyo, ujio wake utakuwa msaada mkubwa kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye ndiye mtendaji mkuu wa Serikali, katika kukabiliana na kero mbalimbali kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa.

“Rais Samia amekuwa akilalamika kuwa watumishi hawatekelezi majukumu yao hadi viongozi wa juu watembelee maeneo husika.

“Kwa hiyo kama Waziri Mkuu Majaliwa akipata msaidizi atasaidia, akipita huku na mwenzake akapita kule, wanaweza kufuatilia mambo yaende haraka,” alisema Dk Richard Mbunda, mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mbali na hilo, katikakatika ya umeme ambayo imekuwa ikisumbua nchini, nalo litakuwa fupa gumu kwa waziri huyo, lakini madaraka yake yaliyoongezwa yanatarajiwa kusaidia kukabiliana nalo.

Pia analo la kupanda kwa gharama za mafuta, wakati mwingine likichangiwa na masuala ambayo hayako kwenye wizara hiyo, kama upungufu wa dola, kodi na mengineyo.

Kwa upande mwingine, Biteko anatarajiwa kuwa nguzo ya siasa eneo la Kanda ya Ziwa kuelekea chaguzi za mwaka 2024 na 2025 na kukabiliana na mtikisiko ulioachwa na Hayati John Magufuli, Rais wa awamu ya tano aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Migogoro ya ardhi

Eneo ambalo halijapata utulivu pengine kuliko yote ni la ardhi, kutokana na migogoro iliyopo kila kona, hivyo huo ni mtihani wa waziri mpya wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa.

Tofauti na mawaziri wengine ambao huanzia kuwa naibu mawaziri kabla ya kuwa waziri kamili, Silaa ameingia moja kwa moja barazani akitarajiwa kukabili vilivyo kero za makazi, upimaji wa ardhi na migogoro ya ardhi baina ya wananchi na wananchi na wananchi na taasisi za Serikali.

Mdau wa haki za ardhi, Bernard Baha alisema changamoto kubwa iliyopo mbele ya Silaa ni kutokupangwa kwa ardhi kunakosababisha manyanyaso kwa wananchi.

“Anatakiwa kulinganisha masilahi ya wananchi, wawekezaji na maeneo ya uhifadhi kwa sababu tumeona mara nyingi uzani unaelemea kwa wawekezaji na hifadhi, huku wananchi wakinyanyaswa,” alisema.

Akiwa mwanasiasa kijana mwenye shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara, stashahada ya uzamili ya sheria na shahada ya sayansi ya kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Silaa anatajwa kubebwa na uzoefu wa kuwa meya na mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya uwekezaji. Siku za karibuni alisimama kidete kutetea uamuzi wa Serikali katika mkataba wa uendeshaji wa bandari kati ya Tanzania na Dubai.

Zigo la Katiba

Vuguvugu la kudai Katiba mpya nalo linatajwa miongoni mwa masuala magumu yanayowakabili mawaziri hao, likiwa mabegani mwa Dk Pindi Chana.

Hili lilikuwa limepamba moto hata wakati wa mtangulizi wake, Dk Damas Ndumbaro aliyehamishiwa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.

Zaidi, anatakiwa kutoa ufumbuzi kuhusu nia ya Serikali ya kutoa elimu ya Katiba kwa miaka mitatu, kinyume na matazamio ya wadau.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Chacha Wangwe alisema ujio wa Pindi Chana utaleta nuru mpya ya upatikanaji wa Katiba na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha mchakato huo, hasa suala la utoaji wa elimu kwa miaka mitatu.

“Tunampongeza Rais Samia kwa kumwondoa Dk Ndumbaro kwenye wizara hii, tunampongeza Dk Chana kwa kuteuliwa kushika nafasi hii na tutampa ushirikiano, tunatoa wito kwake kutoa ratiba ya hatua za mchakato wa Katiba mpya ili kuondoa sintofahamu iliyotawala,” alisema.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Jukata, Deus Kibamba alisema upatikanaji wa Katiba mpya utaepusha wananchi kupitishiwa mambo ya hovyo.

Kibamba alisisitiza hakuna mwananchi aliyekataa Katiba na maneno yanayotolewa kuashiria wananchi hawapo tayari kwa mchakato huo, ni kauli ya viongozi walioshindwa.

Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Hebron Mwakagenda alisema “mchezo ni uleule, kubadilisha watu ni mbinu ya kuchelewesha, baadaye muda utatuishia tutaingia kwenye uchaguzi bila mabadiliko yoyote”.

Uwekezaji bandari

Licha ya kupunguziwa mzigo wa majukumu ya Wizaya ya Ujenzi na Uchukuzi akibakiziwa tu eneo la uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ndiye ataendelea kukabiliana na sakata la uwekezaji na uendelezaji wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai.

Makubaliano hayo ambayo yeye ndiye aliyetia saini kwa niaba ya Serikali, yamekuwa kiini cha mjadala mzito yalipowekwa hadharani, yakiwa yamewagawa wadau baadhi wakipinga na wengine wakikubali, hali iliyomlazimu atoe ufafanuzi wa mara kwa mara.

Mapato Tamisemi

Wakati Mohamed Mchengerwa akiondolewa Wizara ya Maliasili na Utalii na kupelekwa Ofisi ya Rais (Tamisemi), mambo anayotarajiwa kupambana nayo ni pamoja na ubadhirifu wa mapato unaodaiwa kufanywa na watumishi wa umma, bila kusahau mikwaruzano baina ya viongozi na watendaji wa Serikali, wakiwemo wakuu wa wilaya na mikoa, makatibu tawala na wakurugenzi wa halmashauri, ambayo imedaiwa ni tatizo sugu.

Mengine yanayomsubiri ni pamoja na changamoto ya miundombinu ya elimu, zikiwamo shule, vifaa vya kufundishia, hasa kutokana na ongezeko la wanafunzi pamoja na miundombinu ya afya, zikiwamo hospitali na vituo vya afya pamoja na uhaba wa watumishi.

Mizozo hifadhini

Kibarua kingine kigumu kinamkabili Angellah Kairuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii, ambako kuna mizozo ya kila mara kati mamlaka za Serikali na wananchi kuhusu uvamizi wa maeneo ya hifadhi na uingizaji wa mifugo.

Suala jingine katika eneo hilo ambalo joto lake halijapoa ni la kuwahamisha wananchi wanaoishi katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha kwenda Kijiji cha Msomera mkoani Tanga.

“Kuna kasi kubwa ya kuongeza maeneo ya hifadhi na kuwahamisha wananchi bila kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi,” alisema Baha alipotoa maoni katika eneo hilo.

Uraia pacha

Taarifa za kuteuliwa kwa Waziri January Makamba kutoka Wizara ya Nishati kwenda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zimesindikizwa mindaoni na kilio cha muda mrefu cha mahitaji ya uraia pacha.

Makamba ameambatana na aliyekuwa Naibu wake Wizara ya Nishati, Steven Byabato anayeendelea kuwa naibu wake Mambo ya Nje, ikidaiwa lengo ni kutaka kuiboresha wizara hiyo.

Uboreshwaji wa wizara hiyo umedhihirishwa na kauli ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka alipokuwa akitangaza mabadiliko hayo juzi.

“Hapa nisisitize, Mheshimiwa Rais ameamua kuimarisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuongeza Naibu Waziri na Katibu Mkuu. Kwa hiyo katika hii wizara kutakuwa na makatibu wakuu wawili, mmoja atakayeshughulikia kipekee masuala ya Afrika Mashariki,” alisema Kusiluka. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Magabilo Masambu alisema uteuzi wa Makamba hauna shaka, kwa sababu ataifanya kazi hiyo kutokana na uzoefu alionao.

“Aliwahi kuwa mwandishi wa hotuba wa Rais Jakaya Kikwete, maana yake kwa kiasi fulani ana uelewa wa masuala ya nje kwa sababu Rais anafanya kazi ndani na yanayoshirikisha mataifa ya nje, kwa hiyo anaweza kuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania na mataifa mengine hasa kutokana na pia na muda aliokaa serikalini,” alisema.

Akizungumzia uteuzi huo kwa ujumla, Dk Mbunda alisema licha ya Rais Samia kuona udhaifu wa watendaji wake, anapaswa kuwawajibisha badala ya kuwabadilisha na kuteua wengine.

“Pamoja na kuwa na nguvu ya kuteua na kutengua, Rais Samia amekuwa akilalamika bila kuchukua hatua. Huwezi ukategemea matokeo mapya kwa kuteua watu walewale kila mara,” alisema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi