Connect with us

Kitaifa

Siri 11 za mateso ya Rais Samia kwa Ma-RC, DC

Nimemsikiliza Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akifunga mafunzo ya siku sita ya wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa, Kibaha, Pwani, kisha nikairejea Sheria ya Mamlaka za Mikoa.

Nikapata wasaa wa kudurusu kitabu “Mzee Rukhsa” cha Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi, vilevile “My Life, My Purpose” – “Maisha Yangu, Kusudi Langu” cha Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa.

Haitoshi, nikaperuzi vema Dhana ya Hulka (Trait Theory), ambayo inafundishwa kwenye masomo ya saikolojia, vilevile kwa wasomi wa sayansi ya siasa.

Sasa, nipo kwenye wakati mzuri kuchambua kile ambacho Rais Samia alikisema, kwamba kuna hali ya kuleana baina ya wakuu wa mikoa na wilaya, pamoja na wakurugenzi wa halmashauri.

Yupo mtu anajiuliza, mkuu wa mkoa atawafanya nini wakuu wa wilaya ikiwa mamlaka ya uteuzi ni moja? Wakati fulani Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amewahi kuwaambia wakuu wa wilaya: “Mimi sio bosi wenu.” Alitaka wajue bosi wao ni Rais.

Rais Samia alishangaa, mkuu wa mkoa huwaapisha wakuu wa wilaya, lakini anashindwa hata kuwasimamisha kazi au kutoa taarifa kwa mamlaka za juu kwa hatua za kinidhamu. Ripoti za makatibu tawala wa mikoa huonesha hali ni shwari.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anapofanya ziara, ndiye humfikishia taarifa ya ubovu wa wakuu wa wilaya. Rais Samia alitafsiri hali hiyo kuwa kuna kuogopana baina ya wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri.

Nguvu ya Mkuu wa Mkoa

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 61 (4), imempa mamlaka na wajibu mkuu wa mkoa kusimamia shughuli zote za serikali katika mkoa ambao amepangiwa.

Kwa tafsiri hiyo, maana yake mkuu wa mkoa ni bosi wa kila mtumishi wa serikali ndani mkoa aliopangiwa. Ibara ya 61 (1) ya Katiba, inamtambulisha mkuu wa mkoa kama kiongozi wa Serikali. Kwa mantiki hiyo, mahali alipo Serikali inamtazama yeye.

Ufafanuzi huo tu pekee wa Katiba, unatosha kumfanya mkuu wa mkoa kutambua mamlaka yake juu ya kila ofisi ya Serikali kwenye mkoa aliopangiwa. Hivyo, mkuu wa mkoa ni bosi wa wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

Ni kweli, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wanateuliwa na Rais, hata hivyo, Katiba imempa hadhi kubwa mkuu wa mkoa. Yeye ndiye msimamizi wa shughuli za Serikali katika mkoa aliopo. Kusimamia shughuli za Serikali, maana yake ni kuwasimamia wafanyakazi wa Serikali.

Pitia pia Sheria ya Mamlaka za Mikoa ya mwaka 1977, sehemu ya pili, kifungu cha 5 (1, 2 na 3), mkuu wa mkoa anatambulishwa kuwa ndiye mwakilishi mkuu wa Serikali, msimamizi wa sheria na maagizo ya Serikali, vilevile ni mwezeshaji mkuu wa Serikali kwenye mkoa husika.

Kifungu cha 13 (3), Sheria ya Mamlaka za Mikoa, kinaeleza kuwa mkuu wa wilaya atapokea maagizo, mwongozo na maelekezo kutoka kwa mkuu wa mkoa. 13 (4), mkuu wa mkoa amepewa mamlaka ya kuteua mtu wa kukaimu nafasi ya mkuu wa wilaya kama kiti kipo wazi.

Ufafanuzi wa Katiba na Sheria ya Mamlaka za Mikoa, lengo ni kutuleta kwenye siri ya kwanza inayomtesa Rais Samia kwa wasaidizi wake, hususan wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri; hawasomi Katiba, sheria na miongozo ya kazi (instruments).

Wakuu wa mikoa hawatambui nguvu kubwa ya mamlaka ambayo wamepewa na Katiba pamoja na sheria. Kadhalika, wakuu wa wilaya hawajui hadhi ya wakuu wa mikoa kwa sababu hawasomi.

Nadharia ya hulka

Ndani ya somo la saikolojia, inatafsiriwa kama kipimo cha kung’amua hulka, hisia, fikra na uhusika wa kiongozi. Kuna siri saba zenye kumtesa Rais Samia kwa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi, katika uchambuzi wa nadharia hii.

Mwinyi kwenye “Mzee Rukhsa”, ameeleza kisa cha mgongano kwenye wizara, baada ya kumteua Augustino Mrema kuwa Naibu Waziri Mkuu, akiwa pia Waziri wa Mambo ya Ndani.

Kwa mujibu wa Mwinyi, mawaziri wengine walikuwa wakigombana na Mrema kwa kuona anaingilia mamlaka zao. Hili ni tatizo la kutotambua mipaka ya kazi.

Hii ni siri ya pili inayomtesa Rais Samia. Wasaidizi wake hawajui mipaka yao, kutoka mkuu wa mkoa, wilaya hadi wakurugenzi. Ni vigumu kuona matokeo bora katika hali kama hiyo.

Mkapa katika “My Life, My Purpose”, amesimulia mkasa wa aliyekuwa Waziri Fedha, Profesa Simon Mbilinyi na naibu wake, Kilontsi Mporogomyi. Jinsi walivyokuwa hawaelewani, ilimfanya awaondoe wote.

Hali kama hiyo ilitokea kwa Dk Hamisi Kigwangalla, alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, hakuwa akiiva na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda, hadi Rais John Magufuli aliingilia kati.

Hata Rais Samia mwenyewe amewahi kuisema migongano ya wasaidizi wake. Hii ni siri ya tatu; kuvimbiana. Kwa vile wote wameteuliwa na Rais, basi hayupo wa kumwonya mwenzake. Ndivyo ilivyo kwa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi.

Siri ya nne ni kukwepa wajibu. Mkuu wa mkoa anaona makosa ya wakuu wa wilaya na wakurugenzi, lakini hachukui hatua kwa sababu anaogopa kuonekana mbaya. Anasubiri rungu litoke juu.

Hii ni hulka iliyozama ndani kabisa kwenye maisha ya Watanzania. Mwenye bidii ya masomo anaitwa msongo. Mchapakazi na mwadilifu kazini jina lake mnoko. Wakuu wa mikoa wanakwepa kuwashughulikia wakuu wa wilaya na wakurugenzi, wasiitwe wanoko na wasionekane wasongo.

Hata kutoa taarifa hasi dhidi ya mfanyakazi mwenza, hata kama ni ya kweli, hutafsiriwa ni unoko au umbea. Si ajabu wakuu wa mikoa au makatibu tawala wa mikoa, wanaogopa kuitwa wanoko au wambea, matokeo yake kazi zinaharibika.

Siri ya tano ni uvivu. Wakuu wa mikoa hawafuatilii kikamilifu utendaji wa Serikali kwenye mikoa yao, matokeo ndio hayo, Waziri Mkuu akifanya ziara anabaini madudu ambayo hayaonwi na mkuu wa Serikali kwenye mkoa husika.

Siri ya sita ni woga. Mkuu wa mkoa hajui mkuu wa wilaya au mkurugenzi anazungumza nini kila siku na viongozi wa juu. Ama Rais, Waziri Mkuu au hata Waziri wa Tamisemi.

Hilo ni tatizo kubwa serikalini. Jambo ambalo limo ndani ya mamlaka ya mtu, anaogopa kuchukua hatua kwa sababu anahisi ataingia matatizoni na nguvu kubwa ya juu, endapo atamchukulia hatua wa chini yake.

