Kitaifa
Uchaguzi Mkuu 2025 bila Katiba mpya
Dar es Salaam. Mchakato wa Katiba mpya huenda ukakamilishwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kutokana na Serikali kuanzisha mkakati wa miaka mitatu wa kuelimisha wananchi utakaokamilika mwaka 2026 huku ikieleza kwamba suala la lini itakamilika si la Serikali, bali la wananchi wenyewe.
Hayo yalibainishwa Agosti 28, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro wakati wa kikao kilichowakutanisha mawaziri wakuu wastaafu, mawaziri wa sheria na wanasheria wakuu wastaafu na waliopo ili kupata maoni yao kuhusu mchakato wa Katiba mpya.
Hata hivyo, msimamo huo umepingwa na wadau wengine wa siasa wakisema kinachopaswa kufanyika ni kutoa ratiba jinsi ya kukamilishwa mchakato wa Katiba na sio kuanza kutoa elimu kwa umma. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemeafikiana na uamuzi huo kikisema wananchi wanapaswa kuelimishwa kwanza.
Mchakato wa awali wa Katiba mpya ulikwama mwaka 2014 wakati ukisubiri kura ya maoni baada ya kupitishwa Katiba Inayopendekezwa.
Wananchi wanaweza kuamua
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Dk Ndumbaro alisema Serikali haijipangii lini Katiba mpya ipatikane, bali wananchi ndiyo wanaweza kuamua lini ipatikane, viongozi wa Serikali ni watumishi wa wananchi.
“Watanzania wakisema wanataka Katiba mpya kesho na sisi tutafanya jitihada za kupata Katiba mpya kesho, wakisema wanataka Katiba mpya leo, na sisi tutafanya jitihada za kupata Katiba mpya leo,” alisema.
Waziri huyo alifafanua kwamba maudhui ya Katiba na lini ikamilike si suala la Serikali kuweka ukomo wa muda, bali ni suala la wananchi kuamua. Alisema namna ya wananchi kuamua na kuukwamua mkwamo wa Katiba, ndiyo mchakato unaoendelea sasa wa kushirikisha wadau.
Akizungumzia mapendekezo ya kupata Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu 2024/24, Dk Ndumbaro alionya Watanzania wasifanye kosa la kudhani kwamba Katiba inahusiana na kipengele kidogo cha uchaguzi.
Alisema Katiba inaanzisha mihimili mitatu, Serikali, Bunge na Mahakama na mle ndani yake kuna mambo mengi. Kwake yeye, alisema jambo la msingi kwenye Katiba ni haki za binadamu kwa kuwa Watanzania wote wanahitaji haki za binadamu.
“Kosa ambalo naliona ni wengi kuweka mbele mahitaji ya kisiasa kwenye Katiba wakasahau kwamba kuna mahitaji mengine mbali na ya kisiasa. Katiba inaongelea haki ya kupata elimu, ajira, uhuru wa kutembea. Hayo ni mambo ya msingi yanayopaswa kuangaliwa.
“Sasa ukisema tunataka Katiba kwa sababu ya uchaguzi, tunapokea hilo wazo lakini tuangalie yale ya msingi zaidi, na ili tupate ya msingi, tusifanye kosa la kufanya kazi chini ya shinikizo la ndani au la nje, tuandae Katiba mpya kwa mahitaji halisi ya Watanzania,” alisisitiza Dk Ndumbaro.
Dk Ndumbaro alisema wizara yake imeamua kulipa kipaumbele namba moja suala la elimu ya Katiba kwa wananchi kwa kile alichodai kwamba tafiti mbalimbali zinaonyesha zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hawaifahamu, wengine hawajawahi hata kuiona.
Alisema kutokana na umuhimu wa Katiba katika Taifa, Serikali inao wajibu wa kuhakikisha hiyo asiliamia 50 ya Watanzania wanaifahamu kwa kuwa wasipofanya hivyo, wataamini hata upotoshaji unaofanyika huko mitaani.
Kutokana na umuhimu huo, alisdema Wizara hiyo imekuja na Mkakati wa Taifa wa Elimu ya Katiba kwa Umma (Mteku 2023/2026) utakaotekelezwa kwa miaka mitatu ili kuhakikisha kwamba elimu ya Katiba inawafikia wananchi wote.
Waziri huyo alibainisha kwamba utoaji wa elimu ya Katiba utakwenda sambamba na mchakato wa Katiba kwa kuwa suala la elimu ni endelevu.
“Jambo hili tumelipa msukumo mahsusi tunaokwenda nao kwa miaka mitatu ili kuhakikisha Watanzania wote wanaijua Katiba yao,” alisema Dk Ndumbaro wakati akifungua mkutano wa viongozi wastaafu.
Awali, akizungumzia kikao hicho, Waziri mstaafu wa Sheria na Katiba, Dk Mary Nagu alisema endapo mabadiliko kwenye Katiba yatafanyika, basi yafanyike kikamilifu ili Katiba ya Tanzania ifanane na ya Marekani iliyodumu kwa miaka mingi huku ikifanyiwa marekebisho madogo madogo baada ya muda mrefu kupita.
“Mwaka 2026 tutakapoanza mchakato wa Katiba mpya, tuwe na unakika wa jambo ambalo litafanyika. Tuna nafasi ya kuangalia mambo gani tuyaweke, mambo gani yamepitwa na wakati tuyaondoe,” alisema Dk Nagu.
Kauli ya Mnyika, Zitto
Akitoa maoni yake kuhusu kauli ya Dk Ndumbaro, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema Rais anapaswa kumchukulia hatua waziri huyo kama hajamtuma kusema hayo aliyoyasema kwa kuwa Januari 3, 2023 (Rais) alisema mchakato wa Katiba utaendelea na akaahidi kuunda kamati na hakusema anaunda kamati ya kutoa elimu kwa miaka mitatu.
“Hii ni mara ya tatu Waziri wa Katiba na Sheria anatoa kauli potofu baada ya kauli ya Rais. Aliitoa Uwanja wa Majimaji aliposema (mchakato) utaendelea Septemba mwaka huu kwa kutoa elimu ili kujua mabaya na mazuri yake.
“Kauli nyingine ni aliitoa bungeni kwamba ametenga fedha wakati wa bajeti yake na kwenye majibu ya majumuisho. Kwa kiwango cha upotofu anachokisema, Rais anapaswa kumchukulia hatua,” alisema Mnyika.
Aliongeza kuwa kikao cha mawaziri na wanasheria wakuu wastaafu, Serikali ilipaswa kuwasilisha kwao muswada wa kuendeleza na kumaliza mchakato wa Katiba pamoja ratiba ili kupata maoni yao kujenga mwafaka na kuharakisha kuvipeleka kwenye Bunge linaloanza leo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe pia alisema mambo anayozungumza Waziri yanachelewesha na kukinzana na maagizo na maekelezo ya Rais, wanachokitaka ni ratiba ya utekelezaji.
“Sisi tumekwisha kufanya kazi kwenye kikosi kazi na kimetoa mapendekezo ya jinsi ya kuukwamua mchakato, tumetoa mapendekezo kwa ajili ya kuwezesha kuwa na Tume huru ya uchaguzi kabla ya mwaka 2024 na 2025 na tunachokitaka sisi ni kutoa ratiba ya utekelezaji wa kikosi kazi na ndiyo mahitaji yetu,” alisema Zitto na kuongeza:
“Kama ni elimu, ilishatolewa kupitia Kamati ya Jaji Warioba. Na huu mchakato unaoendelea wa mjadala juu ya mageuzi ya kisiasa kupitia makongamano na mikutano mbalimbali ni elimu tosha. Hakuna haja ya kupoteza muda tena. Twende na hatua zilizopendekezwa na Kikosi Kazi.”
Kwa upande wake Naibu katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Anamringi Macha alisema baadhi ya watu wanasukuma Katiba kwa lengo la kutafuta masilahi yanayowahusu lakini lazima Katiba iandaliwe kwa masilahi ya wananchi wote.
“Jambo langu la msingi, wananchi wanatakiwa kuelimishwa juu ya jambo linalokwenda kufanyika, Katiba ni ya wananchi, hivyo lazima wananchi wapate uelewa wa kutosha juu ya hilo jambo, Katiba si la kikundi cha siasa wala dini,” alisema.
Macha alisema tangu Katiba mpya ilivyokwama mwaka 2014 hadi sasa, wapo watu wengine umri umebadilika, hivyo lazima elimu itolewe kuwatosheleza.
Wanachelewesha mchakato
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe alisema wameshtushwa na kauli ya Waziri Ndumbaro na walianza kuwa na wasiwasi naye alipoanza kugusia suala la kutoa elimu kwa kuwa wanajua ni njia ya kuchelewesha Katiba mpya.
“Tunafahamu kabisa watu hujifunza kutokana na mchakato, tunaona kabisa hili jambo ambalo linaenda kuchezea maoni ya wananchi na kupoteza muda wa kupata Katiba mpya,” alisema mwanaharakati huyo.