Hili suluhu yake ni kama hivyo Rais Samia kusema, lakini kubwa na muhimu ni kuacha mifumo ifanye kazi kuliko maagizo ya mara kwa mara kwa njia ya simu. Mkuu wa mkoa hawezi kuwa mkali kwa mkuu wa wilaya ambaye anajua anazungumza kwa simu na kwa ukaribu na Rais.

Uadilifu unabeba siri mbili. Ya kwanza kutokana na uadilifu, lakini ya saba kwa mtiririko ni hii; bila shaka Rais Samia anafahamu kuwa wasaidizi wake hawaishi kwa kutegemea mishahara. Na kipato halali ni posho ambazo hupata kwa kazi za kutoka nje ya ofisi.

Wakurugenzi wa halmashauri ndio wanatajwa kuwa na mafungu mengi ya pesa, kwa hiyo hunyenyekewa hadi na wakuu wa mikoa na wilaya. Mazingira hayo kweli uadilifu utakuwepo?

Upo msemo “weka pesa kwenye kinywa chako.” Maana yake pesa ndio hutenda kuliko maneno. Rais Samia anaweza kulalamika kuwa wakuu wa mikoa hawafanyi chochote, kumbe pesa imewekwa kinywani.

Siri ya nane, lakini ya pili kwenye kipande cha uadilifu ni kwamba uwanja wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku umesheheni siri nyingi. Kila mmoja anajua ya mwenzake. Hapo ndio inakuja ngano ya “nani wa kumfunga paka kengele?”

Huyu anaogopa kumsemea mwenzake kwa sababu na yake yatasemwa. Anakwepa kuonekana kiherehere kufuatilia wa chini yake, maana yake pia yanajulikana. Ni mwendo wa kuogopana na kufichiana siri.

Uhuru wa kujitawala anaotoa Rais Samia kwa wasaidizi wake ni siri ya tisa inayomtesa kwa wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi. Anataka watu ambao hawana nidhamu ya kujisimamia, wajisimamie na yeye aone matokeo akiwa Ikulu.

Siri ya 10 ni kuwa Rais Samia anaongoza nchi kidemokrasia, akimfuatia Magufuli ambaye hakuamini demokrasia. Mathalan, Rais Samia, amewafukuza kazi aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Vijijini, Hanafi Msabaha na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Tatu Issike.

Sababu ya kuwatimua ni kuchepusha mradi wa maendeleo. Rais Samia alisema, Hanafi na Tatu, walikataa kupeleka mradi mahali ulipopangwa kwa sababu eneo hilo lina wapinzani wengi, badala yake wakapeleka kwingine ambako haukuwa umepangwa.

Kwa uamuzi huo, wanachama wa CCM ambao ni wakazi wa eneo ambalo lilinyimwa mradi, walirejesha kadi za chama. Rais Samia alisema, asingeweza kukubali kuona watu wanarejesha kadi za CCM, anawatimua.

Rais Samia alitanguliwa na Magufuli ambaye alipata kukaririwa mara kadhaa akisema “mnachagua wapinzani halafu nilete maendeleo?” Kwa Magufuli, kuchagua upinzani ni kosa la kutoletewa maendeleo. Samia anaamini wapinzani nao ni Watanzania na wanastahili maendeleo.

Kuna wakuu wa mikoa na wilaya bado wana misimamo ya wakati wa Magufuli, hili lazima limtese Rais Samia. Tukio la Hanafi na Tatu ni mojawapo kati ya mengi.

Siri ya 11 ni sheria. Anachotaka Rais Samia ni kuona wakuu wa mikoa wanawaadhibu moja kwa moja wakuu wa wilaya. Tatizo wakuu wa mikoa hawana mamlaka kisheria hata ya kuwasimamisha kazi wakuu wa wilaya. Aagize muswada wa mabadililo ya sheria uende bungeni ili apate anachotaka.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi